1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sherehe za kanivali zashika kasi

P.Martin14 Februari 2007

Nchini Ujerumani,kila mwaka katika maeneo ya Rhein na Main pirika pirika za kujianda kwa kanivali,huanza rasmi tarehe 11 mwezi Novemba.

https://p.dw.com/p/CHld

Na leo hii sherehe hizo ndio zinashika kasi na kuendelea hadi Jumatatu hasa katika miji kama vile Bonn,Cologne,Düsseldorf,Aachen,Frankfurt au Mainz inayojulikana kama ni ngome za kanivali.

Kitamaduni Kanivali,Fasching au Fastnacht ni wakati wa furaha na sherehe usio na kifani, unaotangulia kipindi cha Kwaresima yaani kipindi cha saumu cha Wakristo.Kanivali haisherehekewi Ujerumani au nchi za jirani za Ulaya tu,bali hata huko Amerika ya Kusini na kwenye visiwa vya eneo la Karibea.”Carnival in Rio” ya nchini Brazil ikiwa maarufu kote duniani.

Lakini kwa hivi sasa tunabakia Ujerumani ambako kuanzia leo Alkhamisi hadi Jumatano ya Majivu, katika miji kama Cologne na Düsseldorf inayojulikana kama ngome za kanivali,mitaa inajaa watu wenye mavazi ya fensi.Siku ya leo,hujulikana pia kama “Weiberfastnacht”-siku ambayo wanawake waliojipamba kwa mavazi ya fensi hujikusanya mbele ya makao makuu ya halmashauri ya jiji na meya wa jiji huashiria kuwapa wanawake hao ufunguo wa jiji hilo.Kuanzia hapo,wanawake wana uhuru wa kufanya wapendavyo kwani leo jiji limo mikononi mwao.Hapo tena wanawake ndio huitumia fursa hiyo,hasa kuwatania polisi na ye yote anaepita njiani.Na wanaume wanaovaa tai leo hii,ndio wanajitafutia balaa,kwani wanawake hutembea na mikasi na ye yote alievaa tai hanusuriki - tai hiyo hukatwa na kijipande tu hubakishwa.Mitaa hujaa watu wenye mavazi ya kila aina kama vile chale,Muhindi Mwekundu, polisi,mtawa au daktari.

Mavazi ya fensi ni biashara kubwa wakati huu wa kanivali,kwani mbali na maduka maalum yanayouza mavazi ya Karneval mwaka mzima,siku hizi,hata maduka ya kawaida huwa na sehemu maalum kwa ajili ya mavazi ya fensi.Baadhi ya watu hulalamika kuwa kanivali sasa imekuwa biashara,kwa vile Siku Kuu ya Krismasi inapomalizika tu,maduka mengi hujazwa mavazi mbali mbali ya fensi kuwavutia washabiki wa kanivali.Na kila mwaka kuna mada fulani:kwa mfano mwaka huu baada ya Ujerumani kushinda Kombe la Mpira wa Mkono,takriban kila mmoja anajibandika masharubu makubwa kufanana na kocha wa timu ya taifa ya mpira wa mkono wa Ujerumani.

Shamrashamra za kanivali zitafikia kilele siku ya Jumatatu inayojulikana kama “Rosenmontag”.Siku hiyo,katika miji kama Cologne,Düsseldorf na Mainz,misururu ya magari ya mashirika mbali mbali yaliyopambwa kwa maua na makaragosi,huandamana kwa sherehe katika mitaa iliyojaa watu ambao hurushiwa peremende,chakleti na maua.Kwa mfano katika jiji la Cologne peke yake,kiasi ya tani 150 za peremende na chakeleti,au kwa jina maarufu “Kamele” hurushwa miongoni mwa watu wanaopiga makelele Kamele….Kamele….Kamele!!!