1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rowhani ni rais mpya wa Iran

15 Juni 2013

Sheikh wa msimamo wa wastani Hassan Rowhani ametangazwa kuwa rais mpya wa Iran leo Jumamosi(15.06.2013) kufuatia ushindi wa moja kwa moja wa uchaguzi ambao unakomesha miaka minane ya wadhifa huo kuhodhiwa na wahafidhina.

https://p.dw.com/p/18qc1
Hassan Rowhani
Hassan RowhaniPicha: presstv.ir

Rowhani mwenye umri wa miaka 64,mpatanishi wa zamani wa suala la nuklea la Iran ambaye alikuwa akipigania kuwa na mawasiliano ya tija na mataifa ya magharibi amepata ushindi huo kwa kujizolea kura milioni 18.6 au asilimia 50.68 ya kura zilizopigwa.Akitangaza ushindi wa Rowhani,Waziri wa Mambo ya Ndani Mohammad Mostafa Najjar amesema watu milioni 36.7 au asilimia 72.7 wamepiga kura hapo Ijumaa.

Zaidi ya wananchi milioni 50.5 wa Iran walikuwa na haki ya kupiga kura kumchaguwa mtu wa kuchukuwa nafasi ya Mahmud Ahmadinejad ambaye katiba haimruhusu kuwania wadhifa huo baada ya kuutumikia kwa vipindi viwili mfululizo.Wingi wa kura alizopata kumemhakikishia kutokuwepo haja ya marudio ya uchaguzi huo,Meya wa Tehran Mohammad Baqer Qalibaf ameshika nafasi ya pili kwa kupata kura milioni 6.07.Msuluhishi wa sasa wa suala la nuklea la Iran Saeed Jalili ameshika nafasi ya tatu kwa kupata kura milioni 3.17.

Kilichochangia ushindi

Kujitowa kwa mwanamageuzi pekee kutoka katika kinyan'ganyiro hicho kumempa nafasi Rowhani ya kuzoa kura zote za wanamageuzi na watu wa msimamo wa kati na hiyo kuwapita sana wapinzani wake wa kihafidhina wenye misimamo mikali ambao wamegawika.

Hassan Rowhani baada ya kupiga kura yake Ijumaa (14.06.2013).
Hassan Rowhani baada ya kupiga kura yake Ijumaa (14.06.2013).Picha: AFP/Getty Images

Makamo wa rais wa zamani Mohammed Reza Aref alijitowa hapo Jumanne baada ya kuombwa kufanya hivyo na rais wa zamani Mohammad Khatami ambaye baadae naye akamuunga mkono Rowhani.

Rowhani anarithi uchumi ambao umeathirika vibaya kutokana na vikwazo vya Umoja wa Ulaya na Marekani vilivyolenga sekta ya mafuta na mabenki.

Uchaguzi huo wa Ijumaa ni wa kwanza tokea uchaguzi tata wa kuchaguliwa tena kwa Ahamedinejad hapo mwaka 2009 kusababisha maandamano makubwa ya mitaani na wafuasi wa wapinzani wake maandamano ambayo yamekandamizwa kwa kutumia nguvu na kusababisha maafa.

Hapo mwaka 2003 wakati Rowhani alipokuwa msuluhishi mkuu wa nuklea wa Iran chini ya utawala wa Khatami, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikubali kusitisha mpango wake tata wa kurutubisha urani.Mpango huo ulianzishwa tena miaka miwili baadae wakati Ahmadinejad alipochaguliwa kuwa rais kwa mara ya kwanza.

Ahadi za Rowhani

Iran imekuwa ikikwaruzana na mataifa makubwa duniani kutokana na mpango wake huo wa nuklea ambao mataifa ya magharibi yanashuku kuwa una lengo la kutengeneza silaha za nuklea.Serikali ya nchi hiyo imekanusha madai hayo lakini vikwazo vilivyowekwa kutokana na mzozo huo vimesababisha kutengwa kimataifa kwa nchi hiyo.

Moja ya vikao kuhusu mpango wa nuklea wa Iran.
Moja ya vikao kuhusu mpango wa nuklea wa Iran.Picha: picture-alliance/dpa

Wakati wa kampeni Rowhani ameahidi kuregeza vikwazo hivyo ambavyo vimesababisha matatizo makubwa ya kiuchumi kwa nchi hiyo.Mfumuko wa bei umefikia zaidi ya asilimia 30 na sarafu ya rial ya nchi hiyo thamani yake imeshuka kwa asilimia 70 huku ukosefu wa ajira ukizidi kuongezeka.Suala la uchumi lilikuwa mada kuu ya wapiga kura.

Rowhani pia anajivunia uhusiano wake na rais wa zamani wa msimamo wa wastani Akbar Hashemi Rafsanjani na amekuwa muangalifu katika uhusiano wake na kiongozi mkuu wa Iran Ali Khamenei ambaye ana usemi wa mwisho kwa masuala yote muhimu ya nchi hiyo likiwemo suala la mpango wa nuklea.

Uhusiano mpya na mataifa ya magharibi

Rowhani alikuwa mwaklishi wa Khamenei katika Baraza la Usalama la Taifa ambacho ni chombo cha juu cha usalama nchini Iran na amekuwa katibu wa baraza hilo kwa miaka 16 hadi hapo mwaka 2005.

Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei.
Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei.Picha: picture-alliance/dpa

Amesema hatosalimu amri kwa madai ya mataifa ya magharibi katika mazungumzo juu ya mpango wa nuklea wa Iran lakini ameahidi kufuata msimamo wa tija zaidi badala ya malumbano.Kufuatia Khatami kumuunga mkono Rowhani limeibuka vuguvugu la mtandao kwa wafanyakazi wa mitandao ya kijamii kuwahimiza wananchi wanaogoma kupiga kura wasipoteze kura zao na badala yake wampigie Rowhani.

Rowhani ameahidi kurudisha tena uhusiano wa kidiplomasia na Marekani ambao iliuvunja uhusiano huo baada ya ubalozi wake kutekwa na wanafunzi wa itikadi kali za Kiislamu nchini Iran.Pia ameahidi kwamba ubaguzi dhidi ya wanawake hautovumiliwa.

Rowhani ameowa na ana watoto wanne na ana shahada ya uzamili katika sheria kutoka Chuo Kikuu cha Glasgow cha Scotland.Amezaliwa mwaka 1948 katika mji wa Sorkheh kusini mashariki mwa Tehran.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri: Caro Robi