1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Safari za ndege zaanza barani Ulaya

Kabogo Grace Patricia21 Aprili 2010

Safari hizo zimeanza baada ya mamlaka za ndege barani humo kulegeza masharti za kuzuia safari za ndege.

https://p.dw.com/p/N1bu
Ndege zikiwa katika uwanja wa ndege wa Munich, Ujerumani.Picha: AP

Siku sita baada ya mripuko wa volkano nchini Iceland kusababisha sehemu kubwa ya anga barani Ulaya kufungwa, mamlaka za usafiri wa ndege barani humo jana zilianza kupunguza marufuku ya safari za ndege. Shirika linaloratibu safari za ndege barani Ulaya-Eurocontrol, limesema kuwa nusu ya safari zake za ndege 28,000 za kila siku zilianza kuruka kama kawaida kuanzia hiyo jana.

Shirika la usalama wa anga la Ujerumani-DFS limeongeza marufuku ya safari zake za ndege angalau hadi asubuhi ya leo. Lakini shirika hilo limelipa ruhusu shirika la ndege la Lufthansa kusafirisha abiria waliokwama kwa masharti ya kufanya chini ya asilimia 15 ya safari zake za kawaida.

Maafisa wa anga nchini Uingereza wametangaza kuwa ndege zinazoingia na kutoka nchini humo zimeanza safari zake. Hata hivyo Denmark, Ireland na Sweden ni miongoni mwa nchi ambazo bado zimeendelea kufunga anga zao.