1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Martin Schulz atowa tahadhari ya la wakimbizi

Saumu Mwasimba
23 Julai 2017

Mgombea ukansela wa chama cha SPD asema Ujerumani yahitaji kuchukua mikakati ya kuzuia wimbi la wakimbizi waliomiminika Itali

https://p.dw.com/p/2h1i3
Berlin SPD-Kanzlerkandidat Schulz präsentiert Zukunftsplan
Picha: picture-alliance/dpa/M. Gambarini

Mgombea atakayepambana na Angela Merkel  katika kinyang'anyiro cha Ukansela nchini Ujerumani Martin Schulz kutoka chama cha Social Democratic SPD ameliambia shirika la habari la Reuters leo Jumapili(23.07.2017)kwamba Ujerumani inahitaji kuchukua hatua sasa za kuzuia kujirudia kile kilichoshuhudiwa mwaka 2015 ambapo wakimbizi 890,000 walimiminika nchini Ujerumani.

Septemba mwaka 2015 kansela Angela Merkel alitangaza sera ya kuiacha mipaka  wazi kwa ajili ya kuwaruhusu maelfu ya wakimbizi kuingia nchini ili kuepuka janga la kibinadamu hatua ambayo baadaye ilikuja kuutia dosari umaarufu wake na kumuharibia vibaya na badala yake ikaimarisha umaarufu wa chama kinachopinga wahamiaji cha siasa kali kinachoitwa chama mbadala kwa wajerumani AFD. Hata hivyo chama cha kihafidhina cha Kansela Merkel tangu wakati huo kimejitahidi na kurudisha hadhi na umaarufu wake huku uungaji mkono wa chama cha AFD ukipungua.

Italien - Flüchtlingsboote - Mittelmeer
Picha: Getty Images/C. McGrath

Martin Schulz ambaye chama chake cha Social Demokratic SPD kiko nyuma ya chama cha kansela Merkel kwa asilimia kubwa katika kura za maoni kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Septemba tarehe 24 ameonya dhidi ya kujirudia kwa matukio kama yaliyoshuhudiwa huko nyuma baada ya zaidi ya wahamiaji 93,000 wengi kutoka nchi za Afrika zilizoko kusini mwa jangwa la Sahara na Bagladesh kuwasili kwa maboti kusini mwa Italia hadi kufikia sasa katika kipindi cha mwaka huu wa 2017. Zaidi ya asilimia 17 ya kiwango kilichoshuhudiwa katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Martin Schulz akizungumza kupitia mahojiano aliyofanyiwa akiwa mji wa Aachen huko Magharibi mwa Ujerumani amesema idadi ya wakimbizi wanaowasili kwa hivi sasa nchini Itali inatia wasiwasi mkubwa. Inaarifiwa kwamba maelfu wanawasili kwa siku. Kutokana na hali hiyo mgombea huyo wa Ukansela amesema ikiwa Ujerumani haitaki kushuhudia matukio yaliyopita kujirudia basi panahitajika kuchukuliwa hatua hivi sasa wakati ambapo Itali inaelekea kufikia kikomo katika uwezo wake wa kukabiliana na wimbi la wakimbizi.

Nchi nyingine za Umoja wa Ulaya zinahitajika kuisaidia Itali kwa kuchukua hatua za kuwapokea wakimbizi ameongeza kusema Schulz.

Deutschland EU-Pressekonferenz auf dem G20-Gipfel in Hamburg
Picha: picture-alliance/Geisler-Fotopress

Tayari Schulz ameshazungumza na mkuu wa tume ya Umoja wa Ulaya Jean Claude Junker leo Jumapili kuhusu ni aina gani ya msaada wa fedha au miundombinu unaoweza kutolewa na Umoja huo katika kuzisaidia nchi kujiandaa kuwachukua wakimbizi na kubaini kwamba atazungumza na serikali ya Itali na tume hiyo ya Umoja wa Ulaya kuhusiana na suala hilo wiki inayokuja.

Katika mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la Ujerumani la  Bild am Sonntag Schulz amesema hali ni mbaya sana na kusema kwamba anataka kulizungumzia suala hilo katika kampeini za uchaguzi akisema wale wanaochezea muda na kujaribu kulipuuza suala hilo hadi uchaguzi wanakosea. Kiongozi huyo wa chama cha SPD anatarajiwa kwenda Itali Alhamisi wiki ijayo kukutana na waziri mkuu Paolo Gentiloni.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:John Juma