1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulio la Boko Haram lauwa zaidi ya watu 100

30 Juni 2014

Zaidi ya watu 100 inahofiwa kuwa wameuwawa kaskazini mashariki ya Nigeria kufuatia mashambulizi kwenye vijiji vitatu yanayodaiwa kufanywa na kundi la Waislamu wa itikadi kali la Boko Haram.

https://p.dw.com/p/1CScq
Mripuko uliotokea Bauchi Nigeria unaoshukiwa kufanywa na Boko Haram.
Mripuko uliotokea Bauchi Nigeria unaoshukiwa kufanywa na Boko Haram.Picha: picture-alliance/dpa

Mashambulizi hayo yaliyolenga makanisa matano yalifanyika katika siku ya kwanza ya mfungo wa Ramadhan karibu na mji wa Chibok ambapo Wakristo walivamiwa na kuuwawa wakiwa njiani kuelekea makanisani kwa ajili ya ibada.

Wanamgambo hao baadae waliwashambulia raia katika kitongoji cha jirani cha Kautikari na Guradina na kuyateketeza majengo.

Moses Zakwa mwenyekiti wa chama cha vijana cha Kibaku katika kijiji hicho amewaambia waandishi wa habari kwamba waasi hao walikuwa wakivamia jamii moja baada ya nyengine.Watu ishirini miongoni mwa wale waliouwawa alikuwa akiwajuwa binafsi.

Zakwa amesema binamu yake na mmojwapo wa wajomba zake ni miongoni mwa hao waliouwawa. Ameongeza kusema kwamba mjomba wake huyo alikuwa na wake watatu na watoto zaidi ya ishirini na kwamba shambulio hilo lilianza kama saa mbili asubuhi na lilidumu kwa zaidi ya saa nne.

Shambulio kanisani

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo wa vijana waasi hao waliwafyatulia risasi waumini wakati wa misa kanisani na kwamba watu wengi walikimbilia misituni na kuziacha nyumba zao.

Wanajeshi wa Nigeria.
Wanajeshi wa Nigeria.Picha: AFP/Getty Images

Baadae mwanamgambo mmoja wa eneo hilo amewaambia waandishi wa habari kwamba takriban maiti thelathini zimepatikana nyingi zikiwa kanisani katika kijiji cha Kwada kama kilomita 10 kutoka Chibok kwenye jimbo la Borno. Amekaririwa akisema bado wanaendelea kupekuwa vichaka kutafuta watu waliojeruhiwa au maiti.

Msemaji wa polisi Gideon Jibril amesema maafisa wa serikali hawana idadi kamili ya maafa kutokana na hali ngumu ya mawasiliano katika eneo hilo.

Ongezeko la mashambulizi

Boko Haram imekuwa ikizidisha mashambulizi yake hususan kwa kulenga watu wanaokusanyika kwenye vituo vya kuangalia michuano ya soka Kombe la Dunia.

Mripuko uliolenga kituo cha kuangalia michuano ya soka Kombe la Dunia huko Damaturu, Nigeria.
Mripuko uliolenga kituo cha kuangalia michuano ya soka Kombe la Dunia huko Damaturu, Nigeria.Picha: picture-alliance/AP

Hapo mwezi wa Aprili Boko Haram liliwateka nyara zaidi ya wasichana 200 kutoka kwenye bweni la shule katika mji wa Chibok.Kundi hilo limeuwa zaidi ya watu 2,000 kaskazini mwa Nigeria mwaka huu pekee.

Wakati Boko Haram lilipoanzisha mashambulizi hapo mwaka 2009 waasi hao walikuwa wakiwalenga zaidi Wakristo chini ya kisingizio cha kutaka kuanzisha dola ya Kiislamu.

Tokea mwaka 2013 Boko Haram imekuwa ikiyaelekeza mashambulizi yake kwa vikosi vya usalama vya serikali na raia wa Kikristo halikadhalika wa Kiislamu majumbani, sokoni, hospitalini na katika shule.

Mwandishi : Mohamed Dahman/dpa

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman