1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda kufanya uchaguzi Jumatatu

Sekione Kitojo6 Agosti 2010

Siku ya Jumatatu , utafanyika uchaguzi wa rais katika nchi ndogo ya Rwanda nchi iliyopo katika eneo la Afrika ya kati.

https://p.dw.com/p/Oe7P
Rais Kagame akiwa katika mkutano wa kampeni ya uchaguzi.Picha: DW

Siku  ya  Jumatatu , utafanyika  uchaguzi  wa  rais katika nchi  ndogo  ya  Rwanda,  iliyopo  katika  eneo   la  Afrika ya  kati. Kwa  hivi  sasa   rais   Paul  Kagame  hukusanya maelfu  ya  makundi  ya  Wanyarwanda  katika   kampeni zake. Maelfu  ya  watu  hufurahia  na  kuimba  nyimbo  za kumsifu.  Kwa  watu  wa  Rwanda,  Kagame  ni kiongozi pekee  ambaye  anaweza  kuhakikisha   hali  ya  amani  na uthabiti.

Lakini  bado  linatanda  wingu  la  mauaji  ya  kimbari  ya mwaka  1994  katika  historia  ya  Rwanda. Na  Kagame anajiona  kuwa  ndie  binafsi  anaweza  kutatua   na kuhakikisha  kwamba  wingu  hili  jeusi  halirejei  tena nchini  humo. Hakuna  shaka  kabisa  kwamba  siku  ya Jumatatu   katika  uchaguzi  wa  rais  atashinda  kwa asilimia  90. Lakini  pia  amevitendea  ukatili  mkubwa baadhi  ya  vyama  vya  upinzani , na  baadhi  kuvifanya kuwa  vibaraka  wake  katika  demokrasia   inayoonekana kuwa  kama  mchezo  wa  kuigiza. Vyama  vya  upinzani binafsi  vimesalim amri, na  kumuunga   mkono  Kagame.

Inasikika   kama  ni  tamasha  la  muziki katika  kampeni  za uchaguzi  za  Kagame. Katika  eneo  kubwa  la wazi   baina ya vilima  vikubwa,  mashariki  ya   Rwanda,  kuna  maelfu ya   watu  waliokusanyika.  Wamevalia  fulana  zenye picha ya   Kagame na  kupepea  vibendera  vya  rangi  ya  buluu, nyeupe na  nyekundu,  rangi  za  bendera  ya  chama tawala   nchini  Rwanda, FPR. Na  wanaimba   wimbo  wa kumsifu  Kagame.

Hali  ni  ya  joto  majira  ya  mchana. Na  watu  wanatoka jasho, na  wana  kiu. Katika   eneo  lote,  watu  hawa wamekuja  hapa   tangu  asubuhi  na  mapema wakisafirishwa  kuja  katika  eneo   hili  kwa  mabasi. Watoto, wanawake  wakiwa  na  watoto, wazee  na   wasio jiweza, vilema  wakiwa  katika  vigari  vya  kujisukuma. Mbinyo kwa  jamii  ni  mkubwa , nchini  Rwanda ni  wajibu kwa  kila  mtu kuwa  mzalendo na  kumuunga  mkono Kagame, ambaye  anajiona  kuwa  ndio mtatuzi wa  wingu jeusi  la  mauaji  ya  kimbari  mwaka  1994,  na  pia  kama mtu  anayeweza  kuhakikisha  makabila  mawili  ya Wahutu  na  Watutsi  kuishi  pamoja, anasema  Taye Manzi. Mzee  huyu  yuko  katika  kundi  kubwa  la  watu  na amevaa   fulana  yenye  picha  ya  Kagame   na  kofia.

Ametuletea  amani,  na  kuijenga  nchi  yetu. Yeye  ni pekee  ambaye  ameweza  kufanikisha  kuwaunganisha watu  wetu. Anawasaidia  vijana  na  wanawake. Tunafahamu kuwa  demokrasia  ni  hatua. Na  tuna matumaini  kwamba  atafanikisha kile  alichotuahidi  pamoja na  mambo  mengine  zaidi.

Kagame  binafsi  anazungumzia  mengi  kuhusu demokrasia katika uchaguzi  huu. Imekuwa  ndio  mada kuu, kwa  kuwa  jumuiya  ya  kimataifa  haikubaliani  na demokrasia  yenye  mapungufu. Kagame  alichaguliwa kwa  asilimia  90 miaka  saba  iliyopita. Hakuna  mtu mwenye  kutia  shaka , kwamba  mara  hii  atapata   zaidi ya  asilimia  90  ya  kura . Lakini  watu  wanamhakikishia kupata   asilimia 100  katika  mikutano  wa  hadhara. Na Kagame  anasema  katika  moja  ya  hotuba  zake  kuwa asilimia  100 pia  ni  demokrasia. Kwa  jinsi  hali inavyoonekana  nchini  Rwanda   hivi  sasa  ni  mchezo  wa kuigiza  wa  vyama  vya  siasa  katika  demokrasia. Kwa sababu  hata  vyama  vya  upinzani  vinamuunga  mkono rais.

Kusini  mwa   Rwanda  chama  cha   Kiliberali  kinafanya mkutano  wake  wa  hadhara. Kiasi  cha  watoto  20 wanacheza  katika  uwanja , watu  wachache wamehudhuria  na  wanataka  kupewa   fulana hizi zinatolewa  bure. Chama  cha  Kiliberali  kina uwakilishi bungeni. Kinatumiwa  na  chama  tawala  cha  rais Kagame  ili  kuonyesha  kuwa  kuna  demokrasia, anasema makamu   mwenyekiti   wa  kundi  la  vyama  vya  eneo hilo, ambae  kutokana  na  hofu  hakutaka  jina lake lijulikane. Yuko  kiwanjani  hapo  na  anagawa  fulana  za rangi  ya  kijani.

Hatuna  wapiga  kura  wengi , kama  unavyoona  leo  hapa. Tumefadhiliwa  na  chama  tawala  cha  FPR. Katika chama  chetu  tunafanya kazi  kwa  ushirikiano. Kila tunachokifanya ni  lazima  kiwe  kimeidhinishwa  na  FPR. Hayo  ndio  makubaliano. Tunafurahi  kwa  hilo. Uchaguzi kwetu  sisi  hauna  tatizo.

Victoire Ingabire
Victoire Ingabire,mmoja wa wanasiasa wa upinzani aliyewahi kukamatwa.Picha: AP

Nchini  Rwanda  wapinzani  wanahofu dhidi  ya kupambana  na  Kagame  na  kutoa mtazamo  mbadala. Kwa  sababu  kile  ambacho  wanasiasa  wa  upinzani kilichowatokea  katika  miezi  iliyopita  ni  ukatili  wa  wazi. Frank  Habineza  yuko  katika  ofisi  yake  ndogo  na  ana hofu  kubwa. Hawezi  hata  kutembea  mitaani. Habineza ni  mwenyekiti  wa  chama  cha  kijani. Amejaribu  katika miezi  iliyopita , kukiandikisha  chama  chake. Wafuasi wake  ni  wafuasi  wa  zamani  wa  chama  cha Kagame, ambao  wamekihama. lakini  sasa  Habineza  ana wasiwasi na  maisha  yake. Mmoja  wa  wawakilishi  wake  amekutwa amekatwa  kichwa wiki  tatu  zilizopita.

Hali  yetu  ilikuwa  si  nzuri  tangu  kabla  ya  hapa, lakini hivi  sasa  hali  ni  mbaya  sana. Tulijaribu  kukiandikisha chama  chetu  mwezi  Mei. Hatukupata  jibu  lolote  kutoka serikalini. Siku  chache  baadaye,  makamu  wa  chama chetu  aliuwawa. Tuna matumaini kwamba  baada  ya uchaguzi  huu,  hali  itakuwa  nzuri.  Hatukati  tamaa. Tunajitayarisha  na  uchaguzi  ujao  mwaka  2013. Hata hivyo,  inatisha. Kwa  sasa  tunalalamikia  kuhusu  hali  ya kutokuwa  na  demokrasia, kwa  hivi  sasa  tuna  hofu  ya maisha  yetu. Naomba  nifungwe  tu , na  sio  kupoteza maisha.

Ndio  sababu Habineza  ameamua,  kukimbilia  nje  ya nchi. Hasa  kwa  wakati  huu  wa  uchaguzi. Anataka kupata  hifadhi  ya  kisiasa  nchini  Ujerumani. Mapambano ya  uchaguzi  yanaendelea  nchini  Rwanda.

Mwandishi : Simone Schlindwein / ZR / Sekione  Kitojo.

Mhariri : Othman  Miraji.