1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulizi la bomu laua watu 30 Nigeria

9 Mei 2014

Watu 30 wameuwawa katika mlipuko wa bomu uliotokea katika daraja linalounganisha Nigeria na Cameroun. Shambulio hilo linatajwa kufanywa na kundi la wanamgambo wa itikadi kali za kiislamu la Boko Haram.

https://p.dw.com/p/1Bwsf
Nigeria Bombenanschlag in Abuja
Picha: picture-alliance/dpa

Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la Punch la Nigeria, bomu hilo lililupuka jana jioni nje kidogo ya kijiji cha Gamboru Ngala ambacho kwa wiki hii tu kimeshuhudia zaidi ya watu 200 wakiuwawa huku wasichana 11 wakitekwa na kundi hilo la Boko Haram.

"Ninaamini kuna watu wengine bado wamefukiwa katika vifusi" mkazi mmoja wa kijiji hicho aliliambia gazeti hilo. Mlipuko huo wa bomu umetokea wakati ambapo mataifa kadhaa yamejitokeza kuisaidia Nigeria kuwatafuta wanafunzi wasichana zaidi ya mia mbili waliotekwa nyara na kundi la Boko Haram wiki tatu zilizopita.

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan amekiri kuongea na baadhi ya mataifa yanayotaka kusaidia kuwatafuta wanafunzi hao. Ikulu ya Marekani imesema maafisa wa kijeshi wa nchi hiyo watawasili Nigeria siku tatu zijazo, pamoja na wataalamu wa mazungumzo na wateka nyara na wataalamu wa uchunguzi wa vinasaba kutoka shirika la upelelezi la nchi hiyo FBI.

Mke wa rais wa Marekani aungana katika kampeni ya kupinga utekaji nyara wa wasichana Nigeria
Mke wa rais wa Marekani aungana katika kampeni ya kupinga utekaji nyara wa wasichana NigeriaPicha: Screenshot/Twitter

Wakatii huo huo kampeni za kushinikiza kundi hilo la Boko Haram kuwaachia wanafunzi hao, zimeendelea duniani kote kwa watu maarufu kuzidi kujitokeza, mke wa rais wa Marekani Michelle Obama amejiunga na mtandao wakijamii unaopinga kitendo cha kutekwa nyara wasichana hao.

"Sala zetu tunazielekeza kwa wasichana wa Nigeria waliotekwa pamoja na familia zao, ni muda sasa wa kuwarudisha watoto wetu" aliandika Michelle Obama chini ya picha aliyotuma katika mtandao huo wa kijamii ambayo ilitumwa pia na zaidi ya watu 48,000.

Ofisi ya Umoja wa mataifa inayoshughulika na masuala ya haki za binadamu imetoa onyo kwa kundi la Boko Haram kwamba watahukumiwa kwa kutenda uhalifu dhidi ya ubinaadamu. Polisi wa Nigeria wameahidi zaidi ya dola laki tatu kwa yeyote atakayetaja mahali walipo wanafunzi hao ambao walitekwa April 14 wakiwa katika mabweni ya shule yao iliyopo Chobok karibu na mjii mkuu wa jimbo la Borno.

Mwandishi: Anuary Mkama
Mhariri: Yusuf Saumu