1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Syria yaukombowa tena mji wa Palmyra

27 Machi 2016

Vikosi ya serikali ya Syria vikisaidiwa na mashambulizi ya anga ya Urusi Jumapili (27.03.2016) vimeukombowa tena mji wa kale wa Palmyra uliokuwa ukishikiliwa ma kundi la Dola la Kiislamu tokea mwezi wa Mei.

https://p.dw.com/p/1IKYw
Wanajeshi wa Syria wakiwa na bendera ya nchi hiyo baada ya kuukombowa tena mji wa Palmyra. (27.03.2016)
Wanajeshi wa Syria wakiwa na bendera ya nchi hiyo baada ya kuukombowa tena mji wa Palmyra. (27.03.2016)Picha: picture-alliance/dpa/TASS/V. Sharifulin

Vyombo vya habari vya taifa na shirika la uangalizi wa haki za binaamu vimesema mji huo wa kale wa miaka 2,000 ambao ni turathi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu,Sayansi na Utamaduni (UNESCO) uko kwenye mikono ya serikali baada ya mapigano makali yaliyodumu kwa wiki kadhaa.

Duru za kijeshi zimeliambia shirika la habari la Ufaransa (AFP) kwamba "baada ya mapigano makali ya usiku jeshi lina udhibiti kikamilifu mji wa Palmyra ikiwa ni mji wenyewe wa kale na vitongoji vya wakaazi wa mji huo."

Shirika la Uangalizi wa Haki za Binaadamu la Syria limesema milio ya risasi ilikuwa bado ikiendelea kusikika Jumapili katika eneo la mashariki ya mji huo lakini wapiganaji wengi wa kundi la Dola la Kiislamu walikuwa wameondoka kutoka mji huo.

Shirika hilo lenye makao yake makuu nchini Uingereza likinukuu duru mbali mbali limesema kwamba wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu katika mji huo walikuwa wameamuriwa kuondoka na uongozi wao ulioko katika mji wa kaskazini -mashariki wa Raqqa.Shambulio la mwisho dhidi ya kundi hilo liliandamana na mashambulizi mazito ya anga ya Urusi na vikosi vya Syria halikadhalika mashambulizi ya mizinga na maroketi.

Mabomu yateguliwa

Wahandisi wamekuwa wakitegua mabomu yaliotegwa na wapigamaji wa jihadi katika mji huo.Televisheni ya taifa nchini Syria iliokuwa ikirusha matangazo yake kutoka mji huo wa Palmyra Jumapili asubuhi imeonyesha mitaa ikiwa mitupu na majengo yalioharibiwa vibaya sana.

Wanajeshi wa Syria wakiwa na bendera ya nchi hiyo baada ya kuukombowa tena mji wa Palmyra. (27.03.2016)
Wanajeshi wa Syria wakiwa na bendera ya nchi hiyo baada ya kuukombowa tena mji wa Palmyra. (27.03.2016)Picha: Reuters/Sana

Duri ya kijeshi imekaririwa ikisema ndege za kivita za Syria na Urusi zimekuwa zikiwashambulia wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu waliokuwa wakikimbia na kuteketeza magari yao chungu nzima katika barabara kuelekea mashariki kutoka mji huo.

Makao makuu ya jeshi la Syria imesema katika taarifa kwamba limerudisha tena usalama na utulivu katika mji huo katika operesheni iliyoonyesha kwamba kundi la Dola la Kiislamu limeanza kurudi nyuma na kusambaratika.

Mapambano hayo ya wiki tatu yaliomalizika kwa ushindi wa serikali yamegharimu maisha ya wapiganaji 400 wa Dola la Kiislamu na wanajeshi 180 wa serikali pamoja na wanamgambo washirika wao .

Ushindi wa ishara

Kukombolewa kwa mji huo utakuwa ushindi wa ishara kwa Rais Bashar al Assad na Rais Vladimir Putin wa Urusi.Ni ushindi wao mkubwa kabisa dhidi ya Dola la Kiislamu tokea kuanzishwa kwa mashambulizi ya anga ya Urusi hapo mwezi wa Septemba ambayo pia yameshuhudia vikosi vya serikali vikiyatenganisha maeneo yanayoshikiliwa na waasi katika mji wa pili kwa ukubwa nchini Syria wa Allepo na barabara muhimu za kusafirisha mahiatji kaskazini mwa mpaka na Ururuki.

Wanajeshi wa Syria wakiwashambulia wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu kwa mizinga Palymra.
Wanajeshi wa Syria wakiwashambulia wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu kwa mizinga Palymra.Picha: picture-alliance/dpa/V. Sharifulin

Jeshi la Syria limeapa kuendeleza ushindi wao huo katika mji wa Palmyra kwa kusonga mbele dhidi ya wapiganaji wa jihadi katika ngome zao nyengine.

Jeshi limesema katika taarifa iliyotolewa na shirika la habari la taifa kwamba "Palmyra yatakuwa makao makuu ya kutanuwa operesheni zao za kijeshi dhidi ya Dola la Kiislamu (Daesh) katika meneo mengine mbali mbali hususan Deir Ezzor na Raqa.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP/dpa/

Mhariri : Sudi Mnette