1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sheria kali za uhamiaji Ujerumani

9 Januari 2016

Kansela Angela Merkel amesema Jumamosi (09.01.2016) kwamba anataka kuwepo kwa sheria kali za uhamiaji nchini Ujerumani baada ya mashambulizi kadhaa ya ngono mjini Cologne na katika miji mengine kulifadhaisha taifa.

https://p.dw.com/p/1Hal8
Kansela Angela Merkel akizungumzia mkutano wa chama chake cha CDU alipokutana na waandishi wa habari. (09.01,2016)
Kansela Angela Merkel akizungumzia mkutano wa chama chake cha CDU alipokutana na waandishi wa habari. (09.01,2016)Picha: picture-alliance/dpa/F.von Erichsen

Akizungumza baada ya mkutano miongoni mwa viongozi waandamizi wa chama chake cha Christian Demokrat (CDU) mjini Mainz Merkel amesema " Kile kilichotokea katika mkesha wa mwaka mpya ni vitendo vya uhalifu vya kukirihisha ambavyo vinahitaji kuchukuliwa hatua kali."

CDU mojawapo ya chama tawala nchini Ujerumani imechukuwa hatua hiyo ya kuimarisha sheria ya waomba hifadhi kufuatia mashambulizi makubwa ya ngono dhidi ya wanawake katika mkesha wa mwaka mpya mjini Cologne.

Chama hicho kimelipa kipaü mbele suala la kuharakisha kurudishwa makwao watafuta hifadhi wanaotenda uhalifu nchini katika mpango wao vipengele kumi juu ya mustakbali wa Ujerumani.

Rasimu ya mpango huo wa CDU inajumuisha sheria mpya ambayo itamvuwa mhamiaji hadhi ya kupatiwa hifadhi baada ya kufanya kosa moja la uhalifu.


Hatua hiyo yumkini ikazusha majibu ya moja kwa moja kutokana na taarifa kwamba baadhi ya wanaume waliokamatwa kuhusiana na udhalilishaji wa kingono mjini Cologne kwa kweli walikuwa ni wahamiaji wanaomba hifadhi ukweli ambao ulifichwa kwa sababu za kisiasa.

Wakimbizi kupoteza haki ya ukaazi

Merkel amesema "iwapo mkimbizi anavunja sheria lazima kuwepo na taathira yake, hiyo ina maana wanaweza kupoteza haki yao ya ukaazi hapa nchini bila ya kujali anakabiliwa na kifungo cha nje au cha gerezani."

Kansela Angela Merkel (kulia) akizungumza na waandishi wa habari. (09.01.2016)
Kansela Angela Merkel (kulia) akizungumza na waandishi wa habari. (09.01.2016)Picha: picture-alliance/dpa/F.von Erichsen

Ameongeza kusema iwapo sheria haikidhi haja hiyo basi lazima ibadiishwe na kusisitiza kwamba kuimarishwa huko kwa sheria sio tu kwa ajili ya maslahi ya raia bali pia kwa maslahi ya wakimbizi walioko nchini.

Chini ya sheria za hivi sasa waomba hifadhi wakipatikana na hatia wanaweza tu kufukuzwa nchini iwapo wamehukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani na isitoshe maisha inabidi yasiwe hatarini iwapo watarudishwa makwao.

Wafuasi wa PEGIDA waandamana

Mamia ya wafuasi wa sera kali za mrengo wa kulia wamejitokeza Jumamosi katika maandamano mjini Cologne kupinga vitendo vya unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake vinavyodaiwa kufanywa na wahamiaji katika mji huo wa Ujerumani magharibi wakati wa sherehe za mkesha wa mwaka mpya.

Polisi ikipambana na wafuasi wa Pegida mjini Köln. (09.01.2016)
Polisi ikipambana na wafuasi wa Pegida mjini Köln. (09.01.2016)Picha: Reuters/I.Fassbender

Wafuasi wa vuguvugu la kundi la PEGIDA lenye kupinga kusilimishwa kwa Ulaya walikuwa wakipiga mayowe ya kutaka kufukuzwa kwa wahamiaji na kebeba mabango yenye ujumbe wakimbizi hawatakiwi.Mwanachama mmoja wa kundi hilo aliuambia ummati kwamba Merkel amekuwa hatari kwa nchi yao na kwamba lazima aondoke kauli yake hiyo ilikuwa ikirudiwa kuitikiwa na umati uliomiminika hapo.

Waandamanaji wa sera za mrengo wa shoto pia walifanya maandamano sambamba na hayo kulipinga kundi hilo la PEGIDA wakiwapigia makelele kwa kuwaita Manazi.

Azimio la Mainz

Hata hivyo mabadiliko yoyote yale ya sheria itabidi yajadiliwe na serikali ya mseto ya Merkel ambayo pia inashirikisha chama cha SPD chenye baadhi ya wanachama ambao tayari wameashiria kupinga marekebisho yoyote yale.

Mkutano wa chama cha CDU mjini Mainz (08.01.2016).
Mkutano wa chama cha CDU mjini Mainz (08.01.2016).Picha: Reuters/K. Pfaffenbach

Mbali na sheria "Mainzer Erklärung" yaani Azmio la Mainz linatowa wito wa kuimarishwa kwa usalama katika maeneo ambayo mashambulizi mingi hutokea kwa mfano kituo cha reli cha Cologne,kuweka kamera zaidi za video na wanausalama kuwakaguwa watu kiholela.

Polisi ya Ujerumani hadi sasa imewatambuwa watuhumiwa 32 ishirini na mbili kati yao ni watafuta hifadhi na kuhusiana na makosa 76 kumi na mbili yakiwa na sura ya dhila za ngono .

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/dpa

Mhariri : Amina Abubakar