1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rufaa ya Abu Hamza yatupiliwa mbali

Mwadzaya, Thelma20 Juni 2008

Mahakama kuu nchini Uingereza imeamuru kurejeshwa Marekani kiongozi wa kidini aliye na msimamo mkali Abu Hamza al-Masri ili kujibu mashtaka ya ugaidi yanayomkabili.

https://p.dw.com/p/ENdP
Bunge la UingerezaPicha: AP

Kwa sasa Bwana al Masri anatumikia kifungo cha jela cha miaka saba baada ya kupatikana na hatia ya kuwashinikiza wafuasi wake kuwaua kikatili watu wasiokuwa waumini wa dini ya Kiislamu.Kwa upande mwingine wanasheria wake wanalalamikia hatua hiyo kwa madai kuwa ni ukiukaji wa sheria kwani endapo atapatikana na hatia atahukumiwa kifungo cha miaka 100 jela.


Agizo la kumrejesha mtuhumiwa huyo Marekani lilipitishwa na mahakama ya Westminster na kuidhinishwa na Waziri wa mambo ya Ndani wa Uingereza Bi Jacqui Smith mwezi Februari mwaka huu.Kwa mujibu wa majaji hao uamuzi huo kamwe haupingiki.


Kwa upande mwingine wanasheria wa Abu Hamza al Masri wanasisitiza kuwa ushahidi uliopatikana katika mazingira yaliyohusisha mateso ulitumika kufanikisha hatua ya kutimiza ombi hilo la kurejeshwa Marekani.Kulingana na wao kesi ya Abu Hamza sharti isikilizwe Uingereza ili kuepuka ukiukaji wa haki zake.


Uamuzi haupingiki


Jaji Igor Judge wa mahakama kuu ya Uingereza alipuuzilia mbali madai hayo na kusisitiza kuwa sharti sheria ya mwaka 2003 inayoruhusu hatua ya kuwarejesha watuhumiwa wa ugaidi katika nchi husika ili kujibu mashtaka idumishwe.


Kadhalika wanasheria hao wanadai kuwa muda mwingi umepita tangu shambulio hilo kutokea mwaka 2000.Jambo jengine linalozua utata ni kuwa endapo Bwana Abu Hamza al-Masri anapatikana na hatia huenda akahukumiwa kifungo cha miaka 100 jela nchini Marekani.



Abu Hamza al -Masri anakabiliwa na mashtaka 11 ya kuhusika katika shambulizi la kigaidi la mwezi Septemba mwaka 2001 nchini Marekani pamoja na kufadhili shughuli za kundi la kigaidi la Al Qaeda na wapiganaji wa Taleban.


Kiongozi huyo wa kidini aliye na umri wa miaka 50 ni imamu wa zamani wa msikiti wa Finsbury Park ulioko kaskazini mwa mji wa London. Itakumbukwa kuwa baadhi ya waumini waliofanya ibada kwenye msikiti wa Finsbury aliousimamia ni watuhumiwa wa kupanga njama ya shambulizi la kigaidi la mwaka 2001 Zacarias Moussaoui na Richard Reid.


Siku kumi na nne


Hamza vilevile anakabiliwa na mashtaka ya jaribio la kuanzisha kambi ya kutoa mafunzo ya ugaidi katika eneo la Bly,Oregon katika kipindi cha mwaka wa 1999 na 2000.Mzaliwa huyo wa Misri anayeshabikia shambulio la kigaidi la mwaka 2001 kwenye miji ya NewYork na Washington anakabiliwa na mashtaka ya kuhusika kupanga njama ya kuwateka watalii 16 wa mataifa ya magharibi nchini Yemen mwaka 1998.Mateka wanne kati yao …watatu wa Uingereza na mmoja wa Australia waliuawa pale wanajeshi wa Yemen walipovamia ngome ya wapiganaji hao.


Abu Hamza al Masri alihukumiwa mwezi Februari mwaka 2006 baada ya kupatikana na hatia katika mashtaka 11 kati ya yote 15 yaliyomkabili nchini Uingereza. Kiongozi huyo wa kidini anazuiliwa jela pia kwasababu ya uchochezi ulio na misingi ya ubaguzi wa rangi,kuwa na taarifa za uchochezi vilevile hati zinazoweza kutumiwa na magaidi.


Wanasheria wa Abu Hamza wamepewa siku 14 kuamua iwapo wataomba rufaa katika Baraza kuu la Bunge la Uingereza House of Lords.Endapo hawatachukua uamuzi huo au ombi hilo linakataliwa hatua ya kumrejesha Marekani itafuata katika kipindi cha siku 28.