1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siasa za wahamiaji za EU zamsaidia Merkel?

26 Juni 2018

Mkutano mdogo wa kilele ambao ulioandaliwa Brussels kujadili sera ya uhamiaji na uliofanyika kwa ombi la Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, ambaye alikuwa kwenye shinikizo nchini mwake, haukutoa maamuzi yoyote.

https://p.dw.com/p/30Hnk
Deutschland 2012 | 25. Parteitag der CDU | Horst Seehofer & Angela Merkel
Picha: Imago/J. Sielski

Lakini hotuba za viongozi wa nchi 16 waliohudhuria zinaashiria safari inakoelekea. Swali ni iwapo hatua zilizopangwa kuchukuliwa zitamsaidia Merkel katika mzozo na Waziri wake wa mambo ya ndani Horst Seehofer au iwapo mwanasiasa huyo wa chama cha Christian Social Union, CSU, atanufaika zaidi.

Seehofer anasisitiza suluhisho la muda mfupi la wanaotafuta hifadhi kukataliwa kuingia Ujerumani wanapofika mpakani. Angela Merkel naye matumaini yake ya suluhisho ni maafikiano yatakayotokana na mazungumzo baina ya nchi kuhusu suala la kuwarudisha wahamiaji hao walikotoka. Mkutano huo wa Brussels ulitoa mapendekezo kadhaa na je mapendekezo haya yatakuwa na athari gani kwa siasa za ndani za Ujerumani?

Baadhi ya nchi zinataka kubuniwe vituo vya mapokezi ya wakimbizi Libya

Pendekezo la kwanza lilikuwa kuongeza usalama wa mpaka mkubwa wa nchi za Umoja wa Ulaya. Kutimiza hili, walinzi wapya 10,000 wanastahili kusajiliwa kufikia mwaka 2021 kujiunga na shirika la ulinzi wa mipaka la Umoja wa Ulaya Frontex. Lakini swali ni je, walinzi hawa wanastahili kuilinda Ulaya dhidi ya nani?

EU-Minigipfel
Baadhi ya viongozi 16 waliohudhuria mkutano mdogo wa kilele BrusselsPicha: picture alliance/AP Photo/Y. Herman

Je, wanastahili kuwazuia wakimbizi, wanaotafuta hifadhi na wahamiaji wote? Iwapo ni hivyo basi walinzi wengi zaidi watahitajika ili kuulinda mpaka wa majini katika bahari ya mediterenia. Pendekezo hili halitokuwa na athari kubwa katika mzozo unaoendelea katika serikali ya muungano ya Merkel kwani ni jambo linalohitaji muda na Horst Seehofer anataka hatua za haraka zichukuliwe.

Kuna wazo la kubuni vituo vya mapokezi ya wahamiaji vitakavyokuwa nje ya Ulaya. Austria na nchi nyengine zinalipigia debe wazo hili ambapo wanataka vituo hivyo viwekwe nchini Libya au kwengineko Kaskazini mwa Afrika ili kuwachukua wahamiaji, wakimbizi na watafuta hifadhi watakapookolewa kutoka bahari ya Mediterenia. Katika vituo hivyo watakaguliwa kubaini ni nani mwenye nafasi ya kupewa hifadhi na ni nani asiyestahili. Wazo hili si jipya kwa kuwa lilipendekezwa miaka 14 iliyopita na Otto Schily mwanasiasa wa chama cha Social Democratic, SPD hapa Ujerumani. Waziri Seehofer haoni kwamba wazo hili ni baya ingawa tatizo ni kwamba huenda likachukua miezi kama si miaka kutekelezwa.

Kuwarejesha wahamiaji walikotoka ni baadhi ya mapendekezo mengine

Mkutano huo wa Brussels pia ulitoa wazo la kurudishwa makwao wanaotafuta hifadhi. Lengo la wazo hili ni kuwarudisha angalau asilimia 70 ya wanaotafuta hifadhi katika nchi zao na Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya imekuwa ikitaka hili lifanyike.

Libyen Migranten aufSchlauch von Schiff der deutschen NGO Mission Lifeline gerettet
Wahamiaji kutoka Afrika katika bahari ya MeditereniaPicha: picture-alliance/AP/Mission Lifeline/H. Poschmann

Ujerumani, Italia na nchi nyengine bado hazijatimiza hili. Nchini Ujerumani suala hili limejikokota kutokana na masuala ya kisheria. Mapendekezo mengine yalikuwa ni kuwarejesha wahamiaji walikotoka pindi tu wanapofika mpakani na nchi husika kufanya  mazungumzo baina yao ili kutafuta suluhu, hilo likiwa ndilo jambo linalopigiwa debe na Kansela Merkel. Huenda Seehofer akayapenda mapendekezo yote haya ila ni sharti yatekelezwe kwa haraka.

Kiujumla Kansela Merkel hajapata suluhu la "Umoja wa Ulaya". Sasa kinachosubiriwa ni Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Ulaya utakaofanyika Alhamis na Ijumaa ambapo nchi zote 28 zitakuwepo. Baada ya hapo Seehofer wa chama cha CSU ataamua iwapo atajitenga na kuihatarisha serikali ya mseto ambapo vyama vya Christian Democratic Union, CDU, na SPD ndivyo vitakavyosalia.

Mwandishi: Bernd Riegert

Tafsiri: Jacob Safari

Mhariri: Josephat Charo