Shambulizi mjini Berlin: Dunia yatoa rambirambi

Viongozi mbali mbali wa dunia wametoa salamu za rambirambi kwa Ujerumani, kwa watu waliouawa katika mkasa huo wa mjini Berlin ambao unatazamwa kama shambulizi la kutumia lori katika soko la Krismasi.

Katika salamu zake za rambirambi, rais wa Ufaransa Francois Hollande amesema Ufaransa inaomboleza pamoja na Ujerumani katika msiba ambao amesema umeikumba Ulaya nzima. Wizara ya mambo ya ndani ya nchi hiyo imetangaza kuchukua hatua zaidi za kiuslama katika masoko ya Krismasi nchini humo.

Meya wa mji wa Nice Philippe Pradal amesema kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, kwamba kitendo cha kuingiza lori katika ukumbi wa watu mjini Berlin linafanana kabisa na lile lililotokea katika mji wake mwezi Julai na kuuwa watu 86. ''Ni mtindo ule ule wa mashambulizi, ghasia zile zile za kimkumbo, chuki ile ile dhidi ya watu wenye kufurahia maisha'', ameongeza meya huyo katika ujumbe wake.

Rais wa Halimashauri ya Umoja wa Ulaya Jean Claude Juncker, mbali na kuzipa pole familia zilizopoteza wapendwa wao katika shambulizi hilo, amesema inasikitisha zaidi unapotilia maanani kwamba walioshambuliwa walikuwa wamekusanyika katika sherehe za kabla ya Krismasi, ambazo zinawaunganisha watu wengi.

Waziri Mkuu mpya wa Italia Bernard Gentiloni, ameelezea mshikamano na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na nchi nzima ya Ujerumani, katika huzuni iliyosababishwa na shambulio hilo.

Marekani: Tunasimama pamoja na Berlin

#b#Marekani, kupitia msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa katika Ikulu ya White House mjini Washington, Ned Price, imesema inasimama upande wa Ujerumani, katika kile alichokiita, na hapa nanukuu ''Mapambano dhidi ya wale wote wanaotishia jamii yetu'', mwisho wa kumnukuu. Ned Price ameongeza kuwa Ujerumani ni moja ya nchi washirika wakubwa kabisa wa Marekani.

Rais Mteule wa Marekani Donald Trump yeye amekwenda mbali na kuliita tukio la mjini Berlin, ''Shambulizi la kutisha la kigaidi''. Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter, Trump amesema magaidi wa kiislamu wameendelea kuwachinja wakristu, na kutoa wito kwa dunia iliyostaarabika kubadilisha mtazamo wake. Hata hivyo Trump hakutoa maelezo yoyote kuhusu iwapo kipo chanzo chochote kinachothibitisha kuwa magaidi wa kiislamu walihusika katika shambulio la mjini Berlin.

Rais Putin wa Urusi pia ametoa pole kwa Ujerumani, akiyaita mashambulizi ya jana jioni, kuwa yenye misingi ya chuki.

Tunaomboleza waliouawa: Merkel

Muda mfupi baada ya ripoti kutokea kuhusu shambulizi hilo, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, kupitia msemaji wake Steffen Seibert, amesema, Tunaomboleza wale waliouawa, tukiwa na matumaini kuwa waliojeruhiwa watapata msaada.

Rais wa Ujerumani Joachim Gauck ameliita tukio hilo katika soko la Krismasi, jioni mbaya kwa Berlin na kwa nchi nzima ya Ujerumani. Naye waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesema habari mbaya kutoka Kanisa la Makumbusho la Berlin, limempa mtikisiko mkubwa.

Watu wengi kutoka kote duniani wametoa rambirambi zao kupitia mtandao wa Twitter, katika hashtag maalumu za ''PrayforBerlin'', au sala kwa Berlin, na ''Ich bin ein Berliner'', maana yake, mimi ni mkazi wa Berlin, wakirudia kauli ya rais wa zamani wa Marekani John F Kennedy aliyoitoa katika hotuba yake maarufu ya mjini Berlin.

Mwandishi: Daniel Gakuba/DW

Mhariri:Iddi Ssessanga

http://www.dw.com/en/world-leaders-pledge-solidarity-with-berlin-after-christmas-market-tragedy/a-36840501

Maudhui Zinazofanana

Tufuatilie