1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shimon Peres ameaga dunia

Bruce Amani
28 Septemba 2016

Rais wa zamani wa Israel Shimon Perez ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 93. Peres ambaye hadithi ya maisha yake iliandamana na kuzaliwa kwa taifa la kiyahudi alifariki mapema leo katika hospitali mmoja mjini Tel Aviv

https://p.dw.com/p/2Qg4H
Israel Prortrait Shimon Peres s/w
Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Scheiner

Mwanawe wa kiume Chemi, alithibitisha kifo cha babake kwa wanahabari waliokusanyika nje ya hospitali ambayo Shimon Peres amekuwa akitibiwa kwa wiki mbili zilizopita. Hali ya Peres ilizorota kufuatia ugonjwa wa kiharusi wiki mbili zilizopita, uliosababisha kuvuja damu kwenye ubongo. Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alitoa taarifa akiomboleza kifo cha Peres.

Alisema ataandaa kikao maalum cha Baraza la Mawaziri baadaye leo. Baada ya hapo, kamati maalum itaandaa mipango ya mazishi ambayo wageni wengi mashuhuri wa kimataifa na viongozi wa dunia wanatarajia kuhudhuria.

Maafisa wamesema mwili wa Peres utawekwa katika majengo ya bunge Alhamisi ili kuwapa fursa wananchi kutoa heshima zao za mwisho. Mazishi yake yamepangwa Ijumaa katika Mlima Herzl, eneo la makaburi ya kitaifa mjini Jerusalem.

Norwegen Oslo Friedensnobelpreis für Arafat, Peres und Rabin
Peres alipokea Tuzo ya Amani ya Nobel pamoja na Yasser Arafat na Yitzhak Rabin mjini OsloPicha: picture-alliance/Photoshot

Wakati habari za kifo cha Peres zikienea, salamu za rambirambi zilianza kumiminika kutoka Israel na kote duniani. Rais Barack Obama alimwelezea Peres kuwa mtu aliyejitolea kwa ajili ya Israel.  Alisema mwangaza umezimika, lakini matumini aliyouachia ulimwengu yataendelea kuwaka milele.

Rais wa zamani Bill Clinton na mgombea wa urais wa Democratic Hillary Clinton walisema wamempoteza rafiki wa dhati. Marais wa zamani George H Bush na George W Bush pia walitoa salamu zao za rambirambi. Rais wa Ujerumani Joachim Gauck alisema Peres aliiongoza Israel kuliko mwanasiasa mwingine yoyote. Aliihudumia nchi yake katika majukumu tofauti na misingi imara wakati lilipokuja suala la usalama wa Israel na pia nia thabiti wakati lilipohusika suala la kuendeleza mchakato wa amani na Wapalestina.

Naye waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier alisema Peres ndiye aliyetengeneza mahusiano mazuri kati ya Israel na Ujerumani baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Shimon Perez ambaye pia aliwahi kuwa waziri mkuu mara mbili, ni miongoni mwa kizazi cha mwisho cha wanasiasa walioshuhudia kuzaliwa kwa taifa jipya la Israel mnamo mwaka 1948. Alishinda tuzo ya Nobel kwa pamoja na waziri mkuu Yitzhak Rabin na aliyekuwa kiongozi wa Wapalestina Yasser Arafat kutokana na mchango wake katika mazungumzo ya mikataba ya Oslo, ambayo ilitoa fikira ya kuundwa taifa huru la Palestina.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri:Hamidou Oummilkheir