1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sakata la wahamiaji wa Kiafrika nchini Israel

Zainab Aziz
7 Februari 2018

Nchini Israel wahamiaji wa Kiafrika wanasema ni bora kufungwa jela kuliko kufukuzwa kutoka nchini humo wahamiaji hao wanaona hiyo ni afadhali kuliko kupelekwa kwenye nchi wasiyoijua.

https://p.dw.com/p/2sEa9
Flüchtlingslager Holot für afrikanische Asylsuchende in Israel
Picha: Getty Images

Mmoja wa wahamiaji hao ni kijana Abda Ishmael mwenye umri wa miaka 28 kutokea nchini Eritrea aliyeko katika kizuizi hicho cha wazi ambako takriban wahamiaji 1,200 wanazuiliwa huku kituo hicho kikitarajiwa kufungwa ifikapo tarehe mosi mwezi April mwaka huu, huo ukiwa ni mpango wa serikali ya Israel katika sera yake ya kuwafukuza wahamaiaji kutoka nchini humo. Ishmael aliwaambia waandishi wa habari wa AFP kwamba hataki kufikwa na dhiki kama zilizowafika wahamiaji wenzake waliopelekwa nchini Uganda au Rwanda.

Israel inapanga kuwafukuza kutoka nchini mwake maelfu ya wahamiaji kutoka Eritrea na Sudan ambao inasema wameingia nchini humo kinyume cha sheria katika kipindi cha miaka kadhaa. Imewapa wahamiaji hao muda hadi tarehe mosi April kuwa wameondoka nchini humo vinginevyo watakabiliwa na adhabu ya kifungo jela.

Wahamiaji wa Kiafrika kwenye kizuizi cha Holot nchini Israel
Wahamiaji wa Kiafrika kwenye kizuizi cha Holot nchini IsraelPicha: picture-alliance/dpa

Wakati huo huo wale watakao amua kuondoka kwa hiari hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu serikali ya Israel imesema itawapa marupurupu ya kiasi cha dola 3,500.  Hata hivyo mpango huo wa Israel umeshutumiwa na Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa pamoja na baadhi ya raia wa Israel wakiwemo wahanga wa mauaji ya Wayahudi (Holocaust) ambao wanasema nchi yao Israel ina wajibu maalum wa kuwalinda wahamiaji.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka wizara ya mambo ya ndani hadi sasa kuna wahamiaji 42,000 wa Kiafrika nchini Israel, nusu yao ni watoto na wanawake au wanaume walio na familia. Taarifa ya wizara hiyo inasema watu hao hawamo kwenye orodha ya watakaoondolewa ifikapo mwezi Aprili.

Kambi ya kuwazuia wakimbizi wa Kiafrika ya Holot
Kambi ya kuwazuia wakimbizi wa Kiafrika ya HolotPicha: picture-alliance/dpa

Maafisa wa Israeli wamesisitiza kuwa hakuna mtu atakaye fukuzwa kutoka nchini humo iwapo amethibitishwa rasmi kuwa ni mkimbizi au anayeomba hifadhi. Wizara ya mambo ya ndani imesema kati ya jumla ya maombi 15,400 yaliyopokelewa, 6,600 yameshashughulikiwa huku watuma maombi 11 tu wakiwa wamepata majibu mazuri.

Wasudan 1,000 kutoka jimbo la Darfur wamepewa ruksa maalum ya kubakia nchini humo na hivyo kuepuka kufukuzwa. Makundi ya kidini na wanasiasa wakihafidhina wameonyesha kuwa hawapendezwi na kuwepo kwa wahamiaji wa Kiislamu au Wakikristo, wanasema watun hao ni tishio kwa desturi na utamaduni wa Wayahudi katika nchi yao ya Israel.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Reuters/T. Melville

Mara kwa mara waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ametoa mwito wa kufukuzwa kwa wahamiaji hao. Lakini makundi ya kutetea haki za binadamu yanataka wahamiaji hao watambuliwe kama wakimbizi na watetezi hao wanasema wanahofia kuwa wahamiaji hao watakabiliwa na hatari kubwa iwapo watafukuzwa kutoka Israel. Waziri wa mambo ya ndani wa Israel Arye Deri amesema atahakikisha kwamba wote wanapewa haki.

Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE

Mhariri: Iddi Ssessanga