1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Seleka wakubali mazungumzo

2 Januari 2013

Wakaazi wa mji wa Bangui bado wanaishi katika hali ya wasiwasi huku hatma ya mji huo ikiwa haijafahamika vizuri wakati wanajeshi wa kulinda amani kutoka nchi za Afrika wakiendelea kumiminika

https://p.dw.com/p/17CCL
Rais Francois Bozize akiwahutubia wafuasi wake
Rais Francois Bozize akiwahutubia wafuasi wakePicha: Reuters

Seleka wasusa kukaa na Bozize

Taarifa zilizotolewa na shirika la habari la Reuters zinasema kwamba muungano wa waasi,nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati Seleka umewataka wapiganaji wake kusitisha harakati za kuwania kuingia mji mkuu ,Bangui na kwamba wawakilishi wa kundi hilo watajiunga na mazungumzo ya amani yanayoandaliwa kufanyika mjini Lebreville nchini Gabon.

Tangazo hilo limetolewa na msemaji wa Seleka Eric Massi kwa njia ya simu kutokea mjini Paris.Hata hivyo msemaji huyo amefahamisha kwamba tayari wako katika mazungumzo na washirika wao kuandaa mapendekezo ya kuumaliza mgogoro huo lakini kilicho bayana ni kwamba suluhisho la kisiasa wanalolitaka ni kuweko kipindi cha mpito ambacho hakitomuhusisha rais Bozize.

Rais Francois Bozize
Rais Francois BozizePicha: Getty Images

Wasiwasi na matumaini

Hata hivyo hali ya wasiwasi bado imetanda katika mji mkuu wa Bangui, baada ya hapo jana kuzuka vurugu kubwa kufuatia kuuwawa kijana mmoja wa kiislamu kwa madai ya kushirikiana na waasi.Vurugu hizo zilisababisha polisi mmoja kuuwawa. Aidha ghasia hizo zimetibuka wakati nchi za kanda hiyo zikiwa zimetuma wanajeshi kuulinda mji mkuu Bangui.

Mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati unaokaliwa na watu 700,000 umeukaribisha mwaka mpya bila ya kujuwa hatma yake itakuwa ipi katika siku na miezi ijayo.Vikosi vya serikali vikiungwa mkono na kikosi cha wanajeshi wa kanda hiyo vimeweka kambi katika eneo la Damar kiasi kilimota 75 kutoka mji mkuu Bangui wakati waasi nao wakiushikilia mji wa Sibut ulioko kiasi kilomita 185 kutoka mji mkuu.

Pamoja na kwamba rais Francois Bozize aliyeko madarakani kwa takriban muongo mmoja,amependekeza kuwa tayari kuongoza serikali ya mseto pamoja na waasi,waasi hao wameonekana kugawanyika juu ya tamko hilo huku kundi moja likitangaza kutoliamini tangazo hilo.

Msemaji wa muungano huo wa waasi wa Seleka ambao ni muungano wa makundi matatu ya waasi wanaozidi kuenea kote nchini amesema hawaamini pendekezo lilotolewa na rais huyo.Koloni la zamani la Jamhuri ya Afrika ya Kati,Ufaransa imeshatamka wazi kwamba haitothubutu kuulinda utawala wa Bozize ingawa inawanajeshi wake kiasi ya 600 katika nchi hiyo kwa ajili ya kulinda tu maslahi yake.

Nchi za Afrika zatuma Jeshi

Nchi zilizoko katika eneo hilo la Afrika ya Kati zimeshatuma wanajeshi katika mji mkuu wa Bangui kuulinda dhidi ya waasi ambao wanaonekana kuyadhibiti maeneo mengi ya taifa hilo la Jamhuri ya Afrika ya Kati na ambao wanamtaka rais Francois Bozize aondoke madarakani.

Jeshi la Jamhuri ya Afrika ya Kati laungwa mkono na kikosi cha wanajeshi wa nchi za Afrika
Jeshi la Jamhuri ya Afrika ya Kati laungwa mkono na kikosi cha wanajeshi wa nchi za AfrikaPicha: dapd

Gabon,Congo Brazaville na Cameroon zimeahidi kutuma wanajeshi zaidi kuungana na wanajeshi wengine 400 kutoka chad ambao tayari wameshapelekwa chini ya kikosi cha mataifa ya Afrika cha kulinda amani FOMAC kuulinda mji wa Damara.Mji huo ndio mji wa mwisho muhimu kabisa ulioko karibu sana na Bangui na ambao waasi wa Seleka walioliteka eneo kubwa la nchi hiyo wakiwa kilomita 160 kutoka mji mkuu wanapania kuufikia kabla ya kuingia Bangui.Takriban wanajeshi 120 kutoka Gabon waliwasili hapo jana katika mji huo wa Damara huku kundi jingine la wanajeshi likitazamiwa kuwasili jioni ya leo.

Aidha kutoka Kongo Brazzaville wanajeshi 120 waliwasili jumatatu huku wanajeshi kutoka Cameroon wakitarajiwa kuwasili mwishoni mwa wiki hii.Kikosi kizima cha kulinda amani cha nchi za Afrika kitaongozwa na jenerali kutoka Gabon kikiwa na wanajeshi 760 mjini Damara.

Mwandishi:Saumu Yusuf

Mhariri:Josephat Charo