1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SEOUL: Maandamano ya kuipinga Korea Kaskazini yafanywa

21 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD0N

Watetezi takriban 3,000 wa Korea Kusini, wanaopinga utawala wa kikomunisti, wameandamana leo mjini Seoul kuilaani Korea Kaskazini kwa kufanya jaribo lake la kwanza la zana za kinyuklia.

Aidha waandamanaji hao wameihimiza Korea Kusini ikomeshe misaada yote ya kiuchumi kwa Korea Kaskazini.

Walipiga kelele za kutaka kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-il aondolewe madarakani na mabomu ya kinyuklia ya nchi hiyo yaharibiwe.

Watetezi hao walibeba bendera za Korea Kusini na kuinua mishumaa iliyokuwa ikiwaka wakati wa mkutano wa hadhara nje ya jengo la serikali ya mji katikati mwa mji wa Seoul.

Watetezi hao pia wamemtaka rais Roh Moo-Hyun wa Korea Kusini awachane na sera ya mdahalo, maridhiano na mabadilishano na Korea Kaskazini na afutilie mbali miradi yote na nchi hiyo, ikiwa ni pamoja na kiwanda kikubwa kilicho katika mji wa mpakani wa Kaesong na safari za kitalii kwenda eneo la mapumziko la Mlima Kumgang.

Waandamanaji wanadai Korea Kaskazini imetumia fedha ilizopata kutokana na miradi hiyo kutengeza mabomu ya kinyuklia.