1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

110209 Entwicklungsländer DEG

Charo Josephat 12 Februari 2009

Licha ya changamoto za kuporomoka kwa uchumi wa dunia shirika la DEG litaendelea kufadhili miradi ya maendeleo

https://p.dw.com/p/GsVb
Winfried Polte wa shirika la DEGPicha: DEG

Licha ya kuporomoka kwa uchumi wa dunia, shirika la uwekezaji na utoaji misaada ya kimaendeleo la Ujerumani, DEG, bado linalichukulia jukumu la kufadhili miradi ya uwekezaji kuwa na umuhimu mkubwa katika nchi zinazoendelea na zinazoinukia haraka kiuchumi duniani. Tangu kuanzishwa kwake mnamo miaka 45 iliyopita, shirika la DEG, linakabiliwa na changamoto kubwa wakati huu wa kuporomoka kwa uchumi wa dunia. Hata hivyo mwaka uliopita shirika hilo lilifaulu kupata faida.

Swali ambalo lazima lijitokeze ni kwamba shirika la DEG ni tawi la benki ya maendeleo ya Ujerumani, ambayo ilipoteza mabilioni ya fedha kutokana na kuporomoka kwa uchumi. Je ni kwa umbali gani shirika hilo liliathiriwa.

Winfried Polte, msemaji wa shirika la DEG anasema, "Hatuna fedha za kugawa. Sisi ni shirika linalotaka kujipatia faida zake kutegemea hali jumla ya shirika hili. Ingawa faida yetu mwaka huu haikuwa kubwa sana, kutakuwa angalau na matumaini kidogo. Lakini hata hivyo tunaweza kuendeleza shughuli zetu bila matatizo yoyote."

Kwa kiwango cha ahadi ya yuro bilioni 1,2 shirika la DEG lilifaulu kupata faida ya asilimia 1,6 katika mwaka uliopita wa 2008 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia 2007.

Kiwango jumla cha ahadi za fedha kiliongezeka kufikia yuro bilioni 4,4 mwishoni mwa mwaka jana. Changamoto za kikanda zilijitokeza upya barani Asia kwa mapungufu ya takriban yuro 450, ikifuatiwa na Amerika Kusini, Ulaya na Afrika.

Msemaji wa shirika la DEG, Winfried Polte, anasema, "Kudhamini uwekezaji wa kibinafsi barani Afrika ni jambo ambalo kwa kulifahamu umuhimu wake, limetukaa moyoni mwetu. Mwaka uliopita 2008 tumewekeza yuro milioni 179 barani Afrika na kwa njia hiyo kujipatia faida ya kufurahisha kama ilivyokuwa mwaka 2007. Nchini Kenya kwa mfano tumedhamini kiwanda cha kwanza cha kibinafsi cha kutengeneza nishati inayotokana na chemichemi za maji; na kwa njia hiyo tumetoa mchango wetu katika kuyalinda mazingira utakaolisadia eneo hilo."

Changamoto muhimu ya mwaka uliopita kwa shirika la DEG ni kuimarika kwa sekta za fedha katika mataifa shirika. Ahadi za fedha zililingana na kiasi cha yuro milioni 487 hiyo ikiwa ni faida ya takriban asilimia 40. Benki za biashara zilikuwa miongoni mwa mashirika yaliyopata ufadhili. Kuhusiana na vipi kuporomoka kwa uchumi kulivyoziathiri nchi zinazoendelea na zinazoinukia haraka kiuchumi, Winfried Polte, anasema bara la Afrika liko katika nafasi maalum.

"Kwa ujumla mtu anaweza kusema, kwa kuwa bara la Afrika halijajumulishwa sana katika masoko ya fedha ya kimataifa, halikuathiriwa sana na kuporomoka kwa uchumi wa dunia kulinganisha na nchi nyingine. Pamoja na hayo unaweza kusema, kwa kuwa kama inavyojulikana Afrika hupokea kiwango kikubwa cha misaada, kwa njia hiyo kulikuwa na kiwango cha kati cha ufadhili wa uwezekaji. Kwa upande lakini mwingine Afrika imeathiriwa na kushuka kwa bei za malighafi."

Mbali na sekta ya fedha, shirika la DEG pia hudhamini uwekezaji katika sekta ya viwanda, kampuni binafsi za kujenga miundombinu na miradi ya kilimo na ya utoaji misaada ya chakula.