1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jimbo la Northrhine Westphalia ndio ngome ya Wasalafi

Zainab Aziz
22 Oktoba 2018

Jimbo la Northrhine Westphalia ndilo lenye idadi kubwa ya waislamu wasalafi nchini Ujerumani. Hata hivyo watu hao hawaonekani wazi katika ngome yao kuu hiyo, wanaendesha shughuli zao chini kwa chini na wanajibadilisha.

https://p.dw.com/p/36w7E
Köln Salafisten Veranstaltung
Picha: picture-alliance/dpa

Hakuna jimbo lenye wasalafi wengi kuliko la Northrhine Westfalia na hakuna jimbo lingine lenye idadi kubwa ya wasalafi wenye itikadi kali kama jimbo hilo la kaskazini magharibi mwa Ujerumani. Baadhi yao walikwenda kwenye sehemu iliyoitwa dola la kiislamu.

Mia tatu walikwenda huko kati ya 1000 wanaofahamika kuwapo nchini Ujerumani kote. Takriban mashambulio yote ya kigaidi yaliyotukia nchini Ujerumani mnamo miaka ya hivi karibuni yalifanywa na watu waliopuliziwa kasumba ya itikadi kali kwa kupitia kwa masalafi. Anis Amri ni mmojawapo. Tarahe 19 Desemba mwaka wa 2016 gaidi huyo alifanya shambulio la kigaidi kwenye soko la krismasi la mjini Berlin na kuwaangamiza watu 12.

Hayo yalikuwa mauaji makubwa kabisa kuwahi kufanywa na waislamu wenye itikadi kali nchini Ujerumani hadi wakati huo. Hata hivyo inafaa kutilia maanani kwamba sio kila mtu anayefuata itikadi ya kisalafi ni gaidi lakini pia ni kweli kwamba magaidi wengi waliofanya mashambulio waliwahi kuwa wasalafi. Watu mbalimbali wanaozifuatilia nyendo za waislamu hao wanakubaliana juu ya tathmini hiyo.

Hata hivyo yapasa kutambua kwamba ndani ya jumuiya ya wasalafi wamo waumini mbalimbali wenye tasfiri kali ya uislamu lakini idadi kubwa ni ile ya wale wenye malengo ya kisiasa wanaolenga shabaha ya kuunda kinachoitwa dola la kiislamu.

Wasalafi wa Ujerumani
Wasalafi wa Ujerumani Picha: Imago/C. Mang

Watu hao wanapinga mambo ya kidunia kama vile katiba ya Ujerumani. Msingi wa maisha yao ni sharia za kidini. Wasalafi wenye itikadi kali wapo tayari kumwaga damu ili kuendeleza itikadi zao. Kwa mujibu wa idara ya usalama wa ndani ya jimbo la Northrhine Westphalia wapo waumini wapatao 3000 katika jimbo hilo na 800 miongoni mwao wanazingatiwa kuwa watu wa hatari ambao wakati wote wako tayari kumwaga damu.

Asilimia 12 ya watu hao ni wanawake na miongoni mwa wale waliokwenda nchini Iraq na Syria asilimia 28 au hata mara mbili ya idadi hiyo walikuwa wanawake. Ndiyo sababu wanawake wa madhehebu ya salafi na watoto wao wanamulikwa kwa makini na idara ya usalama, na hasa wale wanaorejea kutoka sehemu iliyoitwa dola la kiislamu.Watoto wao waliorejea kutoka dola la kiislamu sasa wanakwenda shule na wadogo wanapelekwa kwenye shule za chekechea. Mwakilishi wa mpango wa kuwaondolea kasumba ya itikadi kali watu hao Kaan Orhon anataka watu hao wawekewe miundombinu maalumu kwa ajili ya kuwasaidia.

Ngome kuu ya wasalafi katika jimbo la Northrhine Westphalia ni mji wa Bonn lakini katika miji mingine  kadhaa watu hao pia wapo kama vile Dortmund na Mönchengladbach. Harakati za wasalafi zinagonga vichwa vya habari mara kwa mara katika mji wa Bonn ambao hapo zamani ulikuwa mji mkuu wa Ujerumani.

Mnamo mwaka 2012 ambapo maandamo ya watu hao yalileta hatari. Watu hao walipambana na kundi la wajerumani wenye itikadi kali ya mrengo wa kulia waliokuwa na mabango ya kumkejeli mtume wa dini ya kiislamu. Waandamanaji wa kundi la wasalafi walimshambulia mshiriki mmoja wa kijerumani na polisi wawili kwa kisu. Watu hao watatu walijeruhiwa vibaya.

Mnamo mwaka 2008 ndugu wawili Yassin na Mounir Chouka kutoka mji wa Bonn walikwenda kwenye mpaka wa Pakistan na Afganistan ambako walitengeneza ukanda wa video na kutoa miito ya kufanya mashambulio ya kigaidi nchini Ujerumani. Mhubiri Abu Dujana pia anaishi mjini Bonn.  Abu Dujana ni kiongozi mmojawapo muhimu katika kampeni ya kugawa nakala za Koran.

Zoezi la wasalafi la kugawa nakala za Koran
Zoezi la wasalafi la kugawa nakala za KoranPicha: picture alliance/dpa/J. Stratenschulte

Hata hivyo mandhari ya wasalafi imebadilika katika jimbo la NRW tangu ujio wao mnamo miaka ya 2003/2004. Hayo amesema mkuu wa idara ya usalama wa ndani wa jimbo hilo Burkhard Freier. Ameeleza kwamba hapo awali waliohusika walikuwa na nasaba ya kijerumani. Lengo la hapo awali lilikuwa kufanya kazi ya kueneza itikadi ya kisalafi. Wengi waliofanya kazi hiyo walikuwa mbumbumbu hapo awali hata kama wazazi wao walikuwa watu wa dini.

Lakini tangu kuchakazwa kwa dola la kiislamu mambo yamebadilika kwa wasalafi nchini Ujerumani.

Mkuu wa idara ya usalama ameeleza kuwa tangu wakati huo, familia za wasalafi zinaundwa hatua kwa hatua na zinaimarika. Ameeleza kuwa sasa wako wasalafi wasiohitaji kinachoitwa dola la kiislamu na wala hawahitaji itikadi kali kutoka nje.

Mwandishi:Zainab Aziz/ Esther, von Hein, Matthias

Mhariri:Josephat Charo