1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudia: Ni wazi Iran ndiyo iliyoshambulia vituo vya mafuta

19 Septemba 2019

Saudi Arabia imeonyesha mabaki ya kile ilichoelezea kuwa ni ndege zisizo na rubani za Iran na makombora yaliyotumika katika vituo vyake vya uzalishaji mafuta.

https://p.dw.com/p/3PrAp
Saudi-Arabien | Nach Angriff auf Ölanlagen in Saudi-Arabien
Picha: Reuters/H. I. Mohammed

Msemaji wa Wizara ya ulinzi ya Saudi Arabia Kanali Turki al-Malki amewaambia waandishi wa habari kuwa jumla ya ndege zisizo na rubani pamoja na makombora ya angani 25 yalitumika katika mashambulizi ya mwishoni mwa wiki iliyopita. Malki ameongeza kuwa makombora matatu hayakufika katika eneo lililokuwa limelengwa.

"Ninatoa wito kwa jamii ya kimataifa kutambua kwamba mashambulizi yalifanywa kutoka Iran. Licha ya juhudi zake za kutaka kuficha ukweli, Iran inastahili kukubali kwamba mashambulizi haya hayakutokea Yemen."

Maliki amesema kwamba uchunguzi bado unaendelea kubaini hasa makombora hayo yalirushwa kutoka sehemu gani ambapo mara kadhaa alikataa kujibu maswali ya waandishi wa habari kuhusiana na kuhusika kwa Iran katika mashambulizi hayo.

Baada ya Saudi Arabia kutoa ushahidi huo, Rais Donald Trump amesema kuwa ameiagiza Wizara ya fedha ya Marekani kuongeza vikwazo zaidi kwa Iran. Haikuwa wazi hasa ni hatua gani ambazo Trump amemuagiza Waziri Steven Mnuchin kuchukua dhidi ya Jamhuri hiyo ya Kiislamu.

Brüssel US-Außenminister Mike Pompeo
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike PompeoPicha: Getty Images/AFP/K. Tribouillard

Wakati huo huo Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo ameunga mkono kauli hiyo ya Saudi Arabia akisema kuwa madai ya waasi wa Houthi kwamba wao ndio waliohusika ni uongo mtupu. Pompeo ameongeza kuwa shirika la ujasusi la Marekani lina imani kubwa kwamba waasi hao wa Houthi hawana silaha zilizotumika katika mashambulizi hayo.

Huku hayo yakiarifiwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema wataalam wa Umoja huo wameelekea Saudi Arabia kufanya uchunguzi kuhusiana na mashambulizi hayo ya mwishoni mwa wiki iliyopita. Guterres ameonya huenda kukashuhudiwa athari kubwa iwapo mzozo huo utazidi.

"Nililaani sana shambulizi hilo. Nafikiri shambulizi hilo litaleta kuongezeka kwa machafuko katika eneo la Ghuba na tunastahili kusitisha hali hii ambayo ina athari ya moja kwa moja katika masoko ya mafuta. Iwapo kutakuwa na mzozo mkubwa katika Ghuba athari zitakuwa katika eneo hilo na dunia nzima."

Nchini Ujerumani chama chake Kansela Angela Merkel kilikuwa kinaanza kupata shinikizo kutoka kwa baadhi ya wanachama wake kuhusiana na kuondoa marufuku ya kuiuzia silaha Saudi Arabia baada ya mashambulizi hayo, ila kupitia msemaji wa serikali, Ujerumani imethibitisha marufuku hayo yataendelea hadi Machi mwaka 2020.