1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali na LRA wasaini makubaliano mengine kuelekea amani

1 Machi 2008

-

https://p.dw.com/p/DG7o

KAMPALA

Serikali ya Uganda imesema hapo jana kwamba imetia saini makubalino na waasi wa LRA ya kuweka chini silaha.Hatua hiyo ni ya mwisho kabla ya kusainiwa makubaliano kamili ya amani ya kumaliza zaidi ya miaka 20 ya vita.

Akizungumza kutoka Juba huko Sudan msemaji wa Ujumbe wa serikali ya Uganda katika mazungumzo ya kusaka amani ya kaskazini mwa Uganda Captain Chris Magezi amesema hiyo ni hatua nyingine kubwa na muhimu kuelekea amani katika eneo hilo.Hii inamaanisha waasi wa LRA lazima waweke chini silaha, waruhusiwe kurudi nchini na kujumuishwa tena katika jeshi la taifa.

Wiki iliyopita pande hizo mbili serikali na waasi zilitia saini mapatano ya kudumu ya kukomesha mapambano ambayo yamesababisha kuuwawa kwa maelfu ya raia na wengine milioni mbili wakaachwa bila maakazi kaskazini mwa Uganda.Mapigano katika eneo hilo yalianza tangu mwaka 1988 wakati kiongozi wa LRA Joseph Kony alipoongoza vita dhidi ya serikali.Hata hivyo Kony ameapa kutosaini mkataba wa mwiho wa amani hadi pale mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC ya mjini The Hague itakapoondoa mashtaka rasmi dhidi yake na viongozi wengine wa LRA.Wabunge wa kaskazini mwa Uganda jana waliitaka serikali kuiomba mahaka ya The Hague kufuta warranti wa kukamatwa waasi hao kwa ajili ya amani kaskazini mwa Uganda.Makubaliano ya mwisho ya amani yanatazamiwa kutiwa saini mwezi huu wa Marchi.