1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Syria, upinzani zatofautiana kabla ya mazungumzo

13 Machi 2016

Serikali ya Syria na upande wa upinzani zimetofautiana vikali kuhusu hatima ya Rais wa nchi hiyo Bashar Al Assad huku serikali ikiapa kuwa mjadala kuhusu kuondoka kwake madarakani ni jambo lisilojadilika

https://p.dw.com/p/1ICIn
Syrien Porträt von Baschar al-Assad in Damaskus
Picha: picture-alliance/dpa/Y. Badawi

Upinzani nao umeapa kuwa ni sharti Assad aondoke madarakani akiwa hai au akiwa amekufa. Mvutano huo kati ya pande zinazozana Syria unakuja huku duru nyingine ya mazungumzo ya kutafuta amani nchini humo ikitarajiwa kuanza hapo kesho Jumatatu mjini Geneva.

Mazungumzo hayo yatakayosimamiwa na Umoja wa Mataifa ndiyo juhudi za hivi karibuni za jumuiya ya kimataifa kujaribu kuutafutia ufumbuzi mzozo wa Syaria ambao umedumu kwa zaidi ya miaka mitano na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 270,000.

Serikali ya Syria na kundi rasmi la upinzani zimekubali zitahudhuria mazungumzo hayo ya kutafuta amani baada ya duru iliyopita kukamilika bila ya mafanikio mwezi Februari.

Syrien Außenminster Walid al-Muallim
Waziri wa Mambo ya kigeni wa Syria Walid MuallemPicha: Getty Images/AFP/L. Beshara

Lakini mazungumzo hayo yanatiliwa shaka iwapo yatafanikiwa kutokana na kuibuka mitazamo na misimamo mikali kutoka pande zinazozana kuhusu hatima ya Rais Assad.

Waziri wa mambo ya nje wa Syria Walid Muallem amewaambia wanahabari katika mji mkuu wa Syria, Damascus kuwa hawatafanya mazungumzo na mtu yeyote ambaye anataka kujadii suala la urais na kuongeza Rais Bashar Al Assad ni mstari mwekundu usiopaswa kuvukwa. Muallem amesema iwapo upinzani utaendelea na ajenda hiyo, basi hakuna haja ya wao kuelekea Geneva kwa mazungumzo. Upinzani kwa upande wake umesema sharti Assad aondoke madarakani iwapo kuna nia ya kufikiwa makubaliano yoyote.

Mjumbe mkuu wa upinzani Mohammad Alloush amesema wanaamini kipindi cha serikali ya mpito kinapaswa kuanza tu baada ya kuangushwa kwa Assad au baada ya kifo chake ili mazungumzo ya kutafuta amani yawe na nafasi ya kufanikiwa.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Staffan de Mistura amesema vikao vitakavyofanyika mjini Geneva havitadumu kwa zaidi ya siku kumi zijazo.

De Mistura amesema mazungumzo hayo yanatarajiwa kuangazia kuundwa kwa serikali mpya, katiba mpya na kuandaliwa kwa chaguzi za urais na bunge zitakazosimamiwa na Umoja wa Mataifa katika kipinidi cha miezi kumi na minane ijayo.

Hata hivyo Muallem amesema De Mistura hana mamlaka ya kuibua suala la chaguzi za Rais kwani suala hilo ni haki ya Wasyria pekee kufanya maamuzi.

Staffan de Mistura UN Sondergesandter
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Staffan de MisturaPicha: picture-alliance/dpa/M. Trezzini

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Syria amesema mazungumzo ya Geneva yanastahili kutuama katika kuundwa kwa serikali ya muungano ambayo itateua kamati ya aidha kuandika katiba mpya au kuifanyia mageuzi katiba iliyopo, kisha baada ya hapo kuwepo kura ya maoni ambapo raia wa Syria wataamua mustakabili wao.

Upande rasmi wa upinzani umetaka kuundwe kwa serikali ya mpito iliyo na mamlaka kamili ya uongozi na Allloush amesema matamshi ya Muallem yanaonyesha serikali haijajitolea kuhusu mchakato wa kisiasa.

Suala la iwapo Assad asalie madarakani au la, limekuwa suala tete hata katika duru zilizopita za mazungumzo. Urusi ambayo ni mshirika mkubwa wa utawala wa Assad imepinga mapendekezo ya kiongozi huyo wa Syria kuondoka madarakani kutokana na shinikizo kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.

Marekani na Saudi Arabia ambazo zinayaunga mkono makundi ya upinzani yametoa wito kiongozi huyo ang'atuke madarakani.

Urusi imemtaka De Mistura kuwajumuisha wakurdi wa Syria katika mazungumzo ya kutafuta amani lakini mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa amesema licha ya kuwa hawatashirikishwa katika meza ya mazungumzo, wakurdi wanapaswa kupewa nafasi ya kueleza maoni yao.

Mapigano yamepungua nchini Syria tangu kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano wiki mbili zilizopita. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema ghasia zimepungua nchini humo kwa kati ya asilimi80 na 90 tangu tarehe 27 mwezi uliopita.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Bruce Amani