1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saa kubwa ya majira ya waislam kujengwa Mecca

10 Agosti 2010

Waislamu kote duniani hatimae wataweza kurekebisha saa zao kulingana na majira mapya, wakati arkabu za saa kubwa kabisa duniani itakapoanza kufanya kazi huko Mecca Saudi Arabia

https://p.dw.com/p/Ohat
Jengo la Burj Khalifa nchini Dubai ambalo ni refu kuliko yote dunianiPicha: picture-alliance/ dpa

Saudi Arabia inatumai kwamba sura nne za saa hiyo juu ya msikiti mkubwa wa Makka kutoka kile kinachotarajiwa kuwa jengo refu kabisa duniani,litaufanya mji huo kuwa mahala mbadala pa kuzingatia majira ya saa, badala ya majira ya hivi sasa ya Greenwich ambayo ni tafauti ya muda wa saa 3 na Afrika mashariki.

Saa hiyo kubwa nchini Saudi Arabia inatarajiwa kuanza kazi kwa kipindi cha majaribio cha miaka mitatu katika wiki ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani unaoanza leo au kwa wengine hapo kesho Agosti 12.

Urefu wa jengo hilo kwa mujibu wa Shirika la habari la Saudia, utafikia mita 601 na hivyo kuwa jengo la pili refu kabisa duniani, ikilitangulia lile la Taiwan lenye urefu wa mita 509. Jengo refu kuliko yote duniani ni Burj Khalifa mjini Dubai lenye urefu wa mita 828.

Wafanyakazi wakiislamu wenye ujuzi wapatao 250 wamekuwa wakikamilisha kazi za kuweka saa hiyo kubwa.

Mkaazi mmoja wa Makka amesema kila mtu anahamu ya kuiona saa hiyo, ingawa hakuna maelezo juu ya saa hiyo ,ufundi au matumizi yake,yaliotolewa hadi sasa.Saa hiyo imepambwa kwa upanga wakijani, nembo ya falme ya Saudi Arabia.

Saa hiyo inatimiza ndoto ya baadhi ya Waislamu kutaka paweko na saa mbadala itakayochukua nafasi ya saa inayotumika kwa majira duniani ya Greenwich Mean Time - GMT. Saa hii mpya mjini Mecca itajulikana kama Mecca Mean Time-MMT. Itakuwa kubwa kwa upana mara sita zaidi kuliko ile maarufu ya Big Ben ya mjini London, ikiwa na maandishi ya jina la Mwenyezi Mungu "Allah" kwa lugha ya kiarabu, iking´arishwa na mwanga wa taa ndogo ndogo milioni mbili. Mwangaza wa saa nyengine 16 utamulika na kutoa nuru umbali wa mita 16.

Halikadhalika mradi huu ni sehemu ya mpango wa serikali ya Saudia kuujenga mji wa Makka uweze kupokea mahujaji hadi milioni 10 kila mwaka, kutoka idadi ya sasa ya milioni tatu.

Hilo ni muhimu kuwapa nafasi kubwa zaidi Waislamu, kuweza kuhiji kwa wingi, kama inavyotakiwa kufanya hivyo alau mara moja maishani kwa kila mwenye uwezo.

Mmisri mkaazi wa jiji la Makka Ahmed Haleem, anasema ni jambo la kujivunia kwani wakati miaka yote watu walikuwa wakitegemea majira ya saa ya magharibi ya Greenwich, sasa waislamu wanaweza kutumia majira yao wenyewe kwa kuzingatia saa ya Makka. Akiomba awe mmoja wa wale watakaoshuhudia kufunguliwa rasmi kwa saa hiyo kubwa, Hallem alitamka " itakua ni heshima na furaha kujaaliwa kuwa mahala hapo wakati huo.

Mwandishi:Mohammed Abdul-Rahman/afp

Msomaji:Aboubacary Liongo

Mhariri:Josephat Charo