1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuwashughulikia wakimbizi wanaoomba hifadhi

6 Novemba 2015

Kansela Merkel ambaye amekuwa akiongoza juhudi za Umoja wa Ulaya katika kulishughulikia suala la mgogoro wa wakimbizi Ulaya ametangaza mipango ya kuharakisha utaratibu wa kuwashughulikia wanaoomba hifadhi ya ukimbizi

https://p.dw.com/p/1H11i
Kansela Angela Merkel Horst Seehofer na Sigmar Gabriel
Kansela Angela Merkel Horst Seehofer, na Sigmar GabrielPicha: picture-alliance/dpa/B.v.Jutrczenka

Mipango hiyo imefikiwa baada ya kuwepo mazungumzo ya kina kati ya washirika katika serikali ya Ujerumani

akubaliano hayo yanaweka wazi kwamba watu wanaoomba hifadhi ya ukimbizi nchini Ujerumani watalazimika kurudishwa walikotokea ndani ya kipindi cha wiki tatu endapo maombi yao yatakataliwa,katika kile ambacho Kansela Angela Merkel amekiita ni hatua nzuri na muhimu ya kuelekea mbele katika kukabiliana na mgogoro huo.Aidha ikiwa muombaji hifadhi ya ukimbizi ataamua kukata rufaa kesi yake itashughulikiwa ndani ya wiki mbili .Kwa mujibu wa mipango hiyo kuna vituo vitatu hadi vitano vitakavyoanzishwa kote nchini Ujerumani vitakavyokuwa na dhamana ya kuzidurusu fomu za maombi ya ukimbizi.

Wakimbizi wanaolengwa katika mpango huo wa mwanzo ni wale wanaotokea katika zile nchi zinazotajwa kuwa salama katika eneo la Balkan ambao hawastahili kupewa hadhi ya ukimbizi pamoja na wale waliopigwa marufuku kurudi nchini Ujerumani.Wakimbizi watakaoathirika kutokana na mpango huo ni pamoja na wale ambao tayari wameshatuma maombi yao ya kuomba hifadhi ya ukimbizi muda mrefu na wale ambao hawajapata vitambulisho rasmi.

Hatua hiyo kali ya Merkel kuhusu sera ya uhamiaji imeungwa mkono na Sigmar Gabriel kiongozi wa chama mshirika katika serikali cha sera za wastani za mrengo wa kushoto SPD pamoja na Horst Seehofer kiongozi wa chama cha kihafidhina cha CSU kutoka Bavaria ambacho ni chama ndugu na CDU chama kinachoongozwa na Kansela Angela Merkel. Kwa maana hiyo,mpango uliotangazwa jana na Merkel unaashiria kufikiwa maridhiano ya pamoja katika serikali ya mseto ya Merkel iliyokuwa katika mfarakanokatika wiki za hivi karibuni kufuatia masuala kadhaa ikiwemo pendekezo la kutengwa maeneo maalum mapakani ya kupokelewa kwa muda wakimbizi pamoja na sera ya kansela Merkel ya kuacha milango wazi kwa wakimbizi wanaotaka kuingia Ujerumani.

Wakimbizi wakisubiria mgao wa chakula katika kituo cha kupokea wakimbizi Lesbos
Wakimbizi wakisubiria mgao wa chakula katika kituo cha kupokea wakimbizi LesbosPicha: Reuters/A. Konstantinidis

Kimsingi kwa kipindi cha miezi miwili iliyopia Kansela Merkel amekuwa akishikilia msimamo kwamba Umoja wa Ulaya unaweza kukabiliana na mmiminiko wa wahamiaji bila ya kufunga mipaka yake au kujenga uzio na kuapa kwamba nchi yake itawapa makaazi wakimbizi wote watakaothibitika kuwa wanastahili kupewa hifadhi hiyo.

Takwimu rasmi zinasema kwamba Ujerumani itachukua wakimbizi 800,000 mwaka huu lakini wizara ya mambo ya ndani inasema tayari imeshawaandikisha wakimbizi wapya 758,000 katika kipindi chote cha mwezi Oktoba kwahivyo ni dhahiri inaonesha idadi iliyotajwa mwanzo itapindukia.Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya imeshasema kwamba kwa ujumla idadi ya wahamiaji na waombaji hifadhi ya ukimbizi itafikia milioni 3 kufikia mwaka 2017.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri :Daniel Gakuba