1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Msumbiji na upinzani wasaini mkataba wa amani

John Juma
2 Agosti 2019

Serikali ya Msumbiji na upinzani Renamo wamesaini makubaliana ya kihistoria kumaliza uhasama ambao umedumu kwa miaka mingi. Baadhi ya wanachama wa Renamo wanaosalimisha silaha watajumuishwa katika jeshi na polisi.

https://p.dw.com/p/3ND7P
Friedensvertrag Mosambik
Picha: DW/A. Sebastião

Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi na kiongozi wa upinzani nchini humo Ossufo Momade wamesaini makubaliano ya kihistoria yanayolenga kumaliza rasmi miongo mingi ya uhasama. 

Makubaliano hayo ya kihistoria yamesainiwa katika mbuga ya kitaifa ya jimbo la kati nchini Msumbiji, takriban miaka 27 tangu mwisho wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya taifa hilo la kusini mwa Afrika.

Mkataba huo uliosainiwa jana Alhamisi, unamaliza mchakato mrefu wa mazungumzo ya amani ulioanzishwa na kiongozi wa kihistoria wa chama cha upinzani Renamo Afonso Dhlakama aliyefariki mwezi Mei mwaka uliopita, na pia unajiri miezi miwili tu kabla ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba.

Rais Nyusi: Makubaliano yaanzisha enzi mpya Msumbiji

Rais Nyusi amesema makubaliano hayo yanafungua enzi mpya ya historia ya Msumbiji, ambapo hakuna raia wa Msumbiji atakayehitajika kutumia silaha kusuluhisha mzozo.

"Tunajua migogoro ya vita imesababisha vifo vya ndugu zetu wengi na uharibifu wa mali binafsi. Kama Wasumbiji tumeweka kumbukumbu za uchungu kuhusu kipindi kigumu cha historia yetu kama funzo la kuzuia isijirudie.” Amesema Rais Nyusi.

Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi na kiongozi wa Renamo Ossufo Momade wakisaini makubaliano ya kusitisha uhasama
Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi na kiongozi wa Renamo Ossufo Momade wakisaini makubaliano ya kusitisha uhasamaPicha: DW/A. Sebastião

Naye kiongozi mpya wa Renamo aliyechukua usukani baada ya Dhlakama Ossufo Momade, amesema wanataka kuwahakikishia watu na dunia kwa ujumla kwamba wameizika dhana ya kutumia vita kama njia ya kusuluhisha tofauti zao.

"Hii ni tarehe ya kihistoria kwa sababu baada ya miaka mingi ya migogoro sisi kama ndugu, tumejitolea kuweka amani inayotakiwa na wote kwa manufaa ya nchi.” Mamade amesema.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe Msumbiji

Punde tu baada ya Msumbiji ilipopata uhuru wake kutoka kwa Wareno mnamo mwaka 1975, Renamo iliongoza vita vikali vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 16 dhidi ya serikali ya chama cha Frelimo. Vita hivyo vilisababisha vifo vya watu milioni moja na vilimalizika mwaka 1992.

Mkataba wa amani uliosainiwa 1992 ulivunjika 2013

Baadaye vuguvuvgu la waasi liliingia katika siasa kufuatia mkataba wa amani uliosainiwa mwaka 1992 mjini Rome nchini Italia na kuwezesha uchaguzi wa vyama vingi mwaka 1994.

Vuguvugu la waasi Renamo lilishindwa hata katika chaguzi za baadaye. Lakini Oktoba 2013, Renamo ilitangaza mwisho wa mkataba wa amani wa 1992, baada ya jeshi kufanya msako kambi yake ya msituni eneo la kati la Sathundjira.

Afonso Dhlakama ambaye (marehemu kwa sasa) aliyekuwa kiongozi wa Renamo ndiye aliyeanzisha mchakato wa mazungumzo ya amani kati ya chama chake na serikali.
Afonso Dhlakama ambaye (marehemu kwa sasa) aliyekuwa kiongozi wa Renamo ndiye aliyeanzisha mchakato wa mazungumzo ya amani kati ya chama chake na serikali.Picha: DW/A. Sebastiao

Mapigano mapya yalizuka kati ya serikali na wapiganaji wa Renamo kati ya mwaka 2013 na 2016.

Tangu 2016, serikali na Renamo wamekuwa wakifanya mazungumzo ya amani. Licha ya kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe na kundi hilo kujigeuza kuwa chama cha siasa, liliendelea kuwa na kundi au tawi lenye silaha.

Wanachama wa Renamo wanaosalimisha silaha kujumuishwa kwenye jeshi na polisi

Mnamo Jumanne wiki hii, Renamo ilianza kutoa silaha mikononi mwa wapiganaji wake kama sehemu ya mkataba wa amani ambapo baadhi ya wapiganaji hao watajumuishwa kwenye vikosi vya polisi na jeshi.

Zaidi ya wapiganaji 5,200 wa Renamo wanatarajiwa kusalimisha silaha zao kwa serikali.

Wachambuzi wameonya kuwa siku zinazofuata zitakuwa mtihani mkubwa kubaini ikiwa makubaliano hayo yatadumu kabla ya saini ya mwisho ambayo imepangwa kufanyika Jumanne wiki ijayo mjini Maputo.