1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SADC yakutana tena kuhusu Zimbabwe

Kalyango Siraj27 Oktoba 2008

Tsvangirai atishia kujiondoa katika serikali ya umoja wa taifa

https://p.dw.com/p/FhZe
Thabo Mbeki,kushoto, na Mugabe, kulia.Je! SADC itafanikiwa Zimbabwe?Picha: dpa - Bildfunk

Viongozi wa kanda ya kusini mwa Afrika SADC wanakutana tena jumatatu mjini Harare Zimbabwe kwa mazungumzo yenye nia ya kuunusuru mpango wa kugawana madaraka kati ya chama rais Robert Mugabe cha ZANU PF na cha mpinzani wake mkuu cha Movement for Democratic Change MDC cha Morgen Tsvangirai.Mpango huo umekwama kutokana na ugawanaji wa wizara muhimu.

Mkutano huo wa mjini Harare unafanyika chini ya tisho kuwa waziri mkuu mteule, Morgen Tsvangira wa chama cha MDC, anaweza akajiondoa katika makubaliano ya kugawana madaraka.

Makubaliano hayo yalifikiwa wiki sita zilizopita,lakini hadi sasa wahusika wakuu,Mugabe na Tsvangirai baado wanavutana kuhusu wizara gani ichukuliwe na chama kipi. MDC kinamlaumu Mugabe kwa kukilimbikizia chama chake cha ZANU -PF wizara zote muhimu.Mapema wiki jana Tsvangirai alipinga taarifa kuwa Mugabe amezitenga wizara za Ulinzi,mambo ya ndani na fedha kwa chama chake.

MDC kinataka kupewa usimamizi wa wizara ya mambo ya ndani ambayo inahusika, miongoni mwa mengine,na utoaji wa vibali vya kusafiria.Tsvangirai wiki iliopita alisusia mkutano wa SADC uliokuwa Swaziland, kama ishara ya kulalamika kupinga hatua ya kupewa hati ya kusafiria dakika za mwisho.

Hata hivyo msemaji wa chama cha MDC,Nelson Chamisa,amesema mwishoni mwa juma kuwa, suala sio tu wizara moja ya mambo ya ndani lakini pia kuna takriban wizara 10 ambazo zinahitaji ufafanuzi.Akaahidi kuzijadili kupitia mpatanishi katika mazungumzo ya leo jumatatu.

Makubaliano ya Septemba 15, chini ya usimamizi wa rais wa zamani w Afrika Kusini Thabo Mbeki, ulipelekea Tsvangirai kuteuliwa kama waziri mkuu wa nchi hiyo na mwenzake Arthur Mutambara, wa chama kilichojitenga na MDC ya Tsvangirai, kuwa naibu waziri mkuu.

Mapema mwezi Septemba, viongozi hao walikubali kumuita mpatanishi kumaliza tofauti zao.Lakini mpatanishi alishindwa na mpira kuutupia jumuiya ya mataifa ya kusini mwa Afrika SADC.Lakini jumuiya nayo ilishindwa kufanikisha suluhu kutokana na Tsvangirai kususia kikao.

Na jana jumapili kiongozi huyo alimuonya mpatanishi Mbeki kuwa endapo hataacha upendeleo atajiondoa.Katika mkutano wa leo wa SADC wa mjini Harare,Mbeki ataeleza amefikia wapi katika upatanishi wake.

Katika mpango wa awali wa kugawana madaraka,MDC cha Tsvangirai kilipewa wizara 13, kile cha Mutambara wizara 3 na ZANU -PF cha Mugabe wizara 15.Hata hivyo kizungumkuti kikawa makubaliano hayakufafanua ni wizara ipi itachukuliwa na chama gani.

Na juhudi za sasa za SADC zina nia ya kuwasiaidia watu wa Zimbabwe kupata suluhu kutokana na changamoto walizonazo kwa sasa za kisiasa pamoja na kiuchumi.