1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulio la upinde na mshale lawauwa watu watano Norway

Amina Mjahid
14 Oktoba 2021

Raia wa Denmark aliye na miaka 37 anaendelea kuhojiwa na polisi wa Norway, baada ya kuwashambulia watu kwa upinde na mshale katika mji wa Kongsberg na kusababisha mauaji ya watu watano na wengine wawili wakijeruhiwa

https://p.dw.com/p/41fU0
Norwegen | Angriff mit Pfeil und Bogen in Kongsberg
Picha: Terje Bendiksby/NTB/AFP/Getty Images

Polisi nchini Norway imesema kuna dalili zinazoonesha kwamba mshukiwa katika shambulio hilo la upinde na mshale aliingizwa katika siasa kali baada ya hivi karibuni kubadili dini na kuwa muislamu.

Shambulio hilo lililotokea jana usiku katika mji mdogo wa Kongsberg ulio Kusini Mashariki mwa Norway, ulisababisha mauaji ya watu watano huku wengine wawili wakijeruhiwa, wote wakiwa kati ya miaka 50 na 70 hii ikiwa ni kwa mujibu wa polisi.

Hadi sasa polisi imekataa kuondoa uwezekano kwamba hili lilikuwa shambulio la kigaidi lakini haijasema chochote kuhusu nia hasa ya mshukiwa huyo. Picha zilizooneshwa katika vyombo vya habari nchini Norway, zilionyesha mshale mweusi ukutani huku mishale mengine ikiwa imetapakaa sakafuni. 

soma zaidi:Mshambuliaji wa upinde na mshale aua watano Norway

Baada ya shambulio hilo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba ameshitushwa na kusikitishwa na habari hiyo kutoka Norway.

Waziri Mkuu Erna Solberg asema tukio limeitikisa Norway

Norwegen Oslo | Gedenken an die Opfer der Terrroraattacke 2011 in Utoya
Waziri Mkuu wa Norway Erna SolbergPicha: Heiko Junge/AP/picture alliance

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Norway Erna Solberg anayeondoka leo na nafasi yake kuchukuliwa na Jonas Gahr Store ambaye chama chake cha leba kilishinda uchaguzi wa hivi karibuni wa bunge amesema matukio kama haya huwatikisa.

Hansine mmoja ya walioshuudia tukio hilo aliyetambulishwa kwa jina moja tu ameiambia televisheni ya TV2 kwamba alisikia kelele kisha kamuona mwanamke akikwepa kitu na kujificha kabla ya kumuona mshukiwa huyo akisimama katika kona moja akibeba upinde na mishale, baadaye aliona watu wakikimbia akiwemo mwanamke mmoja na mtoto wake mdogo.

Kwa sasa mshukiwa huyo anazuiliwa na polisi na wakili wake Fredrik Neumann, amesema mteja wake anashirikiana vyema na polisi.

Hili ni shambulio baya kutokea katika taifa hilo Scandinavia tangu mtu mwenye siasa kali za mrengo wa kulia Behring Breivik kuwauwa watu 77 mwaka 2011. Tangu wakati huo Norway ilishuhudia shambulio moja tu kutoka kwa mtu aliyejitangaza kufuata itikadi za manazi mambo leo aliyewashambulia watu msikitini kwa kuwamiminia risasi.

Chanzo: reuters/afp/ap