1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sherehe za kuungana tena Ujerumani zaanza

Kabogo Grace Patricia2 Oktoba 2010

Sherehe hizo za miaka 20 tangu Ujerumani Mashariki na Magharibi zilipoungana tena zimeanza jana katika mji wa Bremen, licha ya kuwepo kwa taarifa za kushtua.

https://p.dw.com/p/PSlO
Nembo ya miaka 20 ya kuungana tena kwa Ujerumani.

Sherehe rasmi za kuadhimisha miaka 20 tangu Ujerumani Mashariki na Magharibi zilipoungana tena zimeanza katika mji wa kaskazini mwa Ujerumani wa Bremen, kabla ya siku rasmi ya muungano wenyewe hapo kesho.

Lakini sherehe hizo zimegubikwa na taarifa za kushtua ambazo zimechapishwa katika gazeti la Ujerumani linaloheshimika la Der Spiegel. Gazeti hilo linadai kugundua nyaraka za siri za serikali ambazo zinaonekana kuonyesha kuwa Ujerumani ililazimika kuitoa mhanga sarafu yake ya Deutschmark kwa ajili ya Euro ili iweze kuungana tena.

Waziri wa zamani wa Fedha wa Ujerumani, Peer Steinbrück ambaye ni kiongozi mwandamizi wa chama cha Social Democrat, amesema katika makala hayo kuwa alizungumza na maafisa wa Ufaransa ambao walithibitisha kuhusu taarifa hiyo. Waziri wa Mambo ya Ndani, Wolfgang Schäuble, mmoja kati ya waasisi wa muungano huo, amesisitiza kuwa kamwe hakukuwa na makubaliano ya aina hiyo.