1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF)

1 Oktoba 2009

Hali ya uchumi yaanza kupambazuka.

https://p.dw.com/p/JvSL
Nembo ya IMFPicha: AP/ DW-Fotomontage

Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF), linatabiri kuwa uchumi wa dunia, umeanza kufufuka,ingawa pole pole kuliko ilivyo desturi. Uchumi wa dunia umejikomboa kutoka msukosuko wake mkubwa kabisa tangu vita vya pili vya dunia na mwakani unatazamiwa kustawi tena ingawa si kwa kasi mno.

Bara la Afrika, linafufuka nalo kutokana na msukosuko wa kupungua kwa maagizo kutoka nchi za nje ya bidhaa zake za malighafi.Dola kuu zinazoinukia kiuchumi-majirani 2 China na India, ndizo zinazotazamiwa kuongoza ukuaji uchumi barani Asia, kwavile, hatua za kuutia jeki uchumi zinaendelea kuhimiza mahitaji ya bidhaa .

Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF), licha ya kutabiri kuwa "baada ya dhiki si dhiki,bali faraji," limeonya itambulike kuwa, kupambazuka huko kwa hali ya uchumi duniani kimsingi, kunatokana na kiinua-mgongo cha michango ya serikali kuimarisha uchumi.Hii ni kwa muujibu wa ripoti ya sehemu ya kwanza ya mwaka ya sura ya uchumi ulimwenguni.

IMF linazindua tutambue kuwa, ununuzi wa bidhaa kwa watu binafsi, bado ni dhaifu,ukosefu wa kazi utaongezeka na kasi ya kustawi uchumi itakuwa ya pole pole zaidi kuliko ilivyokua wakati wa misukosuko iliopita.Makadirio hayo ya sura ya uchumi, ameyatoa mjini Istanbul,Uturuki,mtaalamu mkuu wa kiuchumi wa Shirika hilo la IMF ,Olivier Blanchard.

Alionya pia kuwa tarakimu za hivi sasa ,zisizihadae serikali kudhani msukosuko umeshapita,la hasha.Kwa jumla, alisema Blanchard, uchumi jumla wa dunia, utapungua kwa kima cha 1.1 % mwaka huu kabla kwa kima cha 3.1% mwaka ujao wa 2010.

Barani Asia, gurudumu la kusukuma mbele ukuaji wa uchumi, litazungushwa na majirani 2 -India na China,kwavile , hatua zao za kuutia jeki uchumi zinapalilia mahitaji ya ununuzi wa bidhaa zao . Upepo wa kukua uchumi , utavuma barani Asia katika kipindi cha pili cha mwaka huu wa 2009 na kujenga msingi wa kukua kwa wastani kwa uchumi huko mwakani 2010.Uchumi wa China , utakua kwa kima cha 8.5 mwaka huu,ukiwa umeteremka kutoka kima cha 9 % cha mwaka jana. Uchumi wa India, utakua kwa kima cha 5.4%,kutoka 7.3 % mwaka uliopita.

Bara la Afrika nalo linajikomboa kutoka msukosuko huo wa uchumi ambao uliathiri mahitaji ya bidhaa zake za malighafi inazozasafirisha n'gambo mwaka huu.IMF imeonya hatahivyo, kuwa, umasikini unaweza ukaongezeka zaidi ikiwa hali ya kustawi tena kwa uchumi ikienda pole pole zaidi kuliko ilivyotazamiwa.

Msukosuko wa uchumi uliliathiri zaidi dola kuu la kiviwanda -Afrika Kusini,ambayo uchumi wake umeshikamana sana na masoko ya fedha ya dunia.Ripoti ya IMF inabashiri kuwa,uchumi wa Afrika kwa jumla, utakua kwa kima cha 4% mwakani 2010 baada ya kudofika na kuanguka hadi 1.7% mwaka huu.

Muandishi : Ramadhan Ali /DPAE

Mhariri: O.Miraji