1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Somalia, yakataa juhudi za Umoja wa Mataifa kuandaa Uchaguzi

15 Aprili 2011
https://p.dw.com/p/10tzB
Rais wa Somalia Sheikh Sharif Ahmed, kushoto, na katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon.Picha: AP

Serikali ya mpito nchini Somalia, ambayo muda wake unaisha mwezi wa nane mwaka huu, ilikataa pendekezo hilo la kuandaa uchaguzi nchini humo utakaoweka madarakani serikali ya kudumu.

Mkutano huo wa siku mbili mjini Nairobi ulilenga kuangalia jinsi nchi hiyo iliyo kwenye pembe ya Afrika, inaweza kujiandaa na kipindi cha mpito. Wafadhili wa serikali wa kimataifa nao wanataka nchi hiyo ifanye uchaguzi. Wawakilishi wa serikali ya Somalia iliyopo Mogadishu, hawakuhudhuria mkutano huo, lakini wanamgambo wanaoiunga mkono serikali na wabunge ndio waliohudhuria.

Taarifa kutoka baraza la mawaziri nchini Somalia jana ilisema mkutano huo haukukidhi matakwa ya Wasomalia. Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Somalia, Augustine Mahiga, aliihimiza Somalia kuandaa uchaguzi, utakaoiweka madarakani serikali ya kudumu, lakini ni vigumu kujua jinsi uchaguzi huo utakavyofanyika kwenye nchi hiyo yenye vurugu.

Somalia imewekwa miongoni mwa nchi zilizosambaratika, na haijawahi kuwa na serikali ya kudumu tangu mageuzi ya mwaka 1991 yaliyomuondoa madarakani dikteta Mohammed Siad Barre. Somalia imegubikwa na vurugu zinazojumuisha, kundi la waasi la al Shabaab lenye, mahusiano na kundi la al - Qaeda, na litalotaka kuondoa madarakani serikali, pamoja na vitendo vya uharamia.

Mjumbe huyo maalamu wa Umoja wa Mataifa, Augustin Mahiga aliwaambia viongozi nchini Somalia kuandaa uchaguzi mwezi Agosti mwaka huu, wakati muda wa serikali iliyopo madarakani unakwisha. Augustin Mahiga alipendekeza kuwepo na uchaguzi wa urais na spika wa bunge mwezi huo wa Agosti.

Somalia Kämpfe in Mogadishu AU Panzer
Majeshi ya Umoja wa Afrika ya kulinda amani nchini Somali wakifanya doria.Picha: AP
Kujiongezea muda

Umoja wa Mataifa upo katika malumbano na baraza la mpito la mawaziri nchini Somalia, lililoongeza muda wake hadi Agosti mwaka 2012, likidai linataka kuhakikisha muendelezo wa kuwazuia wapiganaji nchini humo. Bunge la Somalia pia limejiongezea muda wake kwa miaka mitatu.

Augustin Mahiga amasema mkutano huo ulipendekeza kuongeza mamlaka ya bunge hadi miaka miwili, kuliwezesha kukamilisha shughuli zake, ikiwemo kuandaa uchaguzi. Amesema mkutano huo wa siku mbili ndio mwanzo wa mchakato huo, na wa pili utafanyika karibuni nchini Somali.

Serikali ya Somalia imesema kushiriki kwa spika wa bunge wa nchi hiyo kwenye mkutano huo, ulienda kinyume na matakwa ya bunge. Viongozi wa serikali za mikoa nchini Somalia walihudhuria mkutano huo, pamoja na Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, Umoja wa nchi za Kiarabu na Umoja wa nchi za Kiisilamu.

Katika mpango uliowekwa mwaka 2009, muda wa mamlaka ya serikali ya Somalia na bunge, ulikuwa uishe Agosti 20 mwaka huu, wakati ambapo nchi hiyo ilitakiwa imeshafanya chaguzi, pamoja na kuwa na katiba mpya.

Mwandishi: Rose Athumani

Mhariri: Josephat Charo