1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Schweinsteiger amefurahi kujiunga tena na Van Gaal

13 Julai 2015

Habari sasa zimeanza kuingia kichwani kwa mashabiki wa Bayern Munich. Maana ni bayana kabisa kuwa Bastian Schweinsteiger siyo tena mchezaji wao. Na kiungo huyo ameyatangaza wazi malengo yake

https://p.dw.com/p/1Fxwk
Fußball Bastian Schweinsteiger Manchester United
Picha: Reuters/J. Redmond

Bastian Schweinsteiger mchezaji aliyefanikisha ubingwa wa dunia kwa timu ya taifa ya Ujerumani , Die Mannschaft, ameipa mkono wa kwaheri Bayern Munich timu aliyoichezea tangu akiwa kijana mdogo miaka 17 iliyopita. Sasa Basti na Bayern ni historia, ukurasa mpya anaufungua utakapoanza msimu wa kandanda mwaka huu akiwa na Manchester United. Basti aliwahi kuwa na kocha Luis van Gaal , wakati alipokuwa akiipa mafunzo Bayern Munich kwa muda wa misimu miwili, kabla ya van Gaal kutimuliwa. Basti anahamia Manchester ambayo imeipatia Bayern Munich kitita cha euro milioni 20 kupata huduma ya mchezaji huyo mahiri wa kati.

Raheem Sterling
Raheem Sterling amejiunga na Manchester City kutoka LiverpoolPicha: picture-alliance/dpa/P. Powell

Katika Premier League Bastian atakabiliana na wachezaji wengine wa Ujerumani kama Mesut Ozil na Per Mertersacker wa Arsenal. Hata hivyo rafiki yake mkubwa Lukas Podolski ameihama Arsenal na ameelekea Galatasaray ya Uturuki.

Manchester United imekaza kamba katika soko la uamisho msimu huu, ambapo mbali ya kumkamata Bastian Schweinsteiger, imetupa mshipi pia kwa mchezaji wa kati wa Ufaransa na klabu ya Southampton Morgan Schneiderlin na tayari amefanyiwa uchunguzi wa afya klabuni Old Trafford. Mbali ya wachezaji hao pia yumo mlinzi wa kulia wa klabu ya Torino na Italia Matteo Darmian.

Liverpool imekubali pauni milioni 49, sawa na dola milioni 76 kutoka Manchester City ili kumwachia winga machachari Raheem Sterling, vimeripoti vyombo vya habari.

Hata hivyo uhamisho wa Sterling mwenye umri wa miaka 20 unategemea masharti yake binafsi pamoja na uchunguzi wa afya yake.

Sterling aliachwa na Liverpool wakati kikosi cha timu hiyo kilipoondoka kwenda Thailand kwa ajili ya ziara ya kabla ya kuanza kwa msimu jana Jumapili, na kuchochea uvumi zaidi kwamba mshambuliaji huyo yu tayari kujiunga na City. Liverpool inafanya ziara ya mashariki ya mbali , ikiwa itacheza michezo ya majaribio nchini Australia na Malaysia.

WM 2014 Gruppe B 2. Spieltag Spanien Chile
Mlinda mlango Iker Casillas amehamia Porto kutoka Real MadridPicha: Reuters

Real Madrid imeamua kumuaga rasmi nahodha wake wa zamani Iker Casillas anayeihama klabu hiyo leo kufuatia shutuma kuhusu hali ya upweke aliyokuwa nayo wakati akifanya mkutano na waandishi habari wa alipokuwa akiaga jana Jumapili. Casillas ambaye anaihama timu yake ya toka utoto baada ya miaka 16 anahamia Porto ya Ureno , alijikuta yuko peke yake bila viongozi wa klabu hiyo uwanjani Bernabeu na alibubujikwa na machozi kila mara wakati akisoma taarifa na kuishukuru klabu kwa kumpa kila kitu. Real Madrid imeshutumiwa kwa kutowapa wachezaji wake maarufu heshima wanayostahili.

Mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani Kevin Kuranyi anatafuta kurejea katika Bundesliga na amesema amepata maombi kadhaa baada ya kurejea nchini baada ya miaka mitano akiwa na Dynamo Moscow ya Urusi.

Kuranyi amesema anatarajia kufanya uamuzi katika muda wa wiki mbili zijazo. Amesema anataka kujiunga na klabu ambayo ina mfumo mzuri na kocha mzuri. Kuranyi amekuwa akijifua na kujiweka fit na klabu ya daraja la nne ya Saarbruecken lakini amekanusha kwamba anataka kujiunga nayo. Pia amehusishwa na vilabu kama Augsburg na Hannover lakini amesema huo ni uvumi tu. Kuranyi amefunga mabao 111 katika Bundesliga akiwa na VFB Stuttgart katika michezo 261 mwaka 2005-2010 kabla ya kuhamia Dynamo ambako alifumania nyavu mara 50 katika michezo 123. Pia aliichezea timu ya taifa ya Ujerumani na kufunga mabao 19 kati ya mwaka 2003 na 2008.

Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / dpa / rtre /afpe
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman