1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali Ujerumani zatofautiana kuhusu kuondoa vizuizi

Admin.WagnerD25 Mei 2020

Serikali kuu na zile za majimbo nchini Ujerumani leo zimeingia kwenye mkwamo kuhusu namna ya kuondoa vizuizi vya watu kujitenga, katika hatua zake za kukabiliana na janga la corona.

https://p.dw.com/p/3ckDI
Deutschland Berlin | Pressekonferenz Angela Merkel
Picha: Getty Images/O. Messinger

Hali ya kuhitilafiana imezuka baada ya waziri mkuu wa jimbo la mashariki la Thuringia Bodo Ramelow kusema siku ya Jumamosi kuwa ataondoa masharti ya watu kujitenga na kuvaa barakoa kwa kuhimiza mbinu za kawaida za kujikinga na virusi vya corona.

Ingawa serikali za majimbo ya Ujerumani ndiyo zinahusika na kutunga kanuni za maisha ya kila siku ya wakaazi wake pendekezo la Ramelow limezusha hofu miongoni mwa maafisa wa ngazi ya juu wa serikali kuu, kwamba litasababisha kupotea kwa nidhamu ya umma katika kupambana na janga la COVID-19.

Waziri wa Afya wa Ujerumani Jens Spahn ameliambia gazeti la Bild kwamba wajerumani hawapaswi kufikiri kuwa janga la virusi vya corona limekwisha na kusisitiza njia za kujitenga, kuvaa barakoa na kuzingatia usafi ndiyo madhubuti katika kupambana na kadhia ya COVID-19.Ujerumani yakabiliwa na mdororo wa kiuchumi

Tangu mwezi uliopita visa vya mambukizi mapya ya virusi vya corona vimepungua nchini Ujerumani hatua iliyowezesha kufunguliwa tena kwa maduka, mikahawa, majumba ya makumbusho pamoja na makanisa.

Licha ya wasiwasi uliopo serikali ya bibi Merkel inataka kuongeza kasi ya kufungua shughuli za uchumi na kurejea kwa maisha ya kawaida ikiwa ni pamoja na kuruhusu idadi kubwa ya watu kuanza kukutana kwenye maeneo ya wazi.

Premierminister Shinzo Abe Japan  Ausweitung Maßnahmen Coronavirus
Waziri mkuu wa Japan, Shinzo Abe ametangaza kuondoa hali ya dharura nchini humoPicha: Reuters/T. Ohsumi

Kwengineko Japan leo imetangaza kuondoa hali ya dharura iliyowekwa tangu katikati ya mwezi Aprili kwenye mji mkuu Tokyo na mji mwingine mkubwa wa Hokkaido uliopo kaskazini ya nchi hiyo kukabiliana na kusambaa virusi vya corona.

Uamuzi huo umetangazwa na waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe siku sita kabla ya tarehe iliyopanga hapo kabla."Kwa maana ya kufanya matamasha tunaweza kuanza taratibu huku tukichukua tahadhari ya kuzuia kusambaa kwa virusi. Hatupaswi kupiga marufuku matamasha kwa sababbu ya kitisho cha maambukizi. Kuanzia sasa tunahitaji kudhibiti hatari ya maambukizi na kutafakari jinsi ya kuendesha matamasha hayo. Hilo ni muhimu" alisema Abe

Katika hatua nyingine  Umoja wa Ulaya unatarajiwa baadaye leo kutangaza mpango wa uokozi wa Euro Trilioni moja utakaoyasaidia mataifa wanachama kukabiliana na athari za uchumi zilizosababishwa na janga la virusi vya corona.

Mpango huo utawekwa wazi na rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen ambaye anatumai utasawazisha mgongano uliopo miongoni mwa mataifa wanachama wa umoja huo.

Mataifa kadhaa ya Ulaya yamegawika kuhusu jinsi ya kufufua uchumi huku Uhispania na Italia, miongoni mwa mataifa yaliyoathiriwa vibaya na virusi vya corona yakiyatuhumu mataifa tajiri kama Ujerumani kupuuza umuhimu wa kuyapatia msaada wa kunusuru uchumi wao.