1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Robinson ataka DRC izungumze na M23

3 Septemba 2013

Kauli ya Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Kanda ya Maziwa Makuu, Marry Robinson, anayekamilisha ziara yake katika mji wa Goma ya kutaka Kongo izungumze na M23 haikupokewa vyema.

https://p.dw.com/p/19abm
Mary Robinson, UN-Hochkommissarin für Menschenrechte, mit Raymond Tshibanda, Außenminister, bei einer Pressekonferenz in Kinshasa am 29.4.2013 Copyright: DW via Andrea Schmidt, DW Kisuaheli
Mary RobinsonPicha: DW

Akizungumza na waandishi wa habari katika mji wa Goma, hasa akigusia swala la mapigano baina ya waasi wa M23 na jeshi la serikali ya Kongo likiungwa mkono na kikosi maalumu cha Umoja wa Mataifa kilichopewa jukumu la kuingilia kati katika mapigano, Bi Robinson alisema vita hivyo vimezipunguza nguvu za M23 na kwamba wakati umewadia waasi hao kuweka chini silaha, na kwenda kwenye meza ya mazungumzo

''Ni dhahiri kwamba M23 wanapaswa kusimamisha mashambulizi kama ilivyotakiwa katika Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na pia nadhani kwamba mlango uko wazi kwa uwezekano wa kuchukuliwa hatua za kisiasa kuumaliza mgogoro huu."

Akijibu swali kuhusu ikiwa anaweza kuwa muwazi mbele ya viongozi wa Rwanda juu ya shutuma dhidi ya serikali ya Kigali kuwa inawaunga mkono waasi wa M23, Bi Robinson alisema atakwenda Kigali baada ya Kampala hapo tarehe 5 Septemba na kurudi Goma tarehe 6 Septemba pamoja na wenzake.

"Mimi sina shida ya kuzungumza moja kwa moja na viongozi wa Rwanda" kwani aliongeza Bi Robinson aliongeza kwamba Rwanda inamfahamu vizuri tangu alipoitembelea nchi hiyo kama rais wa Ireland.

"Nadhani kuwa ni muhimu kwa kila upande uliosaini mkataba wa Addis Ababa kuuheshimu na hivyo katika kanda hii. Nitalitamka hilo bila uoga kwa marais wote akiwemo Rais Paul Kagame. Naelewa kuwa kuna uwoga hapa kutokana na kuwa karibu na eneo hili kwa jeshi la Rwanda. Hilo nitalijadili na Rais Kagame.''

Kivu ya Kaskazini wakasirishwa

Makundi ya waasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Makundi ya waasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kwa upande wake. Gavana wa Mkoa wa Kivu ya Kaskazini, Julien Paluku Kahongya, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya mazungumzo na Bi Robinson, alisema kwamba haoni umuhimu tena wa kuendelea kwa mazungumzo ya Kampala.

"Kufuatia vitendo vya awali vya M23 na tulivyokuwa tunavitangaza, na kwamba inatupa mabomu katika miji mikubwa kama vile Goma na Gisenyi, hilo kwa sheria ya kimataifa ni ukatili wa kivita. Na sioni kwa upande wa Umoja wa Mataifa ambao wanaheshimu vyombo vya kimataifa kuiomba serikali halali kama vile ya Kongo kuzungumza na wahalifu."

Mwandishi: John Kanyunyu/DW Beni
Mhariri: Saumu Yusuf