1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Schalke yazinduka katika Bundesliga

Sekione Kitojo
3 Oktoba 2016

Schalke 04  yazinduka, yaikaba  koo  Borussia  Monchengladbach, Bayern  yavutwa  shati, wakati  Borussia  Dortmund  yaangukia  pua katika  Bundesliga  mchezo  wa  wiki  ya  sita

https://p.dw.com/p/2Qpz8
Bundesliga | 6.Spieltag | FC Schalke 04 vs Borussia Moenchengladbach
Wachezaji wa Schalke wakifurahia bao baada ya kuiadhibu Gladbach kwa mabao 4-0Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Thissen

 Manchester City  yaonja  kipigo  chini  ya  Pep Guardiola , na majirani  zao  Manchester  United  yaambulia  sare  mbele  ya Tottenham Hotspurs.

Katika Bundesliga,  Schalke 04  ilifikisha  mwisho  masaibu yake  ya  kupokea  vipigo  mfululizo  msimu  huu  ambapo  timu  hiyo ilikubali  vipigo  mara  tano  katika  msimu  huu  wa  ligi  na  kujinasua kutoka  mkiani  mwa  ligi  jana  Jumapili  kwa  ushindi  mnono  wa mabao 4-0  dhidi  ya  Borussia  Moenchengladbach wakati mchezaji aliyesainiwa  hivi  karibuni  Breel Embolo  akifumania  nyavu  mara mbili.

Bundesliga | 6.Spieltag | FC Schalke 04 vs Borussia Moenchengladbach
Breel Embolo wa Schalke 04Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Meissner

Embolo mwenye  umri  wa  miaka  19 , na  kuigharimu  Schalke kitita cha  euro  milioni  22  kutoka  Basel  ya  Uswisi  mwezi  Juni , alifunga mabao  yake  ya  kwanza  kwa  Schalke  katika  kipindi  cha pili  baada  ya  kuwa  sare  bila  kufungana  katika  kipindi  cha kwanza.

"Nimefurahi  kufunga  mabao, lakini  kitu  muhimu ni  kwamba tumeshinda na  tumenufaika  na  mchezo  mzuri  tuliouonesha", amesema  Embolo.

Mshambuliaji  wa  Borussia  Moenchengladbach  Andre  Hahn hakufurahishwa  na  timu  yake  ilivyocheza.

"Kwa ufupi  hatukufanya  vizuri. Katika  kipindi  cha  kwanza hatukuweza  kucheza  vizuri  na  katika  kipindi  cha  pili tulijaribu kubadilika, lakini  ndipo  Schalke ikapata  penalti. Na  kuanzia  hapo wapinzani  wetu waliongeza  ari  na  tulizidi  kuharibikiwa, ulinzi mbovu na  kisha  tukaendelea  kufungwa  mabao.

Bundesliga | 6. Spieltag | FC Schalke 04 vs Borussia Moenchengladbach
Wachezaji wa Schalke wakipambana na GladbachPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Meissner

Matokeo  hayo  yameinyanyua  Schalke  hadi  nafasi  ya  16  katika timu  18  za  ligi  ya  Bundesliga, na  kuicha  Hamburg  ikiwa  mkiani mwa  ligi  hiyo  baada  ya   kupokea  kipigo  cha  mabao 2-0  dhidi ya  Hertha  Berlin  ikiwa  ni  kipigo cha  tano  mfululizo. Gladbach ambayo  ilipoteza  mchezo  wake dhidi  ya  Barcelona  siku  ya Jumatano  katika  Champions League , imeporomoka  hadi  nafasi ya  9 katika  msimamo  wa  ligi.

Katika  mchezo  wa  kwanza  jana  Jumapili  ukame  wa  magoli kwa mshambuliaji  mpya  wa  Wolfsburg  Mario Gomez  uliendelea  baada ya  kutoka  sare  bila kufungana  na  Mainz 05.

Huyu  hapa  Mario Gomez.

"Sio tu  mashabiki  wamevunjika  moyo, lakini  hata   sisi. Leo tulifanya  juhudi  kupita  kiasi. Nitasema  nini ? Ni balaa, kwa  kweli ni  balaa, mpira ulikuwa  hautaki  kabisa kuvuka  msitari. Hatujajizawadia kwa  mchezo  wetu , kwa  kweli  tulikuwa  na  nafasi nyingi , na  tungeweza  kushinda  mchezo  huo  kwa  mabao mengi.

Lakini  Gomez hadi  sasa  ameshindwa  kuutumbukiza  mpira  wavuni kwa  dakika  450 katika  Bundesliga na kuwa  na  jioni  ya kufadhaisha  katika  uwanja  wa  Volkswagen Arena  jana. Wolfsburg imepata  ushindi  mara  moja  tu  katika  michezo  sita  ya  ligi  msimu huu. Sare  hiyo  imeiweka  Wolfsburg , ambayo  ilifikia  robo fainali ya  Champions League  msimu  uliopita , ikiwa  nafasi  ya  13 ya msimamo  wa  ligi  ya  Ujerumani  na  Mainz ikiwa  katika  nafasi  ya 11.

Fußball Bundesliga Werder Bremen - VfL Wolfsburg
Mario Gomez wa Wolfsburg (kushoto)Picha: Picture-Alliance/dpa/C. Jaspersen

Lakini  timu inayoshangaza  msimu  huu  ni  FC Kolon  ambayo haijaonja  kipigo  hadi  sasa  katika  Bundesliga , na  mwishoni  mwa juma  ilitoroka  na  pointi  moja  mbele  ya  mabingwa  watetezi Bayern Munich  katika  uwanja  wa  Alianz Arena  mjini  Munich baada  ya  timu  hizo  kutoka  sare  ya  bao 1-1.

Huyu  hapa  kocha  wa  FC Kolon Peter Stoeger.

"Iwapo utaweza  kupata  pointi  mjini  Munich , basi unafarijika  sana. Tunatambua, kwamba  mchezo  huo  haukuwa  rahisi. Ni  wazi , kwamba  katika  dakika  45  za  kwanza  hawakuweza  kufanya mengi, kuliko  tulivyofanya. Kipindi  cha  pili kilikuwa  kizuri , kwa hiyo  kwetu hali  ilikuwa  nzuri. Tunafurahi jinsi  tulivyofanyakazi kwa pamoja , ni  mara  ya  kwanza  kwetu  kupata  pointi  dhidi  ya bayern. Na inafurahisha.

Mshambuliaji  wa  Bayern Munich Thomas Mueller  alikuwa  na  haya ya  kusema  baada  ya  mchezo  huo.

"Hatukucheza  vizuri kuanzia  kipindi  cha  pili  kilipoanza  hadi  dakika ya  70. Kuanzia  hapo mara  kadhaa  tuliyumba, na  dakika  za mwisho tulipata  bahati, kwa  kuwa  tulijiingiza  katika  hatari. Tulitaka kulinda  ushindi  wetu kwa  kila  hali. Katika  kipindi  cha  pili tulikosa bahati  katika  kumalizia  mipira golini. Kwa  jumla  ni  kawaida kwamba haikuwa  mbaya  sana , wakati unaongoza  kwa  bao 1-0 nyumbani  na  hatimaye  unaambulia  tu  pointi  moja."

Borussia  Dortmund  haikuweza  kuhimili  vishindo  vya  Bayer Leverkusen  baada  ya  kutoka  sare  ya   Real Madrid   katikati  ya wiki , na  kukubali  kipigo  cha  mabao 2-0  katika  uwanja  wa  Bayer Arena  mjini  Leverkusen. Mbali  ya  kubadilisha  benchi  la  ufundi na kuamua  kumpa  jukumu  hilo  kocha  Markus Gisdol  baada ya kumfuta  kazi Bruno  Labbadia  hamburg SV  ilijikuta  ikigaagaa mchangani  tena  baada  ya  kupokea  kipigo  cha  mabao 2-0  dhidi ya  Hertha  Berlin. Huyu  hapa  kocha  Markus  Gisdol.

Bundesliga | Bayer Leverkusen - Borussia Dortmund | Tuchel - Castro - Rode
Kocha Thomas Tuchel wa Dortmund akijaribu kuwaelekeza wachezaji wakePicha: picture-alliance/dpa/B. Thissen

"Unaweza  kuona  kwamba  ni  siku  chache  tu  tumekuwa  pamoja. Na  kumekuwa  na  matukio  mazuri  yaliyoonekana  uwanjani. Ni kweli  kwamba  kuna  mambo  mengi, ambayo  tunapaswa kuyafanya  vizuri  zaidi. Lakini  ishara  ya  kwanza , ambayo  timu imeionesha ,  naona sio  mbaya. Kwa  bahati  kidogo  tu huenda  leo tungeweza  pengine  kupata  kitu.

Premier League yawaka  moto

Nchini  Uingereza  , katika  premier  league  wiki  hii  pia  kumetokea mengi ,  ambapo  timu  mbili ambazo  hazijapoteza  mchezo Tottenham  Hotspurs   na  Manchester  City  zilikutana   na kulitarajiwa  kutokea  kitu  jana  Jumapili. Kikosi  cha  kocha Mauricio Pochettino  kilikizawadia  kikosi  cha  Pep Guardiola  kipigo cha  kwanza  msimu  huu  kwa  ushindi  wa  bao 2-0.

Ushindi  huo umeondoa  mtazamo kutoka  kampeni  ya  City  katika msimu  huu  kuanza  kwa  kasi  ya  ajabu  hadi  katika  kile  ambacho kimekuwa  mwanzo  mzuri  kabisa  wa  Spurs  tangu  msimu  wa mwaka  1960-61 wakati  timu  hiyo  iliposhinda ligi  na  kombe  la FA.

Deutschland DFB Pokal Finale FC Bayern München - Borussia Dortmund
Pep Guardiola kocha wa timu ya Man City ameonja kipigo katika Premier LeaguePicha: Reuters/K. Pfaffenbach

Kwingineko  pia  kulikuwa  na  sare  ambapo Stoke City  ilitoka  sare ya  bao 1-1  na  Manchester United  na  Southampton  ikalazimisha sare ya  bila  kufungana  na  mabingwa  watetezi Leicester  City.

Na  katika  uwanja  wa  Turf Moor  kocha  wa  Arsenal  Arsene Wenger  alikuwa  akisherehekea  miaka  20  akiwa  kocha  wa  The Gunners na  kushuhudia  timu  yake ikinyakua  ushindi  katika  dakika ya  mwisho  wakati  wenyeji  wakidhania  kwamba  wamepata  sare. Arsenal  iliibuka  na  ushindi  wa  bao 1-0 dhidi  ya  Burnley.

Wakati  huo  huo  Swansea  City imemfuta  kazi  kocha  wake Francesco Guidolin  na  kumwajiri  haraka  kocha  wa  zamani  wa timu  ya  taifa  ya  Marekani Bob  Bradley  kuchukua  nafasi  yake.

Ligi ya Uhispania nguvu ya tatu yatawala

Atletico  Madrid inaongoza  ligi  ya  Uhispania , La  Liga  baada  ya kuishinda  Valencia  jana  Jumapili  kwa  mabao 2-0,  ambapo  siku hiyo  ilishuhudia  mabingwa  Barcelona  ikipokea  kipigo cha  mabao 4-3 dhidi  ya  Celta  Vigo  na  Real Madrid  ikitolewa  jasho  na  Eibar kwa  kutoka  sare ya  bao 1-1.

Spanien La Liga Barcelona vs Alaves Messi
Wachezaji wa Barcelona baada ya kipigo dhidi ya Celta VigoPicha: Reuters/A. Gea

Bao  safi  la  Mario Balotelli  dakika  nne  kabla  mpira  kumalizika uliipa  Nice  ushindi  wa  mabao 2-1  dhidi  ya  Lorient jana  na kuiweka  timu  hiyo  ya  Ligue 1 juu  ya  msimamo  wa  ligi  kwa kipindi  hiki  ligi  za  Ulaya  zinaposita  kwa  ajili  ya  michezo  ya  timu za  taifa.

Katika  Serie  A   ligi  ya  Italia Udinese  imemfuta  kazio  kocha wake Giuseppe Iachini  baada  ya  kipigo  cha  mabao  3-0  dhidi  ya Lazio kipigo  cha  nne  mfululizo  katika  michezo  saba  ya  ligi.

Ubingwa wa Nigeria

Barani  Afrika  Rangers  ya  Nigeria  jana  walitawazwa  mabingwa wa  ligi  ya  soka  ya  nchi  hiyo  baada  ya  kusubiri  kwa  miaka  32 wakati  walipoitwanga  El Kanemi Warriors  kwa  mabao 4-0 na kumaliza  wakiwa  juu  ya  msimamo  wa  ligi  katika  siku  ya  mwisho ya  ligi  ya  nchi  hiyo. Rangers  wamemaliza  wakiwa  na  pointi 63 kutokana  na  michezo 36, pointi  tatu  juu  ya  washindi  wa  pili Rivers United. Timu  hizo  sasa  zitaiwakilisha  nchi  hiyo  katika champions League  barani  Afrika.

Mchezaji  wa  zamani  wa  Liverpool Rigobert Song, nahodha  wa  zamani wa  timu  ya  taifa  ya  Cameroon , mwenye  umri  wa  miaka  40, amekuwa  katika  hali  ya kutojitambui leo Jumatatu  akiugua kiharusi. Radio ya  taifa  ya  Cameroon  imerikopti kuwa  Song, ambae pia  aliichezea West Ham United, Metz na  Lens za  Ufaransa, FC Kolon  ya  Ujerumani na  Galatasaray  ya  Uturuki, alikimbizwa  hospitali ya  karibu na  Yaounde jana Jumapili  baada  ya   kupata uvimbe katika  ubongo.

Niederlande Kamerun WM Fußball Weltmeisterschaft Flash-Galerie
Rigobetrt Song mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Cameroon ambaye amepata kiharusiPicha: AP

Marais wa  shirikisho  la  kandanda  barani  Afrika CAF watawekewa  ukomo wa  vipindi vitatu  vya  miaka  minne kuanzia  uchaguzi  utakaofanyika  mwaka  2017, taasisi  hiyo inayosimamia  michezo  barani  Afrika  imesema leo. Hakujakuwa  na  ukomo  hapo  kabla  ambapo  rais  wa  sasa  Issa  Hayatou aliliongoza  shirikisho  hilo  la  Afrika  tangu  mwaka  1988.

Na  katika  mchezo  wa  golf

Marekani  iliwashinda  wachezaji  wa  bara  la  Ulaya  kwa 17-11 katika  ubingwa  wa  Ryder Cup  katika  mchezo  wa  golf  ukiwa  ni ushindi  wa  kwanza  tangu  mwaka  2008, kombe  ambalo hushindaniwa  baina  ya   wachezaji  wa  golf  wa  Ulaya  na Marekani  kila  mwaka .

Kanada Montreal Formel 1 Grand Prix Qualifikation
Sebastian Vettel(kushoto) akiwa na Nico Rosberg (Kulia)Picha: Getty Images/M. Thompson

Nae Sebastian Vettel  wa  mbio  za  magari  za  Formula 1  ameomba radhi  kwa  kugongana  na  Nico Rosberg  mwanzoni  mwa  mbio  za magari  za  Malaysia  Grand Prix, alipompigia  simu Rosberg  jana Jumapili. Dereva  huyo  wa  gari  aina  ya  Ferrari  alimgonga Rosberg  katika  kona  akijaribu  kumpita, lakini aliishia  kuharibu  gari yake na  kumlazimisha  Rosberg  kupunguza  kasi  na  kurudi  nyuma, hata  hivyo  Rosberg  alimaliza  akiwa  namba  tatu.

 

Mwandishi: Sekione  Kitojo / ape / afpe / rtre / dpae

Mhariri : Yusuf , Saumu