1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Seneta Obama, awasili Ujerumani.

Nyanza, Halima24 Julai 2008

Mgombea Urais wa Marekani kupitia chama cha Democratic Barack Obama amewasili Berlin, Ujerumani, ikiwa ni nchi yake ya kwanza barani Ulaya, katika ziara yake ya kutembelea baadhi ya nchi barani humu na mashariki ya kati.

https://p.dw.com/p/Eivg
Seneta Barack Obama, amewasili leo nchini Ujerumani.Picha: AP

Seneta Barack Obama amewasili leo nchini Ujerumani baada ya kumaliza ziara yake Israel, ambako alikutana na viongozi wa nchi hiyo, na pia kupata nafasi ya kutembelea Ramallah, ukingo wa magharibi na kufanya mazungumzo na na Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas.

Akiwa Israel Barack Obama pia alielezea kuendeleza uhusiano usioyumba wa nchi yake na Israel.

Aligusia mpango wa nyuklia wa Iran, ameahidi kushiriki haraka katika mpango wa kutafuta amani, mashariki ya kati iwapo atachaguliwa.

Kwa upande wake Rais Shimon Peres wa Israel, alimtakia kila la kheri Obama iwapo atafanikiwa kuwa Rais wa nchi hiyo na kwamba matumaini yao makubwa ni kwamba atakuwa rais wa kusifika Marekani .''

Barack Obama, ameianza leo ziara yake barani Ulaya ambapo anakutana na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel pamoja na Waziri wa Mambo ya nchi za nje Frank-Walter Steinmeier, ambapo watajadili masuala mbalimbali ikiwemo Biashara, mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na kuzungumzia kuhusian ana Umoja wa Kujihami wa nchi za magharibi.

Leo jioni pia anatarajiwa kutoa hotuba muhimu, kuhusu uhusiano kati ya Ulaya na Marekani katika mkutano wa hadhara, utakaofanyika mjini Berlin, ambapo magazeti ya Ujerumani wanailinganisha na ile hotuba maarufu aliyoitoa aliyekuwa Rais wa Marekani John F Kennedy mwaka 1963, alipojitambulisha kama yeye ni mkazi wa Berlin, lakini Obama atatoa hotuba yake leo mbele ya nguzo ya ushindi kwenye viwanja vilivyoko katika bustani ya Tiergarden, baada ya kuzuiwa kuitoa katika lango kuu la Brandenburg.

Hapo awali kulitokea tofauti baina ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Waziri wake wa Mambo ya nchi za nje Frank-Walter Steinmeier, ambapo Bibi Merkel hakutaka Barack Obama ahutubie katika eneo la lango kuu la Brandenburg mjini Berlin, kwa madai kuwa bado hajawa Rais wa Marekani kwani kwa sasa ni mgombea tu, kutokana na kwamba ni marais tu ndio wanaopata heshima kuhutubia katika eneo hilo.

Wakati wa uongozi wa Kansela Gerhard Schroeder, uhusiano kati ya Ujerumani na Marekani ulidhoofika mno kuliko kipindi chochote, baada ya vita vikuu vya pili vya dunia, kutokana na kupinga kwake uvamizi wa Marekani nchini Iraq mwaka 2003.

Lakini mrithi wake kansela Merkel alijitahidi sana kurekebisha uhusiano na Marekani na kuibuka kuwa mshirika mkubwa wa Rais George W Bush wa Marekani.

Baada ya kuitembelea Ujerumani, Barack Obama ataendelea na ziara yake barani Ulaya, kwa kuelekea Ufaransa na baadaye Uingereza.