1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Safari za ndege.

Abdu Said Mtullya22 Aprili 2010

Wakati baadhi ya viwanja vya ndege vimefunguliwa, bado wapo abiria waliokwama.

https://p.dw.com/p/N2qZ
Ndege zimeanza tena safari.Picha: AP

Wakati baadhi ya nchi barani Ulaya zimeanza  tena safari za ndege baada ya kufungwa kwa muda kutokana na kutanda kwa jivu la mlima wa volkano ulioripuka nchini Iceland,baadhi ya safari hizo kwa  viwanja vya ndege vya Norway na Sweden,zimeendelea kusimamishwa.

Baadhi ya abiria barani humu nao wakiwa bado hawajapata uhakika wa safari zao,wamiliki wa ndege hizo wameanza kushinikiza Serikali,kuwalipa fidia kwa ajili ya hasara kubwa walizopata kutokana na kadhia hiyo.

Waongoza ndege kwa baadhi ya maeneo ya nchi za Sweden na Norway,wamesema kuwa njia ya anga katika mji mkuu wa Stockholm itaendelea kuwa wazi,lakini maeneo ya miji ya kusini mwa nchi ya Sweden ya Goteborg na Malmo,na maeneo kadhaa ya magharibi na kaskazini yataendelea kufungwa kutokana na jivu hilo.

Msemaji wa waongoza ndege wa Sweden Bjorn Stenberg ameeleza kuwa mabadiliko ya upepo unaovuma katika anga la nchi hiyo,limesababisha mtawanyiko wa jivu hilo kuelekea zaidi maeneo ya magharibi ya nchi jirani ya Norway.

Taarifa hizo za kutandao kwa jivu la volkano,pia zimethibitishwa na waongoza ndege nchini Norway,ambao nao wameelezea kuwa, uwanja wa ndege wa mji Mkuu wa Oslo utaendelea kuwa wazi kwa ajili ya kuendelea kutoa huduma za ndege kama kawaida,lakini njia ya anga ya magharibi ya Norway imefungwa tena,ikiwemo viwanja vya Stavanger na Bergen.

Pia imeelezwa kuwa maeneo mengi ya anga nchini Finland,nayo yataendelea kufungwa,ukiwemo uwanja uliopo mji mkuu wa Finland wa Helsinki,wakati anga la nchini Denmark katika nchi hizo za skandinavia litaendelea kuwa wazi.

Wakati hayo yakiendelea,wiki moja baada ya mripuko huo wa vilkano kutokea,na kusababisha hali mbaya zaidi kuwahi kutokea duniani tangu kumalizika kwa vita ya pili ya dunia,wamiliki wa mashirika ya ndege wameanza kuhesabu hasara walizopata kutokana na kadhia hiyo,na kueleza nia yao ya kutaka kujuwa nani atabeba mzigo wa hasara hizo.

Jumuiya ya kimataifa ya usafiri wa anga  IATA,Imeeleza kuwa hasara ya jumla iliyopatikana kutokana na tatizo hilo la jivu kutanda angani,imeyagharimu mashirika ya ndege kiasi cha dola bilioni 1.7,sawa na kupoteza dola milioni 400 kwa siku.

Pia,jumuiya hiyo imeeleza kuwa kufungwa kwa njia za anga kulizingatia zaidi nadharia badala ya kuzingatia hali halisi.

Giovanni Bisignani,Kiongozi wa Jumuiya hiyo inayosimamia maslahi ya wamiliki wa ndege,ameushutumu uamuzi wa Serikali kutangaza kufungwa kwa njia za anga kutokana na mtawanyiko wa jivu hilo la volkano.

Ametolea mfano wa hasara ya kiasi cha dola bilioni 9.4 ambazo sekta ya usafiri wa anga ilipata kwa mwaka jana,ambapo pia sekta hiyo inatarajiwa kupoteza tena kiasi cha dola bilioni 2.8 kwa mwaka huu,na kutaka Serikali kubeba mzigo wa hasara hizo,kutokana na kufanya maamuzi yasiyo ya busara.

Kwa upande mwingine,mshauri wa masula ya miripuko ya volkano kutoka Umoja wa mataifa Gaudru,ameunga mkono uamuzi wa kufungwa kwa njia za anga,kutokana na kutokuwa kutojuwa hali halisi juu ya mazingira ya ndege kuweza kusafiri katika salama katikati ya jivu la volkano.

Uamuzi wa Serikali za barani Ulaya kutangaza kusimamishwa kwa safari za anga kutokana na mtawanyiko wa jivu la volkano,tarehe 14 Aprili,uliathiri mamilioni ya wasafiri wanaotumia njia ya anga duniani,lakini imeelzewa kuwa safari hizo zinaweza kurejea katika hali ya kawaida mapema leo hii.

Mwandishi; Ramadhan Tuwa/ APE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman