1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sakata ya uchaguzi mkuu wa Sudan

6 Aprili 2010

Marekani yaitaka serekali ya Sudan iondoshe vikwazo kwa wapiga kura

https://p.dw.com/p/MofM
Rais wa Sudan, Hassan al-BashirPicha: DW/AP

Marekani imeishinikiza Sudan kuondosha vikwazo dhidi ya vyama vya kisiasa kabla ya kufanywa chaguzi kuu za kwanza katika nchi hiyo iliovurugwa kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu zaidi ya miongo miwili sasa.

"Marekani ina wasiwasi na matukeo yanayosumbua , kama vile vikwazo dhidi ya vyama  vya kisiasa nchini Sudan." Hayo alitamka msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, Phillip Crowley, alipozungumza na waandishi wa habari mjini Washingtion. Akaongeza kuwa " ni muhimu  kwa serekali ya Sudan kuondosha moja kwa moja vikwazo vilivowekwa dhidi ya vyama vya kisiasa na jamii. Vile vile, " Sudan lazima ihakikishe kuwa wapiga kura wote wataweza kushiriki katika uchaguzi huo kwa kuimarisha hali ya mambo nchini, ikiwa ni pamoja  na Darfur na kwengineko, na vituo vya kupiga kura viwepo katika maeneo yanayoweza kufikiwa kwa urahisi.

Bwana Crowley amesema:" watapima kama uchaguzi huo unawakilisha matakwa ya umma na unakidhi viwango vya kimataifa. Hivi sasa kuna hali zinazotia wasiwasi katika pande hizo zote mbili.

Siku ya jumatano, mgombea urais wa Chama cha upinzani cha SPLM cha Sudan ya Kusini, Yasser Arman, alijitoa katika kinyanganyiro cha urais, baada ya ya Rais wa Sudan, Omar al-Basir, kukataa kuahirisha uchaguzi. Yasser Arman  amesema amejitoa kwa sababu mbili: kwanza, ni kuwa baada ya ya kufanya kampeni katika jimbo la magharibi  la Darfur, alitambua kuwa uchaguzi hauwezi kufanywa huko, kwa sababu ya hali ya hatari iliokuwepo. Sababu ya pili  ni visa vya udanganyifu katika utaratibu wa uchaguzi.

Hata Chama cha Umma cha waziri  mkuu wa zamani wa Sudan, Sadiq al-Mahdi, siku ya ijumaa kiliipa serekali muda wa siku nne kutekeleza mageuzi muhimu kabla ya chama hicho kukubali kushiriki katika uchaguzi. Vile vile kimeitaka serekali ikomeshe kile kilichoitwa " hatua za usalama za ukandamizaji", kimedai uhuru wa kutumia vyombo vya habari vya taifa, sawa na kupata msaada wa fedha wa serekali pamoja na ahadi kuwa mgombea wa Darfur atapigania uchaguzi wa urais.

Lakini tume ya uchaguzi ya Sudan imesisitiza kuwa  chaguzi zitafanywa tarehe 11 hadi 13 mwezi huu wa April, kama ilivyopangwa, licha  ya vyma vya upinzani kushikilia ziahirishwe mpaka mwezi wa Mei. Baada ya mpinzani mkubwa wa Rais al-Basir, Yasser Arman, kujitoa katika uchaguzi huo, al-Basihr sasa hana mpinzani mkali, na anatazamiwa kushinda bila ya shida.

Mwandishi: Martin, Prema/AFP

Mhariri: MIraji Othman