1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shirika la kutetea haki za waandishi lalaani mashambulizi.

8 Januari 2008
https://p.dw.com/p/Cmba

Nairobi. Shirika linalotetea haki za waandishi , la waandishi wasio na mipaka leo limeshutumu shambulio dhidi ya waandishi habari wawili nchini Tanzania ambao wamepigwa na mwingine kumwagiwa tindikali machoni.

Shirika hilo lenye makao yake makuu mjini Paris limesema kuwa watu hao waliwashambulia Saeed Kubenea, mchapishaji wa gazeti la kila wiki la Kiswahili la Mwanahalisi, na mhariri wake Ndimara Tegambwage katika ofisi zao mjini Dar es Salaam.

Gazeti la Mwanahalisi linafahamika kwa ripoti zake za uchunguzi. Waandishi wasio na mipaka limesema kuwa shambulio hilo lilikuwa ni jaribio la kuwanyamazisha waandishi hao, ambao gazeti lao limesaidia hapo kabla kufichua kashfa kadha nchini humo. Shirika hilo la kutetea haki za waandishi limesema kuwa shambulio hilo la kinyama lililotokea siku ya Jumamosi , linasikitisha hususan kwa kuwa limetokea katika nchi ambayo kwa kawaida haina utamaduni wa kutumia nguvu kuwanyamazisha waandishi. Haijafahamika nani anahusika na shambulio hilo na polisi wanachunguza. Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete, ambaye pia amekuwa akishutumiwa na gazeti hilo kwa rushwa, ameshutumu shambulio hilo kuwa ni la kinyama.