1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulio la Libya ni uhalifu dhidi ya kivita

Amina Mjahid Mohammed Khelef
3 Julai 2019

Jamii ya kimataifa imeendelea kulaani tukio la shambulio la angani lililosababisha vifo vya takriban wahamiaji 40 katika kituo kilichokuwa kikiwashikilia wahamiaji hao nchini Libya.

https://p.dw.com/p/3LXCF
Libyen Tripolis nach dem Luftangriff auf das Tajoura Detention Center
Picha: Reuters/I. Zitouny

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa taifa hilo la Afrika ya Kaskazini, Ghassan Salame, amesema uvamizi huo ni sawa na uhalifu wa kivita, huku Umoja wa Ulaya ukilaani shambulio hilo la kusikitisha. Miili ya watu ilionekana ikitapakaa kote katika eneo la tukio pamoja na soksi na nguo zilizojaa damu za wahamiaji, hii ikiwa ni kwa mujibu wa mpiga picha wa shirika la habari la AFP.

"Shambulizi hili huenda likachukuliwa kama uhalifu wa kivita, maana limewauwa kwa kushtukiza watu wasio na hatia ambao hali mbaya nchini mwao imewafanya kuwa katika makaazi hayo," alisema Ghassan Salame.

Ghassan Salame
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa taifa hilo la Afrika ya Kaskazini, Ghassan SalamePicha: picture-alliance/AP Photo/Thein Zaw

Pia mjumbe huyo ameitolea mwito jamii ya kimataifa kuwaadhibu wale waliyoamuru, kutekeleza na kutoa silaha za shambulio hilo akibainisha kuwa hii ni mara ya pili makaazi hayo kulengwa.

Waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Italia, Enzo Moavero Milanesi, amesema shambulio ni janga jengine linaloonesha athari ya vita kwa raia, huku Ufaransa ikitaka mapigano nchini Libya kusitishwa mara moja.

Naye Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini, Kamishna wa Umoja huo kuhusu mahusiano kati ya umoja huo na nchi zinazonuia kuwa wanachama wake Johannes Hahn na Kamishna wa umoja wa ulaya anayehusika na uhamiaji Dimitris Avramopoulos kwa pamoja wametaka  pia wale walioyotekeleza unyama huo kufikishwa mbele ya sheria.

Msemaji wa huduma za dharura nchini Libya Osama Ali amesema wahamiaji 120 walikuwa wakishikiliwa katika kituo cha hangar kilicholengwa moja kwa moja katika shambulio la jana usiku. Bado waokoaji wanawatafuta manusura katika vifusi vya kituo hicho huku magari ya kubebea wagonjwa yakiendelea kuonekana katika eneo hilo.

Khalifa Haftar alaumiwa kwa shambulio dhidi ya wahamiaji

Huku hayo yakiarifiwa serikali inayotambuliwa kimataifa iliopo mjini Tripoli imelaani kitendo hicho cha kumnyooshea kidole cha lawama mbabe wa kivita Khalifa Haftar.

Libyen General Chalifa Haftar
Mbabe wa kivita nchini Libya Khalifa HaftarPicha: picture-alliance/dpa/M. Elshaiky

Uturuki inayoiunga mkono serikali hiyo imeitaka jamii ya kimataifa kuanzisha uchunguzi juu ya kile ilichokiita vita dhidi ya ubinaadamu.

Khalifa Haftar, anayedhibiti maeneo mengi Mashariki na Kusini mwa Libya mapema mwezi Aprili alianzisha operesheni ya kuutwaa mji mkuu Tripoli.

Hali ya wahamiaji imekuwa mbaya tangu Khalifa Haftar alipoanzisha mashambulizi dhidi ya Tripoli mwezi Aprili na tangu wakati huo mapigano yamesababisha mauaji ya watu 700, watu 4000 wakijeruhiwa za zaidi ya laki moja wamepoteza makaazi yao.

Vyanzo: afp/ap