1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Seneta wa Marekani azuru Myanmar

14 Agosti 2009

Seneta wa Marekani Jim Webb amewasili Myanmar kwa mazungumzo na kiongozi wa kijeshi wa nchi hiyo Jenerali Than Shwe.

https://p.dw.com/p/JBDb
Nyumbani kwar Aung San Suu Kyi alikoanzia kutumikia kifungo cha nyumbani cha miezi 18Picha: AP

Hii ni mara ya kwanza kwa afisa wa ngazi za juu wa Marekani kukutana na kiongozi huyo wa utawala wa kijeshi katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja.

Seneta huyo wa jimbo la Virginia wa chama cha Demokratik Jim Webb aliwasili mjini Naypidaw hii leo akitokea Laos alikoanzia ziara yake ya eneo hilo itakayodumu  wiki mbili.

Ziara hiyo imefanyika wakati ambapo kiongozi wa upinzani Aung San Suu Kyii ameanza kutumikia hukumu mpya ya kifungo cha nyumbani kwa kipindi cha miezi 18 baada ya kumpokea mgeni wake mwezi wa Mei akiwa kizuizini kinyume na taratibu zilizowekwa.

Mgeni huyo, raia wa Marekani John Yettaw naye pia alihukumiwa kifungo cha miaka saba jela na kazi ngumu.Awali Bibi Suu Kyii alipewa hukumu kama hiyo ila ilipunguzwa makali kufuatia amri ya kiongozi wa Myanmar Jenerali Than Shwe.

Vyombo vya habari vya serikali ya Myanmar vimeeleza kuwa hukumu hiyo ya kifungo cha nyumbani ni hatua kubwa inayoashiria mabadiliko nchini humo na itakuwa na manufaa kwa pande zote husika.      

Kwa mujibu wa afisa mmoja wa Myanmar ambaye hakutaka jina lake lifahamike,Seneta Webb aliye na uhusiano wa karibu na Rais Barack Obama atakutana na Jenerali Than Shwe kesho mchana.Taarifa hizo zimethibitishwa na afisi ya Seneta Webb. 

Mwanasiasa huyo wa ngazi za juu ambaye ni mwenyekiti wa Kamati inayohusika na masuala ya uhusiano wa kigeni katika eneo la Asia na Pasifiki anatarajiwa kuelekea  kwenye mji mkuu wa biashara wa Yangon baadaye hapo kesho.    

Kulingana na msemaji wa Chama cha upinzani cha Bibi Suu Kyii cha National League for Democracy Nyan Win, uongozi wa Myanmar umewaalika wawakilishi wake wa ngazi za juu mjini Naypidaw hii leo kasha wataelekea mjini Yangon wakati wa mchana.

Hata hivyo bado haijabainika iwapo watakutana na Jenerali Than Shwe au Seneta Webb wa Marekani ila wameelezwa kuwa watakutana na mtu muhimu.Msemaji huyo wa chama cha NLD ameipokea vizuri taarifa ya Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa inayoelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu hukumu ya Bibi Suu Kyii kadhalika uamuzi wa Umoja wa Ulaya wa kuiongezea mbinyo Myanmar.

Nordkorea Sanktionen der UN
Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: AP

Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwezi huu Balozi John Sawers wa Uingereza alisisitizia msimamo wao.

´´Wanachama wa Baraza la usalama wanaisisitiza Myanmar umuhimu wa kuwaachia huru wafungwa wote wa kisiasa.Kutokana na hali hiyo Baraza hili limetimwa wasiwasi mwingi na hukumu aliyopewa Aung San Suu Kyi vilevile athari zake katika siasa´´:

Umoja wa Ulaya kwa upande wake uliamua kuiongezea mbinyo Myanmar kwa kuwawekea vikwazo vya usafiri majaji waliohusika katika kesi hiyo pamoja na kuzizuwia mali zao zilizohifadhiwa katika mabenki ya mataifa barani Ulaya.Hat hivyo Jumuiya ya mataifa  ya eneo la Kuisni mashariki mwa Asia ASEAN ina mtazamo tofauti kuhusu suala hilo kama alivyoeleza Waziri Mkuu wa Thailand Abhisit Vejjajiva

Abhisit Vejjajiva Regierungschef Thailand
Waziri Mkuu wa Thailand Abhisit Vejjajiva.Picha: AP

´´Nakubali kuna tatizo hapa ila uamuzi wa kuiwekea vikwazo si kamilifu.Nadhani kwavile wameunda mpango maalum wa kulitafutia suala hilo ufumbuzi ni ishara kwamba juhudi zaidi zinahitaji´´.

Kwa upande mwengine Ikulu ya Whitehouse ya Marekani imefurahishwa na ziara hiyo inayoisisitizia serikali ya Myanmar umuhimu wa mtazamo wao kuhusu masuala ya uongozi bora.

Hata hivyo wanadiplomasia wameyapuuza madai kwamba Seneta Webb yuko katika harakati za kumuombea msamaha John Yettaw aliyehukumiwa kifungo cha miaka 7 jela na kazi ngumu baada ya kumtembelea nyumbani mwake kiongozi wa upinzani Aung San Suu Kyi.

Seneta Webb wa Virginia yuko katika ziara rasmi ya mataifa matano katika eneo la Kusini Mashariki mwa Asia na anatarajiwa kuzizuru Thailand,Cambodia na Vietnam.

Mwandishi:Thelma Mwadzaya /DPAE-AFPE

Mhariri:M.Abdul-Rahman