1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sherehe za kanivali zafikia kilele chake leo

Charo Josephat /DPA23 Februari 2009

Watu takriban milioni moja watazama sherehe hizo

https://p.dw.com/p/GzlS
Sanamu ya kansela Angela Merkel kwenye sherehe za kanivali mjini ColognePicha: AP

Sherehe za kanivali hapa Ujerumani zimefikia kilele chake hii leo. Leo ikijulikana kama Jumatatu ya maua ya waridi, watu takriban milioni moja wameshiriki kwenye sherehe hizo za kanivali.

Kölle Alaaf! Kwa kelele za shangwe na nderemo maandamano ya sherehe za kanivali yameanza asubuhi ya leo mjini Cologne. Muda mfupi kabla ya saa 10.30 zaidi ya watu 10,000 wameshiriki kwenye msafara mrefu wa kilomita 6,5 ulioanzia eneo la Chlodwigplatz kupitia katikati ya mji wa Cologne, mji unaojulikana sana kwa sherehe za kanivali kwenye jimbo la North Rhine Westphalia.

Maelfu ya watu wamevalia mavazi ya ajabu ajabu huku wakisherekea kilele cha sherehe za kanivali chini ya mada mbiu, Unser Fastelovend - himmmlich jeck, yaani sherehe zetu za kanivali za kututia wazimu kiwango cha kutufikisha mbinguni. Watazamaji takriban milioni moja walitarajiwa kuzitazama sherehe hizo za leo za kanivali. Wang Hongmei ni msichana kutoka China aliyehudhuria sherehe za leo za kanivali mjini Cologne.

"Hii ni sherehe kubwa ya kanivali. Watu wote hawa na bia ya Cologne, kanisa kubwa, vyote navifurahia sana. Hakuna jambo kama hili nchini China, lakini hapa kila kitu ni cha kirafiki kwa hiyo nafurahia sana kupigwa busu. Mwaka ujao nikija hapa kwa shereze za kanivali lazima nijifunze lugha ya kijerumani"

Watengenezaji wa magari ya kanivali wa mjini Cologne mwaka huu wamezingatia sana mgogoro wa kiuchumi na wa masoko ya fedha unaoikabili dunia. Kulikuwa na sanamu kubwa ya Marekani, ya Ucle Sam, anayejaribu kuyazuia majumba marefu yasianguke yenye majina ya kampuni za magari na benki za Marekani zilizoathiriwa na mporomoko mkubwa wa kiuchumi.

Chini ya mada 'Sisi ndio mtandao', raia wa Ujerumani wamejenga kwenye gari jingine nyavu ya kumkamata mfanyakazi wa benki aliyesimama bila kuanguka kwenye kamba akiwa hajavaa suruali.

Huku uchaguzi mkuu ukitarajiwa kufanyika mwezi Septemba mwaka huu hapa Ujerumani, kansela wa Ujerumani Angela Merkel pia hakusahaulika kwenye sanamu za leo. Sanamu ya kiongozi huyo ikiwa tu mavazi ya bikini ya rangi za bendera ya Ujerumani, nyekundu, nyeusi na rangi ya dhahabu, ikiashiria matatizo kama vile madeni mapya yanayoikabili Ujerumani na matatizo mengine ya kisiasa.

Mada ya gari ambalo hapo kabla tayari kulikuwa na wasiwasi wa kuzuka mjadala mkali kwa kutaka kuonyesha sanamu ya Angela Merkel akiwa uchi, inasema "Buni mambo mapya kutoka ya kale - kuangazia maeneo ya matatizo."

Reni Molscher, ni mama wa kijerumani ambaye ameandamana na msichana wa kichina Wang Hognmei kwenye shere za leo, na ambaye mumewe anafanya kazi mjini Beijing nchini China. Anaeleza jukumu alilokuwa nalo katika sherehe za leo.

"Hapa nina jukumu la mlinzi anayejaribu kusimamia kila kitu, kuratibu kila kitu, kuchunga kitu chochote kisipotee na kuwa hapa na pale. Kulikuwa na mtihani mdogo wa bia. Kulikuwa na glasi moja ya bia ya Kölsch na moja ya bia ya Pils, na mtu alilazimika kuonja kubaini Kölsch ini ipi na Pils ni ipi. Kulikuwa pia na swali kwa mfano hapa Cologne watu wanasema Kölle Allaf au Kölle Helau?"

Huko mjini Mainz kwa kelele za furaha za 'Helau' kilele cha kanivali kimeanza mwendo wa saa 11.11 asubuhi kwa msafara, huku kukiwa na baridi na hali ya anga isiyopendeza.

Mjini Dusseldorf maelfu ya watu walishiriki kwenye maandamano ya kanivali huku sanamu ya rais wa Marekani Barack Obama akiruka na mabawa yaliyoandikwa maneno Yes we can, ndio tunaweza, huku bara la Ulaya likiwa limeshikilia vazi lake.

Sanamu nyingine ilimuonyesha waziri mkuu wa Urusi, Vladamir Putin akiwa ameshika bunduki ambayo kwenye mtutu wake kunamaneno, Uhuru wa vyombo vya habari wa Putin.

Majira ya kanivali huanza Novemba 11 na kumalizika juma hili kwa sherehe ya kuadhimisha Jumatano ya majivu.