1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sahra Wagenknecht ahojiwa na DW

Josephat Charo
6 Julai 2017

Sahra Wagenknecht, mgombea ukansela wa chama cha siasa kali za mrengo wa kushoto Die Linke amefanya mahojiano yake ya kwanza wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu mwezi Septemba 2017.

https://p.dw.com/p/2g2UP
Sahra Wagenknecht im DW Interview Jaafar Abdul-Karim Ines Pohl
Picha: DW/R.Oberhammer

Mgombea huyo ambaye baba yake ni raia wa Iran alihojiwa na Mhariri Mkuu wa DW Ines Pohl na Jaafar Abdul Karim. Alipoulizwa kuhusu suala la wahamiaji kujumuishwa katika jamii ya Ujerumani. Wagenknecht alisema kuwa kwa ujumla kunafaulu vyema kwa wahamiaji waliozaliwa hapa Ujerumani.

Hata hivyo Wagenknecht alisema, "Lazima uwe muangalifu usiunge mkono mashirika fulani nchini Ujerumani, ukiacha kando fedha za walipakodi, ambayo yanapigia chapuo utengano, yanayohubiri chuki misikitini. Kwa mfano, DITIB, ni mojawapo ya mashirika yanayoendeshwa moja kwa moja na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, na serikali ya Uturuki."

Maoni kuhusu mzozo wa Syria

Katika mahojiano na DW Sahra Wagenknecht alizungumzia mzozo wa Syria akisema njia zote zinazotumiwa kuhamishia fedha kwa wapiganaji wa kundi linalojiita dola la kiislamu zinatakiwa kufungiwa ili wasiwe na uwezo wa kugharamia shughuli zao. Alisema utafiti walioufanya umebainisha benki zinafanya kazi katika eneo linalodhibitiwa na IS ambazo zimeunganishwa na benki za Ulaya na mpaka sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kuzuia fedha kuwafikia wapiganaji hao. Wagenknecht alihimiza ipo haja kuhakikisha hakuna silaha zinazofika katika eneo linalodhibitiwa na dola la kiislamu.

Mgombea huyo wa ukansela wa chama cha Die Linke pia alisema Uturuki si mshirika rahisi katika muungano unaopambana na kundi linalojiita dola la kiislamu IS. Hata hivyo Sahra Wagenknecht anakosoa jukumu la vikosi vya jeshi la Ujerumani, Bundeswehr, katika muungano huo.

Sahra Wagenknecht im DW Interview Jaafar Abdul-Karim Ines Pohl
Picha: DW/R.Oberhammer

"Saudi Arabia imechukua jukumu dogo sana katika mzozo huu. Sio tu sehemu ya pande zinazopigana Syria, na kupokea picha za satelaiti kutoka kwa jeshi la Ujerumani Bundeswehr, lakini wanajulikana pia kwamba wamewapa vifaa na fedha makundi ya kigaidi ya kiislamu nchini Syria. Na nadhani si uaminifu kusema: tunapambana na ugaidi, lakini wakati huo huo tunashirikiana na hata kupeleka silaha kwa wanaounga mkono wazi wazi ugaidi."

Sahra Wagenknecht hafutilii mbali uwezekano wa chama cha Die Linke kujiunga na serikali ya mseto baada ya uchaguzi wa Ujerumani mwezi Septemba, lakini kwa masharti fulani.

"Nataka kuongoza, lakini sitatangaza sera za uliberali mambo leo. Sitaki kuwa sehemu ya usiodhibitiwa na wa maonevu - na hata hivyo hiyo haitahitaji msaada wetu."

Sera ya mambo ya nje

Kuhusiana na sera za kigeni, Sahra Wagenknecht alikuwa na msimamo mkali katika mahojiano na DW. Alipinga kabisa hatua yoyote ya kuwatuma wanajeshi wa jeshi la Ujerumani, Bundeswehr, kwenda kuhudumu katika nchi za nje. Na hii ndiyo sababu kubwa chama cha Social Democratic SPD kinasema chama cha Die Linke hakiwezi kutawala.

Chama cha Die Linke kinachopigania utajiri ugawanywe, jumuiya ya kujihami ya NATO ivunjwe na nafasi yake ichukuliwe na chombo kingine kitakachoijumuisha Urusi na kupinga jeshi la Ujerumani kutuma wanajeshi wake katika nchi za kigeni kwa shughuli zozote zile, kinapania kushinda angalau asilimia 10 ya kura.

Huku kansela wa Ujerumani Angela Merkel akiwa bado ni maarufu sana na uchumi wa nchi ukiwa imara, wapigaji kura huenda wakasitasita kukiunga mkono chama cha Die Linke na ujumbe wake wa kupigania haki za jamii, tatizo linalokikabili pia chama cha Social Democratic, SPD, ambacho umaarufu wake umeporomoka sana katika kura za maoni za hivi karibuni.

Chama cha Die Linke na mgombea wake wa wadhifa wa ukansela Sahra Wagenknecht kinakitegemea chama cha SPD, ili kiweze kuingia madarakani, licha ya uhusiano unaoyumba kati ya vyama hivyo.

Mwandishi: Udo Bauer/Simon Young

Tafsiri:Josephat Charo

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman