1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudi Arabia kukosolewa kuhusu haki za binadamu

6 Machi 2019

Wanadiplomasia wanasema nchi za Ulaya wiki hii zitatoa wito kwa Saudi Arabia kuwaachia wanaharakati walio kizuizini na pia wataitaka nchi hiyo itoe ushirikiano katika uchunguzi wa mauaji ya mwandishi Jamal Khashoggi.

https://p.dw.com/p/3EWCr
Saudi-Arabien Tabuk Mohammed bin Salman
Picha: picture-alliance/abaca/Royal Palace/B. Al Jaloud

Wanadiplomasia hao na waendeshaji kampeni wameyasema hayo katika ukosoaji wa kwanza wa Saudi Arabia kwenye Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za binadamu linalofanyika huko Geneva, Uswisi. 

Taarifa hiyo ya pamoja inayotarajiwa kusomwa Alhamis, inatolewa wakati ambapo kuna hofu inayoongezeka kuhusiana na mustakabali wa watu waliozuiliwa ambao wametambuliwa na makundi ya uangalizi kama wanaharakati wa haki za wanawake, baada ya mwendesha mashtaka wa umma kuripotiwa kwamba anajiandaa kuwafungulia mashtaka.

Wanaharakati wamefurahishwa na kukosolewa kwa Saudi Arabia

Iceland ndiyo nchi iliyoongoza harakati hizo za ukosoaji na imepata uungwaji mkono kutoka kwa nchi za Ulaya na wawakilishi kutoka maeneo mengine. Saudi Arabia ni mojawapo ya nchi inayohudhuria Baraza hilo la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa.

Schweiz - Afghanistan Konferenz in Genf
Baraza hilo la haki za binadamu linafanyika Geneva, UswisiPicha: Getty Images/AFP/D. Balibiouse

Wanaharakati wameipokea vyema hatua hiyo. Omaima Al-Najjar ni mwanablogu na mwanaharakati wa haki za binadamu kutoka Saudi Arabia.

"Ni muhimu kukumbuka kwamba tulichokiona sasa, kufungwa kwa wanawake kuanzia mwezi Mei hadi Agosti, mateso wanayopitia kama kutengwa kwa hadi miezi mitatu wanapokuwa jela ndo mwanzo tu wa mkoko kualika maua katika ukiukaji wa haki za binadamu na ukiukaji wa makubaliano ya kimataifa yanayofanywa na serikali ya Saudi Arabia," alisema Al-Najjar.

Iceland ilichaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka jana na kuichukua nafasi ya Marekani katika Baraza hilo la Umoja wa Mataifa, baada ya Marekani kujiondoa kutokana na kile ilichosema kuwa ni kuonewa kwa Israel.

Waziri asema Saudia itatoa ushirikiano kwa Umoja wa Mataifa

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu lililo na makao yake mjini New York Human Rights Watch, limeikumbatia hatua hiyo liliyoitaja kama ya kwanza inayoangazia haki za binadamu Saudi Arabia na kusema kuwa wanachama wa baraza hilo wanastahili kuishinikiza Saudi Arabia ishirikiane na uchunguzi kuhusiana na mauaji ya Khashoggi, iwache kuwalenga wanaharakati, waandishi wa habari na wakosoaji na iwaachie watu waliozuiliwa jela kimakosa.

Agnes Callamard Sonderberichterstatterin  UN für außergerichtliche, summarische oder willkürliche Hinrichtungen
Agnes Callamard anaongoza uchunguzi wa Umoja wa Mataifa kuhusu kifo cha KhashoggiPicha: Getty Images/AFP/M. Recinos

Wiki iliyopita waziri mmoja wa Saudi Arabia aliliambia baraza hilo kuwa nchi hiyo ya kifalme itatoa ushirikiano lakini hakusema iwapo ni katika uchunguzi wa mauaji ya Khashoggi, ambao unaongozwa na mchunguzi wa Umoja wa Mataifa Agnes Callamard.

Adel bin Ahmed Al-Jubeir ambaye ni waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia aliliambia baraza hilo la Geneva pia kwamba wana mikakati ya kuhakikisha kesi za waliozuiliwa zinaendeshwa njia ya haki, wanaboresha mazingira ya wafungwa pamoja na kuwahamasisha wanawake.