1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utawala wa rais Trump umeanza kutekeleza masharti mapya

29 Juni 2017

Utawala wa rais Trump unaanza leo kutekeleza masharti mapya juu ya upatikanaji wa viza kwa waombaji kutoka mataifa sita ya Kiislamu, ambayo yanawataka waombaji wapya kuwa na watu wanaohusiana nao kifamilia

https://p.dw.com/p/2fdHB
USA Trump signiert Durchführungsbeschluss zum Einreiseverbot
Picha: Reuters/C. Barria

Hatua hiyo inayoyahusisha mataifa yaliyo na Waislamu wenhgi kama vile Iran, Libya, Somalia, Sudan, Syria na Yemen imetumwa katika balozi zote za Marekani nje ya nchi hiyo.

Masharti hayo mapya yanayoanza kufanya kazi siku leo, yanaelezea mahusiano ya kifamilia kama mzazi, mke ama mume, mtoto wa kiume ama wa kike kuwa moja ya vigezo muhimu kuingia nchini Marekani.

Masharti hayo yanajiri baada ya Mahakama ya Juu nchini Marekani kuidhinisha kwa muda agizo la Rais Donald Trump ambalo lilikosolewa kuwa marufuku dhidi ya Waislamu.

Hata hivyo, viza ambazo tayari zimekubalika hazitotafutwa, lakini maagizo yaliyotolewa na wizara ya mambo ya nje hapo jana yalisema kuwa vigezo hivyo pia vinawahusu wakimbizi wote wanaotaka kuingia sasa, isipokuwa kwa wale ambao bado wanasubiri kukubaliwa kuingia Marekani.

Mbali ya wazazi na ndugu wa familia moja, jamaa wengine wote kiukoo hawazingatiwi na amri hiyo ya Trump kuwa ndungu wa karibu, kulingana na taarifa iliyotumwa katika balozi mbalimbali za Marekani jana Jumatano.

Serikali ya Trump inasema lazima uhusiano huo wa kifamilia uwe rasmi, uwekewe kumbukumbu na utengenezwe katika mfumo wa kawaida na sio kwa lengo la kuepuka marufuku hii ya kupinga uingiaji wa wageni kutoka nchi hizo sita.

Hata hivyo, waandishi wa habari, wanafunzi, wafanyakazi au wahadhiri ambao  wana vibali kamili au mikataba ya ajira nchini Marekani wataendelea kuingia bila ya kupigwa marufuku.

Amri hii mpya itabakia mpaka Mahakama ya Juu itakapotoa masharti ya mwisho juu ya swala hilo. Majadiliano mbele ya majaji hayatofanyika mpaka angalau Oktoba, hivyo sheria za muda mfupi zitabaki kutumika.

USA Washington Supreme Court
Mahakama kuu ya MarekaniPicha: picture-alliance/AP Photo/J. S. Applewhite

Muda mfupi tu baada ya kuingia madarakani, Rais Trump alianza mkakati wa sera ambayo itawazuia Waislamu kutoka nchi sita kuingia Marekani. Alisema kuwa sera hiyo inahitajika ili kuilinda Marekani na magaidi, kauli ambayo aliitumia sana wakati wa kampeni yake.

Lakini katika hatua ya kwanza, marufuku hiyo ilipingwa mahakamani, na pia kusababisha mtafaruku katika viwanjwa vya ndege duniani na kuyafanya mashirika mengi ya ndege kukumbwa na matatizo.

USA Virginia Dulles Airport
Mgomo wa kupinga amri ya Trump Dulles Airport mwezi wa FebruaryPicha: DWP. Dadhania

Uamuzi huu mpya bado sio rahisi kwa wahamiaji. Sasa hata wale wanaomba makaazi Marekani, lazima wathibitishe kuwa wana watu wanaohusiana kifamilia. Kwa ufupi, washindi ni wale watakaoweza kuthibitisha kuwa ni wazaliwa wa Marekani, wamemaliza shule ya sekondari, na wamefanya kazi kwa muda wa miaka miwili kwa kazi ambayo ilihitaji mafunzo ya miaka miwili pia.

Mwandishi: Najma Said

Mhariri: Mohammed Khelef