1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Safari ya muziki ya Mzungu Kichaa

Iddi Ismail Ssessanga7 Oktoba 2014

Ni mzungu, Mdeni, na anapokuwa jukwaani, huzungukwa na Watanzania wanachama wa bendi yake, lakini baada ya nyimbo chache katika maonyesho ya moja kwa moja ya mzungu kichaa, tayari ushasahau rangi ya ngozi yake.

https://p.dw.com/p/1DRY1
Mzungu Kichaa Musiker Tansania
Espen Sorensen maarufu Mzungu Kichaa.Picha: DW/I. Ssessanga

Espen Sorensen almaarufu Mzungu Kichaa, alizaliwa nchini Denmark na kukulia Tanzania ambako alizamia katika utamaduni wa taifa hilo na muziki wa kiafrika kwa ujumla, kiasi kwamba alikuja kutambuliwa na kuheshimiwa kama mmoja wa waasisi wa muziki wa Bongo Flava, ambao ni aina ya muziki wa Kitanzania wa miondoko ya hiphop unaochanganya mahadhi ya kiarabu, na kuhusisha pia vionjo vya afrobeat na dancehall. Sorensen ameishi zaidi ya nusu ya maisha yake nchini Tanzania, na hii imechangia kiasi kikubwa kuunda maisha yake.

Mwishoni mwa miaka ya 1990 Mzungu Kichaa alikuwa miongoni mwa wasanii wa kwanza kurekodi muziki wao katika studio za Bongo Records, wengine wakiwa Juma Nature, TID, Mangwaire na Professor Jay. Wakati huo ndiyo pia alipata jina lake la kisanii la Mzungu Kichaa. Hakutokezea miongoni mwa wasanii chipukizi wakati huo, lakini alifanya baadhi ya chorasi katika nyimbo kadhaa mwaka 2001.

Mzungu Kichaa alifanya onyesho kubwa lililowavutia vijana wa mjini Hamburg.
Mzungu Kichaa alifanya onyesho kubwa lililowavutia vijana wa mjini Hamburg.Picha: mediaserver.hamburg.de/C. Spahrbier

Baadaye alikwenda nchini Uingereza, ambako alifanya shahada yake ya muziki na elimu ya utamaduni wa watu. Baada ya kumaliza shahada yake ya uzamili katika masuala ya Afrika, Sorensen alirudia fani ya muziki na kuanzisha kikundi kinachoitwa Effigong mwaka 2006. Mwaka 2008 aliamua kwenda kivyake, na alifanyikiwa kutoa rekodi yake ya kwanza mwaka 2009 chini ya lebo ya Carvan Records.

Kuwepo kwake kwenye jopo la majaji wa Bongo Star Search, kipindi kikibwa cha kusaka vipaji vya muziki nchini Tanzania halikuwa jambo baya, ingawa wengi walimhusisha na Muingireza alieshiriki mashindano, akiimbia nyimbo za msanii 20 Percent.

Ndiyo, ni mzungu na Mdeni, lakini pia amekuwa Mwafrika zaidi kufikia wakati huu. Sorensen alikuja Tanzania na wazazi wake waliokuwa wanafanyakazi katika nyanja ya ushirrikiano wa maendeleo wakati huo akiwa na miaka sita. Akiwa nchini Tanzania, alijifunza kuzungumza Kiswahili kwa ufasaha, na kisha alijihusisha katika muziki.

Maisha nchini Zambia

Baada ya kukaa Tanzania kwa muda mfupi, wazazi wa Sosrensen walihamia nchini Zambia ambako anasema alijifunza maisha hasa ya kiafrika, kwa sababu walikuwa wkiishi kijijini, na wakati huo uchumi wa Zambia ulikuwa chini sana, hivyo maisha yake kama mtoto yalikuwa ni ya kawaida sana.

Kijijini alikokuwa akiishi Sorensen hakukuwa na wazungu wengine, na hii ilimpa fursa ya kujichanganya na watoto wenzake wa kiafrika na bahati nzuri wazazi hawakuwa wakiwazuwia yeye pamoja na mdogo wake kucheza na hivyo aliweza kushirki michezo yote ya mtoto wa kiafrika kama vile kuwinda ndege kwa manati, kuvua samaki, na hata kuiba asali usiku kwenye miti.

Ilikuwa mwaka 1995 ambapo Sorensen alihamia Tanzania moja kwa moja na kuanza safari yake ya muziki. Ni msanii maarufu nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla, akiwa amefanya maonyesho kadhaa katika kanda hiyo tangu alipoanza kujitegemea mwaka 2008. Sorensen, ambaye ni balozi mwenye juhudi wa tasnia ya muziki wa kisasa wa Tanzania anasema safari yake ya kimuziki imekuwa ndefu na iliyojaa vikwazo, ikiwa ni pamoja na kukataliwa na baadhi ya mapromota wazungu kutokana na ngozi yake nyeupe.

Mzungu Kichaa Musiker Tansania
Mzungu Kichaa akifanya mahojiano na DW.Picha: DW/I. Ssessanga

Nyumbani ni nyumbani

Kama raia wa Denmark, Sorensen pia hajakusahau nyumbani, ambako amefanya maonyesho kadhaa akiwa pamoja na bendi yake. Amechaguliwa mara mbili kugombea tuzo za muziki wa kimataifa nchini Denmark - mwaka 2009 katika kategoria ya Albamu bora ya dunia, kwa Albamu yake ya "Tuko Pamoja"na mwaka 2012 wimbo wake wa "Twende kazi" ulichaguliwa kugombea tuzo ya wimbo bora wa dunia. Na mwaka huu, Sorensen na bendi yake watakwenda kufanya onyesho la sita nchini humo.

Sorensen na bendi yake wamefanya maonyeso makubwa pia katika miji ya Hamburg na Bremen kwa kushirikiana na msanii mwingine wa miondoko ya Raggae Manfred, kama sehemu ya wiki ya ushirikiano kati ya miji ya Hamburg na Dar es Salaam, ambapo moja ya maonyesho hayo lilitangazwa moja kwa moja kupitia redio na baadhi ya sehemu za onyesho hilo zilitangazwa na Televisheni. Wakati wa ziara hiyo, wawili hao walitemebelea studio ambako walirekodi wimbo wao wa "Twajiachia.

Sorenseni pia amewashikirisha wasanii maarufu kwenye nyimbo zake, kama vile Profesa Jay, Juma Natura, Lady Jay Dee na Mwasiti wa nchini Tanzania, na pia amemshirkisha mwanamuziki maarufu wa Kenya Dela katika wimbo wake wa "African Hustle". Sorensen anasema ushirikishaji au colabo katika muziki ni hatua muhimu kwake katika kujenga uhusiano kati ya wanamuziki nje ya mipaka ya mataifa, katika jitihada zake za kuimarisha sekta ya muziki Afrika Mashariki, na anasema yuko tayari kutoa mchango zaidi kuhakikisha lengo linafikiwa, lakini anasistiza umuhimu wa wasanii kuungana.

Kusikiliza makala kuhusu msanii Mzungu Kichaa bofya alama ya spika za masikioni hapo chini.

Mwandishi: Iddi Ssessanga
Mhariri: Mohammed Khelef