1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rufani ya Karadzic, haijawasilishwa mahakamani bado.

Nyanza, Halima28 Julai 2008

Mahakama Maalum ya Uhalifu wa Kivita mjini Belgrade leo haijapokea rufani ya Radovan Karadzic kupinga kuhukumiwa katika Mahakama ya Umoja wa Mataifa ya Uhalifu wa kivita mjini The Hague.

https://p.dw.com/p/ElRQ
Aliyekuwa Rais wa zamani wa Waserbia Bosnia Radovan Karadzic, wakati wa utawala wake.Picha: picture-alliance/ dpa

Msemaji wa mahakama hiyo ya uhalifu wa kivita ya Serbia Ivana Ramic, ameelezea kutowasilishwa kwa rufani hiyo leo mahakamani na kwamba hakuna uwezekano tena wa kupelekwa leo, kutokana na muda wa kazi uliobaki wakati akitoa taarifa hii kubaki kidogo.

Awali wakili wa mtuhumiwa huyo Svetozar Vujacic alisema anauhakika kwamba mpango wake wa kucheleweshwa kuhamishwa kwa mteja wake katika mahakama ya uhalifu wa kivita ungefaulu, lengo likiwa kumuwezesha mteja wake kubaki nchini humo kwa siku chache zaidi.

Mtuhumiwa huyo wa mauaji ya halaiki katika vita vya Bosnia Radovan Karadzic, aliwaagiza wanasheria wake kujaribu kuchelewesha kuhamishwa kwake katika mahakama ya The Hague.

Wakili wa mshtakiwa huyo aliarifu kwamba anajaribu kumuwezesha mteja wake aweze kubakia Belgrade mpaka keshi jioni yatakapofanyika maandamano ya aliowaita Waserbia wote, na hadi pale familia yake itakapowasili mjini humo.

Kwa mujibu wa sheria mahakama ya Belgrade haina muda wa mwisho wa kusubiri rufani, na haijulikani itasubiri mda gani kufanya hivyo.

Hata hivyo Mwanasheria wa mtuhumiwa huyo amesema anafikiri kuwa ni muda wa siku tano mahakama kusubiri rufani.

Iwapo Rufani hiyo itawasilishwa mahakamani, majaji watakuwa na siku tatu kuamua rufani hiyo. na iwapo rufani hiyo itatupiliwa mbali, Wizara ya Sheria itasaini waranti na mtuhumiwa huyo atapelekwa The Hague.

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita inamshitaki kiongozi huyo wa zamani wa Waserbia Bosnia kwa mauaji ya halaiki na uvunjaji wa haki za binadamu wakati wa vita vya Bosnia.

Tayari Bwana Karadzic ameshasema kuwa atajitetea mwenyewe iwapo atafikishwa mahakamani hapo.

Kushtakiwa kwa Bana Karadzic kumekuwa kukipingwa vikali na Waserbia wenye msimamo mkali.

Katibu mkuu wa chama cha siasa kali za kizalendo nchini humo Aleksander Vucic alimkosoa Rais wa Boris Tadic kuhusiana na suala hulo.

Karadzic mwenye umri wa miaka 63 alikamatwa wiki iliyopita mjini Belgrade, baada ya zaidi ya miaka 10 ya kujificha kukamatwa.

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ICC inamtuhumu kiongozi huyo wa zamani kwa makosa ya mauaji ya halaiki, ukandamizaji wa haki za binadamu pamoja na kwenda kinyume na azimio la Geneva kuhusiana na vita, ambapo anadaiwa kuongoza mauaji ya kikabila wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Bosnia mwaka 1992 hadi 1995.

Karadzic pamoja na kamanda wa jeshi lake jenerali Ratco Mladic wanatuhumiwa kwa mauaji ya halaiki huko Srebrenica ambapo majeshi ya Serbia yaliwakusanya na kuwauwa baadhi ya Wabosnia Waislamu elfu nane wanaume pamoja na watoto na kuzikwa katika kaburi la pamoja Julai mwaka 1995.