1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Seneta Mutula Kilonzo wa Kenya aaga dunia

Mohamed Dahman27 Aprili 2013

Mutula Kilonzo seneta wa jimbo la uchaguzi la Makueni amekutikana akiwa amefariki leo (Jumamosi 27.04.2013) akiwa katika nyumba yake ilioko kwenye shamba la Maanzoni katika jimbo la Machakos

https://p.dw.com/p/18OLs
From left, Cabinet minister, Raila Odinga, opposition politician, Mutula Kilonzo, Leader of the Official Opposition Uhuru Kenyatta and Politician Joseph Kamotho with "No" campaign supporters of the country's draft constitution give details of the killing of three people during one of their rallies at a news conference in Nairobi, Saturday, Nov. 12, 2005. Police in Kenya shot dead three people during a rally by opponents of the country's draft constitution, a senior opposition leader said Saturday. (ddp images/AP Photo/Sayyid Azim)
Mutula KilonzoPicha: AP

Makamo wa rais wa zamani wa Kenya Kalonzo Musyoka ametangaza habari za kifo chake hicho cha kushtusha wakati akihudhuria mazishi huko Tseikuru katika jimbo la uchaguzi la Mwingi Kaskazini.

Sababu ya kifo chake haijulikani isipokuwa taarifa za awali zimedokeza kwamba Kilonzo alikwenda kulala wakati wa usiku na kushindwa kuamka ilipofika saa nne asubuhi. Wafanyakazi wake walishangaa kuona hakuamka hadi saa saba mchana na walilazimika kuvunja mlango ambapo waliukuta mwili ukiwa umelala kitandani.

Naibu Mkuu wa Polisi Grace Kaindi amesema bado hawajui  chanzo cha kifo chake na uchunguzi wa kina utafanyika ikiwa ni pamoja na upasuaji wa mwili. Wakati akithibitisha kifo hicho Kaindi amesema wamejiandaa kuchukuwa hatua zote kujuwa sababu ya kifo hicho. Wafanyakazi waliwaambia polisi kwamba Kilonzo alichelewa kulala hapo jana usiku na alikuwa katika hali ya uchangamfu.

Kilonzo alikuwa sehemu ya Muungano wa CORD unaoongozwa na Raila Odinga
Kilonzo alikuwa sehemu ya Muungano wa CORD unaoongozwa na Raila OdingaPicha: Reuters

Musalia Mudavadi aliekuwa naibu waziri mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa iliopita ametuma rambi rambi zake kwa familia ya marehemu kwa kusema kwamba seneta Kilonzo alikuwa mwanasheria mahiri ambaye alikuwa akihusudiwa na jamii ya mawakili kutokana na hoja zake nzito za kisheria na kujenga vipaji vya wanasheria vijana.

Mudavadi amesema "katika seneti,Kilonzo angelikuwa anasubiriwa kuingiza hewa mpya kwa ahadi ya taifa kutekeleza wajibu wake." Watu wa kwanza kukimbia nyumbani kwa Kilonzo alikuwa ni Bw.Chris Musau mwenyekiti wa Manzoni Lodge ambaye pia ni shemegi wa waziri huyo wa zamani.

Habari za kifo cha Kilonzo zimepokewa kwa fadhaa kubwa na Wakenya wengi kwani wiki chache tu zilizopita alishiriki katika kuwasilisha Mahakama ya Juu pingamizi ya kisheria ya muungano wa Cord dhidi ya matokeo ya uchaguzi wa urais.Kilonzo aliwahi kuwa waziri wa sheria na masuala ya katiba na baadae waziri wa ulinzi wakati wa utawala Mwai Kibaki. Aliwahi pia kuzitumikia nyadhifa mbali mbali tokea ajiunge na siasa.

Marehemu Mutula Kilonzo aliwahi kuwa mwanasheria binafsi wa rais mstaafu Daniel Arap Moi
Marehemu Mutula Kilonzo aliwahi kuwa mwanasheria binafsi wa rais mstaafu Daniel Arap MoiPicha: AFP/Getty Images

Mutula amejipatia elimu yake katika Shule ya Msingi ya Mboni na Shule ya Sekondari ya Machakos kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam hapo mwaka 1969 na kuhitimu kwa kujipatia Shahada ya Sheria ya Daraja la Kwanza. Pia aliwahi kuwa waziri Maendeleo ya Jiji la Nairobi hadi pale alipochaguliwa kuwa waziri Sheria na Masuala ya Katiba hapo tarehe 4 mwezi wa Mei mwaka 2009 na baadae kuwa waziri wa elimu.

Huko nyuma aliwahi kuwa mwanasheria binafsi kwa rais mstaafu Daniel arap Moi. Mara ya kwanza Mutula Kilonzo aliingia bungeni akiwa mbunge wa kuteuliwa kwa tiketi ya chama cha KANU hapo mwezi wa Januari mwaka 2003. Hadi kufa kwake tarehe 27 mwezi wa April 2013 alikuwa seneta wa jimbo la uchaguzi la Makueni lilioko mashariki ya Kenya.

Mwandishi: Mohamed Dahman/Kenyas' Daily Nation/ The Standard

Mhariri: Bruce Amani