1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sarkozy atangaza kugombea tena

Abdu Said Mtullya16 Februari 2012

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa ametangaza kuwa atagombea kipindi kingine cha Urais wakati ambapo kura za maoni zinaonyesha kuwa yupo nyuma ya mgombea wa chama cha upinzani Francois Hollande

https://p.dw.com/p/14421
Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa
Rais Nicolas Sarkozy wa UfaransaPicha: REUTERS/TF1

"Ndiyo nitakuwa mgombea katika uchaguzi wa urais utakaofanyika kuanzia mwezi wa Aprili."Rais Sarkozy aliyasema hayo jana katika mahojiano ya Televisheni, baada ya kuwaweka watu kizani kwa muda wa wiki kadhaa. Alieleza jana kwamba kung'atuka katika muktadha wa mgogoro wa uchumi kutakuwa sawa na nahodha anaeitelekeza meli wakati wa dhoruba.

Sarkozy ameamua kugombea muhula mwingine kwa sababu, amesema bado anayo ya kuwaambia Wafaransa. Amesema ikiwa hatasimama katika uchaguzi kwa mara nyingine tena, katika nyakati hizi za migogoro,hayo yangelikuwa sawa na nahodha anaeitelekeza meli yake wakati wa dhoruba. Amesema bado anayo ya kuwaambia Wafaransa na bado anayo mapendekezo ya kuyawasilisha kwao.

Hata hivyo kura za maoni zinaonyesha kwamba Rais huyo nyuma ya mshindani wake mkuu, Kiongozi wa chama cha Kisoshalisti Francois Hollande. Kwa mujibu kura hizo za maoni ,Sarkozy angelipata asilimia kati ya 24.5 na 26 endapo uchaguzi ungelifanyika leo. Mshindani wake mkuu Francois Hollande angelipata kati ya asilimia 29.5 na 31.

Kutokana na wasi wasi wa kuwa nyuma katika kura za maoni washauri wa Sarkozy walimshawishi Rais huyo aanze kuipigia chapuo kampeni yake. Wanaiongoza kampeni yake wameahidi kuwasilisha mapendekezo mapya kila siku ili kuwavutia wapiga kura.

Sarkozy atawahutubia watu wanaomuunga mkono kwenye mkutano mkubwa wa hadhara mjini Marseille. Sarkozy amesema mabadiliko makubwa atakayoyafanya ikiwa atachaguliwa tena, yatakuwa ni kuwapa Wafaransa usemi mkubwa zaidi wa kuamua juu ya mustakabal wao, kwa kuaandaa kura za maoni, kwa kuanzia na kura ya maoni juu ya kuweka kikomo katika posho za watu waisokuwa na ajira.

Sarkozy amesema ikiwa Wafaransa wanataka kuudumisha utaratibu wao wa maisha wanapaswa kuleta mabadiliko wakati wote.Ameleeza kuwa mabadiliko ndiyo yatakayoifanya Ufaransa iwe nchi yenye nguvu.

Mwandishi/Mtullya Abdu/ZA/DPEA/

Mhariri/Yusuf Saumu