1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ROME : Bush akutana na Papa Benedikt na Prodi

10 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBt8

Rais George W.Bush wa Marekani alikuwa nchini Italia kumuondolea mashaka Papa Benedikt wa 16 juu ya hali ya Wakristo wachache walioko nchini Iraq na kuondowa tafauti na Waziri Mkuu wa Italia Romano Prodi kufuatia miezi kadhaa ya mvutano kati ya nchi hizo mbili.

Bush ameutaja wasi wasi huo wa Papa kwa Wakristo wa Iraq katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Rome ikiwa haikutimia hata wiki moja tokea kuuwawa kwa kasisi wa Kikatoliki na wahudumu watatu wa kanisa nchini humo.

Bush amesema kwamba Papa ameelezea wasi wasi wake mkubwa kuhusu Wakristo nchini Iraq kwamba alikuwa na wasi wasi nadharia ya mabadiliko ya jamii nchini humo haitouvumilia Ukristo na kwamba amemundolea mashaka papa huyo kuwa wananchi wa nchi hiyo wanaheshimu katiba inayotaka kuwepo kwa uvumilivu wa kidini.

Mauaji ya kasisi kaskazini mwa Iraq hapo Jumapili iliopita yalifuatiwa siku baadae na kutekwa nyara kwa kasisi mwengine na watu watano wa parokia yake.

Papa Benedikt pia amemtaka Bush kutafuta ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo kwa mizozo ya Mashariki ya Kati.

Baadae Rais Bush alikutana na Waziri Mkuu wa Italia Romano Prodi ambapo kufuatia mazungumzo yao amewaambia waandishi wa habari kwamba mpango wa mjumbe wa Umoja wa Mataifa Marti Ahtisari kwa uhuru utakaosimamiwa wa jimbo la Kosovo kutoka Serbia unapaswa kusonga mbele.Serbia na Urusi zinaupinga mpango huo na Urusi imetishia kutumia kura ya turufu kuupinga katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Maelfu ya waandamanaji wamekusanyika katika mji mkuu wa Italia kupinga ziara hiyo ya Bush polisi ilipambana na baadhi ya waandamanaji hao na ilitumia gesi ya kutowa machozi kuvunja maandamano hayo.