1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulio la sumu Syria; 40 wauwawa

Sekione Kitojo
8 Aprili 2018

Shambulio la gesi ya sumu dhidi ya Ghouta mashariki limeuwa dazeni kadhaa za watu, wameripoti watoa huduma za matibabu, na Marekani imesema ripoti hizo kama zitathibitishwa, jumuiya ya kimataifa itoe jibu la haraka.

https://p.dw.com/p/2vg0i
Syrien Luftschläge auf Duma
Picha: picture-alliance/dpa/A. Safarjalani

Taarifa  ya  pamoja  ya shirika  la  kutoa  msaada  wa  matibabu la chama cha  madaktari  wa  Syria  na  Marekani (SAMS) na huduma za  ulinzi wa  raia mashirika  yanayofanya  shughuli  zake  katika maeneo  yanayoshikiliwa  na  waasi, zimesema watu 49 wamefariki katika  shambulio  hilo jioni  ya  Jumamosi. Wengine  wanasema idadi ni   watu  150  ama  zaidi.

Syrien Ost-Ghoua Duma Artilleriebeschuss
Moshi ukifuka baada ya majeshi ya serikali ya Syria kushambulia wilaya ya Douma katika eneo la Ghouta masharikiPicha: picture-alliance/Xinhua/A. Safarjalani

Tangu  kuanza  kwa  mzozo wa  Syria  mwaka  2011, taifa  hilo lililomo  katika  vita, hususan utawala  wa  rais bashar al-Assad, umeshutumiwa  katika  nyakati  kadhaa  kwa  kutumia  silaha  za sumu.

Marekani imeionyooshea  kidole  leo Jumapili  Urusi  kuhusiana  na madai  ya  shambulio  la  sumu mjini  Douma, ngome  ya  mwisho  ya waasi  katika  eneo  la  Ghouta Mashariki, baada  ya  zaidi  ya  watu 80  kuuwawa  katika  mashambulizi  ya  mwishoni  mwa  juma.

Marekani  imesema  iwapo itathibitishwa  Urusi  itawajibika  kutokana na "uungaji  mkono  usioyumba" kwa  utawala  huo. Urusi  inakana kwamba  utawala  wa  Syria  ulitumia  silaha  za  sumu.

Syrien Ost-Ghouta Putin Assad Wandbilder
Mwanajeshi mtiifu kwa rais Bashar al Assad anaonekana katika eneo la Ghouta mashariki.Picha: Reuters/O. Sanadiki

Kiongozi wa  kanisa  Katoliki Papa Francis  leo ameshutumu shambulio  la  gesi  ya  sumu  lililoripotiwa  nchini  Syria  kuwa  ni matumizi ambayo yanayokwenda  kabisa  kinyume  na  sheria  ya "vifaa  vya  maangamizi".

White Helmets, kundi  ambalo  huchukua  hatua  wakiwa  wa  kwanza kutoa  misaada   katika  maeneo  yanayoshikiliwa  na  waasi  nchini Syria, linadai  kwamba  majeshi  ya  serikali  yalitumia "gesi ya  sumu ya  klorini"  katika  mashambulizi, dai  ambalo vyombo  vya  habari vya  dola  vinakana.

Shirika linalopambana dhidi ya matumizi ya silaha za sumu

Shirika  linaloangalia  haki  za  binadamu  nchini  Syria  linaripoti kwamba  darzeni  kadhaa  za  watu  waliathirika  kutokana  na matatizo ya  kushindwa  kupumua kufuiatia  shambulio la  majeshi  ya serikali, lakini  halikutambua  sababu  ya  hali  hiyo.

Shirika  linalopambana dhidi ya matumiziya silaha  za  sumu na  kutaka  kupigwa  marufuku  silaha hizo (OPCW) limesema  limechunguza  mashambulio 70 ya  gesi nchini Syria  tangu  mwaka  2014, kutoka  matukio 370  yaliyoripotiwa.

Syrien UN Waffeninspektoren
Wataalamu wa UN wakikusanya sampuli wakati wakikagua silaha za sumu nchini SyriaPicha: Ammar al-Arbini/AFP/Getty Images

Mwezi  Agosti 2013  majeshi  ya  serikali  yalifanya  mashambulio Ghouta mashariki  na Moadamiyet al-Sham, maeneo yanayoshikiliwa  na  waasi  nje  ya  mji  wa  Damascus.

Upinzani unaushutumu  utawala  wa  nchi  hiyo  kwa  shambulio kubwa  la  gesi  ya sumu. Serikali, ambayo  imekiri  mwaka 2012 kwamba  ina silaha  za  sumu, inakana  madai  hayo.

 

Ripoti  ya  kijasusi  ya  Marekani  inasema  kwa "kujiamini  kabisa" kwamba serikali  ya  Syria  ilifanya  mashambulio  hayo. Inasema watu 1,429 wameuwawa, ikiwa  ni  pamoja  na  watoto 426. Licha ya  kusisitiza kwamba  matumizi  ya  silaha  za  sumu  ni  kuvuka msitari  mwekundu , rais Barack Obama hakuweza  kushambulia syria  kama  jibu  la  matumizi  hayo  ya  gesi  ya  sumu.

Marekani  badala  yake  iliamua  kutumia  diplomasia  na  kuingia katika  makubaliano  na  Urusi  kwamba  inapaswa  kuangalia kwamba hazina  ya  silaha  za  sumu  za  utawala  huo  zinaharibiwa.

Katikati  ya  mwezi  Septemba  ripoti  ya  Umoja  wa  mataifa  ilisema kuna  ushahidi  wa  wazi  kwamba  gesi  ya  sarin  ilitumika.

Wakati  huo  huo  vyombo  vya  habari  vya  serikali  nchini  Syria vinaripoti  kwamba  waasi  katika  eneo  la  Ghouta  mashariki wameomba  kuanza  tena  mazungumzo  ili  kuzuwia  mashambulizi ya  majeshi  ya  serikali  katika  mji  ambao ndio  ngome yao  ya mwisho katika  kitongoji  cha  Ghouta karibu  na  mji  mkuu Damascus.

Syrien Army of Islam Propagandamaterial
Mpiganaji wa kundi la waasi la Army of Islam, "jeshi la Uislamu" akifyatua risasi katika mapambano na jeshi la serikaliPicha: picture-alliance/AP/Army of Islam

Televisheni  inayohusiana  na  serikali  ya  Al-Ikhbariya imeripoti kwamba serikali  imetaka kundi  la wanamgambo  wa  Jeshi  la Waislamu  wawaachie huru  mateka  na  kusitisha  mashambulio yao  dhidi  ya  mji  mkuu  Damascus  kama  sharti  la  kuanza mazungumzo.

Mwandishi : Sekione Kitojo / dpae / afpe / rtre

Mhariri: Oummilkheir Hamidou