1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulio la kigaidi London

Admin.WagnerD23 Mei 2013

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron leo ameitisha kikao cha dharura na wakuu wa kijasusi na kiusalama baada ya washambuliaji wawili kumuua mwanajeshi mmoja kwa kumkata kata kwa mapanga mjini London..

https://p.dw.com/p/18cXo
Shambulio London
Shambulio LondonPicha: Reuters

Waziri mkuu wa Uingereza David  Cameron amesema kuna vidokezo muhimu vinavyoashiria kuwa mauaji hayo yalikuwa kitendo cha ugaidi na washauri wake wakuu watathmini athari za shambulio hilo lilitokea karibu na kambi ya jeshi mjini London.

Cameron amekatiza ziara yake nchini Ufaransa na kurejea Uingereza ili kukutana na kamati ya kiusalama ya kushugulikia mikasa ya dharura ijulikanyao kama COBRA ambayo tayari imeshakutana saa chache baada ya shambulio hilo.

Shada za maua katika eneo la shambulio London
Shada za maua katika eneo la shambulio LondonPicha: Reuters

Mmoja wa washambuliaji hao alionekana katika video iliyorekodiwa na walioshuhududia tukio hilo, akieleza walivyofanya unyama huo na kutamka kulipiza kisasi dhidi ya Uingereza kwa kuhusika  kwa nchi hiyo katika vita dhidi ya mataifa ya kiislamu huku mikono yake ikiwa imejaa damu na kushikilia panga la kukatia nyama.

Mwanajeshi auwawa kinyama

Hata baada ya kumuua mwanajeshi huyo kwa kile walichokitaja kulipiza kisasi,washukiwa hao walisalia katika eneo la tukio na kuwataka wapita njia kuwapiga picha.Mashirika ya habari nchini humo yanaripoti kuwa watu hao wawili kwanza walimgonga mwanajeshi huyo kwa gari kabla ya kumkatakata kwa mapanga.

Washambuliaji hao waliomba radhi kwa kile walichokisema kulazimika kwa wanawake kushuhudia unyama huo lakini mmoja wao alisikika akisema kuwa hiyo ndiyo hali halisi inayoshuhudiwa na wanawake katika  nchi zao za asili, na kwamba wanachokifanya ni kulipiza kisasi,na kuuthibitisha ule msemo wa  jino kwa jino jicho kwa jicho.

Washukiwa hao walipigwa risasi na polisi baada ya shambulio hilo na wamelazwa hospitalini chini ya ulinzi mkali.Bado polisi hawajatangaza jina la mwanajeshi huyo aliyeuwawa wala taarifa kamili kuwahusu washambuliaji hao lakini kulingana na shirika la habari la Reuters  limenukuliwa likisema kuwa duru za kijasusi zinachunguza uwezekano wa wawili hao kutokea Nigeria.

Polisi katika eneo la mkasa
Polisi katika eneo la mkasaPicha: Reuters

Shambulio hilo la hapo jana linakuja mwezi mmoja tu baada ya mashambulio ya mabomu ya mbio za Boston zilizowaua watu kadhaa na kuwajeruhi wengine wengi na kuzua hofu ya kuibuka tena kwa mashambulio ya kigaidi yanayofanywa na watu wasio na mafungamano na matandao wa kigaidi wa Al Qaeda ila walio na itikadi kali.

Kuhusika kwa Uingereza kati vita nchini Afghanistan na Iraq kunaonekana kuzua ghadhabu miongoni mwa makundi ya itikadi kali misimamo mikali nchini Uingereza ambao mara kadhaa wamekuwa wakiwalenga wanajeshi.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/Afp/ap

Mhariri: Saumu Yusuf.